Pages

Monday, February 2, 2015

Mbunge CCM amvaa Pinda


Mbunge wa Bukoba Mjini kwa tiketi ya CCM, Khamis Kagasheki amemtuhumu Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwa ndiye aliyekuza mgogoro wa Bukoba uliosababisha madiwani wa halmashauri kushindwa kufanya vikao, akidai kuwa mtendaji huyo mkuu wa Serikali ameshindwa kuchukua hatua. Pinda hakuweza kupatikana, lakini msemaji wake alisema Waziri Mkuu ameshalishughulikia suala hilo kwa kiasi kikubwa.
Tuhuma hizo za Kagasheki ni za nadra kwa mbunge huyo wa chama hicho tawala kuelekeza kwa mtendaji mkuu wa Serikali na mmoja wa wajumbe wa vikao 



vya juu vya CCM.
Kagasheki, ambaye alikuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, alitoa tuhumu hizo wakati wa mahojiano maalumu na gazeti hili wiki iliyopita, akisisitiza kuwa ni makosa kuutazama mgogoro huo kuwa ni kati ya yake na meya na akataka ijulikane kuwa kinachoendelea Bukoba ni suala la wizi.
Mgogoro huo wa kisiasa, ambao umedumu kwa takriban miaka miwili na unaotishia kugawanyika kwa CCM, umekolezwa na kufunguliwa kwa kesi tatu ambazo zimezuia utekelezaji wa shughuli za maendeleo na umekuwa ukihusishwa na vita vya ubunge baina ya Kagasheki na Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani.
“Hii ni mara yangu ya kwanza kupata nafasi ya kuzungumzia suala hili. Hakuna unafiki hapa, hili nitalisimamia mahali popote na nitalisema mahali popote kuwa Pinda, ndiye tatizo katika mgogoro huu ulioinyima Bukoba maendeleo,” alisema Kagasheki.
“Lakini hiyo hainizuii kusema kuwa Tamisemi ndiyo tatizo, ingawa waziri wake ni Hawa Ghasia. Pinda ndiye msimamizi na bungeni alisema Amani siyo meya tena, lakini hakuna lililofanyika hadi leo na wananchi wanakosa maendeleo,” aliongeza akirejea kauli ya Pinda bungeni kuwa meya huyo alijiuzulu halafu siku chache baadaye Amani akaibuka na kukanusha habari za kuachia kiti cha umeya.
Alisema kuwa awali wakati mgogoro huo unafukuta, uongozi wa juu CCM uliagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG) kwenda Bukoba, naye akaenda kufanya utafiti, akamaliza na akatoa kila kitu.
Kagasheki alieleza: “ Nilikwenda katika kikao cha CCM, Pinda yupo ndani ya chama, kikaagiza madai hayo yafanyiwe kazi, lakini mpaka leo Takukuru hawajafanya chochote. Ndiyo maana nasema, Pinda akija kuomba kura (za urais) Bukoba, pale mjini, hali ni ngumu kwelikweli, atapata shida sana.
“Huu siyo mgogoro, ni wizi wa fedha na ripoti ya CAG ipo wazi lakini wahusika walio chini ya Waziri Mkuu hawataki kuifanyia kazi…Jambo hili lisipofanyiwa kazi, lazima itakuwa ajenda katika Uchaguzi Mkuu.”
Mbunge huyo wa Bukoba Mjini alisisitiza akisema: “Unajua kuna vitu vinaumiza, maana vile siyo vitu vyangu ni taarifa ya CAG na kwa kweli huyu CAG aliyeondoka ungekuwa unamuuliza ukweli, angekwambia amegundua mambo mengi ndani ya Serikali ambavyo hayafanyiwi kazi. Wizi usio na kifani, upotevu wa fedha na jambo zuri ni kuwa ile kazi aliyokuwa akafanya CAG ipo kikatiba.”
Alisema kuwa CCM ilitoa maelekezo na kupitia Serikali ikayapeleka Tamisemi, lakini hadi sasa hakuna pendekezo hata moja la CCM wala CAG lililofanyiwa kazi, lakini Waziri Mkuu yupo kimya.
“Tunapozungumzia Tamisemi, tunazungumzia Waziri Mkuu, bahati nzuri yeye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM. Uamuzi wa Kamati Kuu, Pinda hakufanya hata moja na hapo ndipo mgogoro ukapamba moto,” alidai
- Mwananchi

No comments:

Post a Comment