Pages

Thursday, February 19, 2015

CHADEMA YAWAPIGA "STOP" WANAOTAKA KUWANG'OA LEMA NA NASSARI



Mwenyekiti wa Chadema taifa, Freeman Mbowe akiwa pamoja na Mbunge Joshua Nassari (kushoto) na Godbless Lema (kulia) katika moja ya mikutano ya chama hicho. Picha ya Maktaba 

Chama cha Demokrasia na Maendeleo(chadema), mkoa wa Arusha “kimewapiga stop” wanachama wake, kutangaza nia ya kugombea ubunge katika majimbo matatu, yanayoshikiliwa na wabunge wa chama hicho,hadi hapo Bunge litakapovunjwa rasmi julai 2 mwaka huu.
Majimbo hayo ni jimbo la Arusha mjini, mbunge wake, Godbless Lema, Jimbo la Arumeru Mashariki, mbunge Joshua Nassari na Jimbo la Karatu mbunge, Mchungaji Israel Natse ambapo tayari kuna    wanachama wa chama hicho, wameanza kutangaza nia   za kuwang’oa wabunge hao.
Akizungumza na mwananchi leo, Katibu wa Chadema mkoa wa Arusha, Calist Lazaro alisema, maagizo anayoyatoa ni kutekeleza utaratibu ambao umetolewa na Kamati Kuu ya chama hicho,kuhusiana na uchaguzi mkuu ujao.


“Naomba hapa ieleweke kuwa hatuzuwii mtu kugombea lakini tunataka afuate taratibu ili kuzuia vurugu na kama mtu akikiuka sasa ina maana atakuwa amepoteza sifa”alisema Lazaro.
Lazaro alisema nia ya agizo hilo ni kuondoa vurugu na mpasuko ndani ya chama kabla ya wakati muafaka wa kutangaza nia na kuanza kampeni haujafika, lakini kwa majimbo yaliyo na wabunge wa CCM, wagombea wanaruhusiwa kutangaza nia.
Alisema  chama hicho,  kitatoa ratiba ya uchaguzi karibuni na  fomu za kugombea  nafasi mbali mbali zitapatikana katika ofisi za chama hicho, katika ngazi zote ila kwa maeneo yenye wabunge na madiwani wa chadema, fomu zitapokelewa bila kutangaza nia na kuanza kampeni.
Tamko hilo limekuja kukiwa na mpasuko mkubwa ndani ya Chadema katika majimbo hayo matatu, kutokana na idadi kubwa ya makada wa chama hicho, kuanza kunyemelea majimbo hayo.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment