Dar es Salaam. Licha ya baadhi ya watu kubeza
uteuzi wake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda ameapishwa leo
jijini Dar es Salaam na kusema kuwa atatekeleza majukumu yake kwa mtindo
alioupa jina la STK, akimaanisha atafuata Sheria, Taratibu na Kanuni.
Huku akiwa ameambatana na mkewe, Makonda amesema
kazi yake ni kumsaidia kazi Rais Jakaya Kikwete tu si mtu mwingine,
kusisitiza kuwa hakuwahi kufikiria kuwa kuna siku atateuliwa kuwa mkuu
wa wilaya.
Wakati Makonda akieleza hayo, Mkuu wa Mkoa wa Dar
es Salaam, Said Meck Sadiki ametaja sababu nne zilizomfanya Rais
Kikwete kumteua mkuu huyo wa mkoa na kusisitiza kuwa kwa kazi
alizokwisha fanya, alistahili kuteuliwa muda mrefu.
Mkuu huyo wa wilaya ambaye ni Katibu wa Chipukizi
na Uhamasishaji wa UVCCM aliapishwa jana katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa
Dar es Salaam, kabla ya kuanza kwa kikao cha Kamati ya Ulinzi na
Usalama ya mkoa huo. Baada ya kuapishwa aliingia katika kikao hicho
akielezwa kuwa ameshakuwa mjumbe rasmi.
Makonda ni kati ya wakuu wa wilaya wapya 27
walioteuliwa na Rais Kikwete takribani wiki moja iliyopita. Mbali na
uteuzi huo, rais Kikwete aliteungua uteuzi wa wakuu wa wilaya 12 na
kuwabadilisha vituo vya kazi wengine 64.
Akizungumza mara baada ya kuapishwa Makonda
amesema, “Namshukuru Mungu kwa kumpa Rais Kikwete macho ya kuniona na
hatimaye kuniteua kuwa mkuu wa wilaya.”
Amesema, “Aliniona nafaa ndiyo maana alifanya hivyo. Sikuwahi kufikiria kama kuna siku nitateuliwa kuwa mkuu wa wilaya.”
Akieleza mambo mawili muhimu atakayoyafanya
alisema, “Kwanza, nafasi niliyopewa ni mpya na ni tofauti na ile ya
ubunge. Mbunge anachaguliwa na wananchi ila hii yangu ni ya kuteuliwa.
Nimepewa nafasi hii kumsaidia kazi Rais Kikwete si mtu mwingine.
Nitafanya kile ambacho kinatakiwa kufanywa na mkuu wa wilaya.”
Akieleza jambo la pili alisema, “Nitafanya kazi
kwa mtindo wa STK; yaani nitafuata sheria, taratibu na kanuni.
Ninafungua milango kwa watu wote, wakiwemo wananchi wa wilaya ya
Kinondoni.”
Kabla ya kuanza kutaja sifa nne za Makonda, Said
Meck Sadiki alisema, “Mengi yamesemwa baada ya rais kukuteua. Ila kwa
jinsi ninavyokufahamu ulitakiwa kuwa mkuu wa wilaya kabla ya uteuzi
huu."
Amesema sifa ya kwanza ya Makonda ni uongozi
alionao ndani ya UVCCM, kwamba alipewa kwa sababu ni mtendaji kazi
hodari na pia umemfanya awe na uzoefu.
“Pili, Makonda ni msomi mzuri sana katika hilo
hakuna mwenye shaka kabisa. Tatu, umekuwa mjumbe wa Bunge Maalum la
Katiba. Huwezi kuteuliwa kuwa mjumbe wa Bunge hili kama hauna uwezo,
watu walikupima na kukuona kuwa uko vizuri na una uwezo mzuri tu,”
amesema.
No comments:
Post a Comment