Dustan Shekidele, Morogoro
DADA wa msanii mkongwe wa muziki wa Bongo Fleva, Seleman
Msindi ‘Afande Sele’ Zaria Kambi (30) ambaye alikuwa ni mhudumu wa baa,
amekutwa ameuawa kikatili katika Gesti ya Stavi (Gesti ya Marafiki) iliyopo
Kichangani, mjini Morogoro.
Tukio hilo la kinyama lilitokea usiku wa Jumapili iliyopita
baada ya marehemu kuwa amekubaliana kulala pamoja na mteja aliyekuwa
akimhudumia
kinywaji, ambaye pia alikuwa amechukua chumba katika nyumba hiyo
hiyo iliyokuwa na baa.
Kwa mujibu wa rafiki wa marehemu, ambaye pia alikuwa ni
mhudumu wa gesti hiyo, Rehema Saleh, alisema mtu mmoja asiyefahamika, alifika
kazini kwao na kupanga chumba namba 8A na baadaye alienda upande wa baa kunywa
pombe akihudumiwa na Zaria.
“Mimi na Zaria (pichani) tunaishi jirani, sasa baada ya
kumhudumia na yeye kununuliwa pombe, wakakubaliana walale pamoja, tunaishi jirani hivyo kila siku baa ikifungwa
tunaongozana na jana tuliongozana njiani aliniambia amepata kichwa hivyo
anakwenda nyumbani kuaga na baadaye arejee kwa bwa’nake huyo ambaye ni mara ya
kwanza anaonana naye,” alisema Rehema na kuongeza.
“Cha ajabu saa 8 usiku napigiwa simu na mlinzi akidai Zaria
amenyongwa na mteja wake, sikuwa na jinsi, kulipokucha nilifika hapa gesti na
kukuta mwili wa marehemu ukiwa kitandani,” alisema na kuangua kilio.
Chumba cha Gest alichokutwa amekufa Zaria Kambi.
Mlinzi wa gesti hiyo,
John Emmanuel akizungumzia tukio hilo, alisema majira ya saa 6 usiku Zaria
aliingia katika chumba namba 8A na saa moja baadaye, akasikia kelele zikitoka
chumbani humo, ambazo alihisi ni za kimapenzi.
“Sijakaa vizuri saa 8 usiku jamaa alitoka na begi lake
akitaka nimfungulie aondoke huku mkononi akiwa na tiketi ya basi kuelekea
Mbeya, nikamwambia kwanza twende chumbani kwake nikachunguze ndipo nimruhusu
atoke, awali aligoma na mimi nikagoma kumfungulia geti, tukaganda kama dakika
mbili akakubali kwenda chumbani tulipofika tukamkuta Zaria amekufa huku akiwa
mtupu, nikamjulisha bosi Pascal Mafikiri ambaye aliita polisi wakamchukua
mtuhumiwa na mwili wa Zaria,” alisema.
Mama mzazi wa marehemu, Mwajuma Hassani Kambi ambaye ni
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mwande Kata ya Kichangani kwa tiketi ya Chadema
alipokea taarifa za kifo cha mwanaye Jumapili usiku.
Alisema mwanaye ameacha mtoto anayeitwa Rashid lsmail
Kaliembe ambaye anasumbuliwa na uvimbe tumboni na kwamba kila mwezi alikuwa
akipelekwa Muhimbili kwa matibabu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba mtuhumiwa, Erick Bruno, ambaye
ni mkazi wa Manzese Tip Top Dar es Salaam, anashikiliwa. Marehemu huyo alizikwa
Jumanne iliyopita mjini Morogoro.
No comments:
Post a Comment