Pages

Wednesday, January 21, 2015

WAFANYABIASHARA JIJINI MBEYA WAANDAMANA HADI MAHAKAMANI WAKISHINIKIZA MWENYEKITI WAO AACHIWE



Wafanyabiashara  wanaondesha shughuli zao za kibiashara katika masoko zaidi ya  matano yaliyopo Jijini Mbeya wakiwa kwenye maandamano kuelekea mahakamani wakishinikiza mahakama hiyo kumuachia huru, Mwenyekiti wa Soko la Soweto  Honola Mbogella ambaye alifikishwa mahakamani hapo na halmashauri ya jiji la Mbeya kwa tuhuma za kuzuia watumishi wa umma kufanya kazi zao.
Wafanyabiashara  wanaondesha shughuli zao za kibiashara katika masoko zaidi ya  matano yaliyopo Jijini Mbeya, wakiwa nje ya mahakama ya Mwanzo ya Mbeya mjini wakishinikiza Mwenyekiti wa Soko la Soweto kuachiwa huru.

Baadhi ya maduka yakiwa yamefungwa



MWENYEKITI wa Soko la Soweto jijini Mbeya,  Honola Mbogella amefikishwa katika  mahakama ya Mwanzo Mbeya mjini kwa tuhuma za kuzuia watumishi wa umma kufanya kazi zao.

Kufuatia kukamatwa kwa Mwenyekiti huyo kulisababisha zaidi  ya wafanyabiashara 1000 wanaondesha shughuli zao za kibiashara katika masoko matano yaliyopo Jijini Mbeya, kuandamana na kuizunguka mahakama ya Mwanzo yaMbeya mjini, wakishinikiza mahakama hiyo kumuachia huru.

Mwenyekiti huyo amefikishwa katika mahakama ya Mwanzo ya Mbeya mjini leo na kesi yake kusikilizwa majira ya saa tatu asubuhi  ambapo kesi hiyo ilivuta hisia za watu kutokana na kundi hilo la wafanyabiashara kuizunguka mahakama hiyo, huku jeshi la polisi likilazimika kuimarisha ulinzi.

 Akisomewa mashitaka hayo Mbele ya Hakimu wa Mahakama ya mwanzo ya Mbeya Mjini Ubaswege Mathew, karani wa Mahakama hiyo, Sioni Kasunga alisema mtuhumiwa huyo alifanya kosa hilo January 10 mwaka huu akiwa katika eneo lake la kazi la soko la
Soweto lililopo Jijini Mbeya. Alisema kwa mujibu wa kifungu kidogo cha sheria namba 101(a) sura ya 288 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, mtuhumiwa aliwazuia watumishi wa umma wa halmashauri ya Jiji la Mbeya kufanya kazi yao ya kukusanya ushuru.

 Alisema, mtuhumiwa aliwazuia wafanyabiashara hao kugoma kutozwaushuru wa shilingi 200 hadi 300 na halmashauri ya Jiji la Mbeya kwa maelezo kwamba licha ya wafanyabiashara hao kulipia tozo hiyo kwa kipindi kirefu bado soko hilo limeendelea kukithiri kwa uchafu.

 Aidha, kutokana na kosa hilo, Hakimu wa mahakama hiyo, Ubaswege Mathew baada ya kusikiliza maelezo hayo alitoa nafasi kwa mtuhumiwa ambaye alikana shitaka hilo hivyo, hakimu kuhairisha kesi hiyo mpaka kesho na na kusema kuwa dhamana kwa mtuhumiwa ipo wazi.

 “Kesi  hii nimeihairisha mpaka kesho asubuhi, mtuhumiwa anahaki ya kuwekewa dhamana kwa masharti ya kiasi cha fedha cha shilingi milioni mbili na wadhamini wawili mmoja akiwa ni mtumishi wa serikali,”alisema Wakati kesi hiyo ikiendelea mahakamani hapo, umati mkubwa wa wafanyabiashara wanaoendesha shughuli zao katika masoko matano ya Soweto,Uyole, Mabatini, Sokomatola na Uhindini ulijitokeza na kuizunguka mahakama hiyo kwa kile walichokidai kwamba wenyekityi huyo ameonewa. 

Wakizungumza na Mbeya yetu nje ya mahakama, wafanyabiashara hao ambao waligoma kutaja majina yao, walisema wao wamegoma kulipa ushuru huo kutokana na halmashauri kushindwa kuetekeleza majukumu yao ya ukarabati wa miundombinu pamoja na usafi wa mazingira hivyo Mwenyekiti huyo hausiki na  suala la kuwashawishi kugoma kama inavyodaiwa na halmashauri.

Hata hivyo, wafanyabiashara hao wamegoma kuendelea na shughuli zao mpaka suala hilo litakapo patiwa ufumbuzi kwa halmashauri kurekebisha miundombinu na usafi wa mazingira katika maeneo yabiashara.

Na Mbeya yetu
   

No comments:

Post a Comment