Wakati Taifa likipita katika kupindi kigumu cha kupima
uadilifu wa viongozi, wengine wakijiuzulu na kuendelea kulalamika, NIPASHE
imefanikiwa kupata barua ya kujiuzulu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Ali
Hassan Mwinyi, ikithihibitisha jinsi kiongozi huyo alivyo juu kwa viwango vya
utiifu na uadilifu.
Katika barua hiyo ambayo inasambazwa kwenye mitandao kwa
sasa, inaonyesha jinsi Mwinyi alivyojiuzulu kwa unyenyekevu Januari 22, 1977
wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Ndani.
Kiongozi huyo ambaye mwaka 1985 alikuja kukwea tena ngazi
kuwa Rais wa pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika barua
aliyomwandikia Rais wake, Mwalimu Julius Nyerere, anaeleza jinsi binafsi
alivyoguswa na mauaji ya watu wanaoshukiwa kuwa wachawi katika mikoa ya
Shinyanga na Mwanza mwaka 1975.
Kwa maneno yake Mwinyi alisema: “Kisiasa nakiri kuwa
nahusika, siwezi kukwepa kwa sababu dhamana yangu ya uwaziri inaambatana na
wajibu unaonitaka nijue yanayotendeka wizarani na pia niweze kudhibiti na
kuhakikisha mwenendo mwema wa Jeshi la Polisi.”
Mwinyi alijikuta katika matatizo hayo baada ya Jeshi la
Polisi kuendesha operesheni ya kusaka wauaji wa wachawi katika mikoa ya Mwanza
na Shinyanga, na alikiri kwamba:
“…vyombo vinavyohusika na utekelezaji, polisi ikiwemo,
vilivuka mipaka ya wajibu wao na vikajipa madaraka ya kuogelea katika vitendo
viovu vya kishenzi, kinyama na kikatili hata baadhi ya watu waliokamatwa kwa
kushukiwa tu kwamba wanahusika wakafa na wengine wakapata vilema vya kudumu.”
Ingawa Mwinyi aliweka bayana kwa bosi wake, Mwalimu Nyerere,
kwamba kijinai asingehusika kwani hakushiriki wala kushauri, kuagiza wala
kuelekeza mambo hayo yafanywe hivyo, aliandika barua isiyo na kinyongo kabisa
na yenye unyenyekevu mkubwa kwa Rais Nyerere.
Kwa unyeyekevu mkubwa, Mwinyi alisema: “Kwa hiyo, Mwalimu,
nakuomba mambo matatu. Kwanza naomba radhi mimi nafsi yangu na pia naomba radhi
kwa niaba ya askari wote walio wema. Pili, naomba vilevile uelewe sehemu yangu
katika kosa hili. Tatu, kwa fedheha hili, naomba unikubalie kujiuzulu.”
Kupatikana kwa barua ya Mwinyi ya kujiuzulu na kuwekwa
hadharani inaweka mizania mpya kabisa ya uadilifu katika uwajibikaji wa
viongozi wa umma wanapoingia matatani na kutakiwa kujiuzulu.
Miongoni mwa viongozi wakuu waliowahi kujiuzulu katika miaka
ya hivi karibuni ni pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Serikali ya
Awamu ya Nne, Edward Lowassa, pamoja na mawaziri wawili waliopata kusimamia
Wizara ya Nishati na Madini kwa nyakati tofauti za utawala wa awamu hiyo, Dk.
Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi.
Viongozi hao, ingawa barua zao za kujiuzulu kwa Rais Jakaya
Kikwete hazijapata kuwekwa hadharani, lakini kwa kauli na maelezo yao bungeni
wakati wanatangaza kujiuzulu walionyesha kuwa walionewa tu kufikishwa katika
hatua hiyo.
Kwa mfano, Lowassa alisema wazi “ameonewa na kudhalilishwa
sana” kuhusu suala la mkataba tata wa kuzalisha umeme wa dharura ambao
ulitolewa kwa kampuni feki ya Richmond.
Tangu kujiuzulu kwa Lowassa na wenzake wawili, umezuka
mpasuko mkubwa miongoni mwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), vita
ikipiganwa kuonyesha kwamba kujiuzulu kwa viongozi hao ulikuwa ni uonevu.
Mivutano hiyo ya wabunge ndiyo ilifanya hata Halmashauri Kuu
ya CCM kuunda kamati ya wazee watatu wa busara ikiongozwa na Ali Hassan Mwinyi
na wajumbe ni Spika wa zamani wa Bunge la Afrika Mashariki, Abdulrahman Kinana
na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Pius Msekwa, kusaka suluhu ya uhasama huo.
Wakati kamati hiyo ikiendelea na kazi ya kusaka suluhu ya
uhasama huo, suala la Richmond ambalo ni chimbuko la kujiuzulu kwa viongozi hao
watatu, limezidi kuwa tete kila kukicha, zaidi likijitokeza katika makundi ya
wapinga ufisadi na wale wanaolezwa kuutetea.
Kwa barua ya Mwinyi ambayo gazeti hili limeamua kuichapisha
ilivyo kwa nia ya kuamsha uadilifu unaofanana na kiongozi huyo wa awamu ya
pili, ni fursa nzuri sasa kwa viongozi wote wa umma wanaoachia ngazi si tu
kukubali kuachia ngazi, ila kuishi maisha yanaoonyesha kwamba hawana kinyongo
na hatua waliyochukua.
Mzee Mwinyi kwa maudhui ya barua yake ya mwaka 1977 haikuwa
jambo la ajabu kuja kuwa Rais wa Tanzania miaka minane baadaye, huku akionekana
kama kiongozi aliyeshinda vishawishi na kila aina ya hila kwenye uongozi wake.
IPP NIPASHE: Uadilifu wa Mzee Mwinyi huu hapa, Oktoba 24,
2009
No comments:
Post a Comment