Pages

Monday, February 23, 2015

UANDIKISHAJI: Njombe hawana taarifa za BVR


Njombe. Siku moja kabla ya kuanza uandikishaji wa wananchi katika Daftari la Wapigakura, wakazi wengi wa Mkoa wa Njombe hawajui uwepo mchakato huo, huku wengine wakionyesha wasiwasi na muda utakaotumika.
Pia, wameonyesha wasiwasi wao kuwa kazi hiyo huenda isifanikiwe kwa asilimia 100 kutokana na Serikali pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) 



kushindwa kuwapasha taarifa wananchi wenye sifa za kujiandikisha kwa kiwango kinachotakiwa, kutokana na wengi kutofahamu kuhusu tarehe ya kuanza uandikishaji.
NEC ilipanga kuanza kazi hiyo ya Februari 16, lakini ikasogeza mbele kwa maelezo kuwa inatoa muda kwa vyama vya siasa kuandaa mawakala wake.
“Mimi ndio unaniambia kwamba tunatakiwa kujiandikisha katika Daftari la Wapigakura kuanzia tarehe 23. Binafsi nilikuwa sijui kabisa, sasa kama kuna kujiandisha hiyo siku kwa nini Serikali haijatutangazia mapema ili tujue?” alihoji Robert Msigwa, mkazi wa mtaa wa Kambarage baada ya kuulizwa kama anafahamu lolote kuhusu uandikishaji wapigakura.
“Mimi taarifa ninayo nilisoma kwenye magazeti ila hofu yangu ni muda wa siku saba ni mfupi. Hauwezi kutoa fursa kwa wananchi wote wa Mkoa wa Njombe kujiandikisha hasa ikizingatiwa kwamba kwa sasa ni kipindi cha kilimo wengi wanashinda mashambani na hawana taarifa ya jambo hili,”  alisema Veronica Sanga mkazi wa Mtaa wa Idundilanga.
Hata hivyo, mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva alisema jana kuwa muda huo wa siku saba ni kwa ajili ya uandikishaji kwenye mji mdogo wa Makambako.
Naye Alphonce Mlyuka, mkazi wa Mtaa wa Ramadhani, alisema kazi hiyo haiwezi kufanikiwa kwa asilimia 100 kwa kuwa serikali haikujipanga vyema kuiwezesha kifedha NEC ili kuisimamia kikamilifu, ndiyo maana imesogeza mbele kutoka Februari 16 hadi 23 kutokana na kukosekana kwa vifaa.
Akizungumzia maandalizi ya mkoa wakati alipokutana na vyama vya siasa mjini hapa, Jaji Lubuva alisema: “Kila kitu kimekamilika, mashine zote zimeshafika Njombe na tunachosubiri ni kuanza tu uandikishaji katika vituo 44 na kila halmashauri zitatumika siku 28 na kwa kituo kimoja kitatumia siku saba.”
Akizungumzia mashine 7,750 za BVR ambazo hazijafika, Jaji Lubuva alisema: “Serikali imeshalipia mashine hizo na tunatarajia zitafika wiki ya kwanza au ya pili ya mwezi ujao na zitakapofika tutawatangazia ratiba kamili ya mikoa mingine.”
Makamu mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula, akizungumza na gazeti hili hivi karibuni baada ya kumaliza ziara yake ya siku tatu ya kuangalia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho mkoani hapa, alisema kusogezwa mbele kwa uandikishaji kunatokana na uwezo mdogo wa NEC kulimudu jambo hilo.
Alisema wao kama vyama vya siasa vyenye uwakilishi bungeni (TCD) walishakutana na NEC na kuishauri mambo ya msingi, na kwamba hawapendi kuona tume ndio ikiwa chanzo cha migogoro.
“Tatizo lililosababisha kuchelewa kuanza kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura ni vifaa. Sisi kama TCD na kwa bahati nzuri mimi ni mwenyekiti wake tulishakutana na NEC na kuishauri mambo ya msingi na sisi hatupendi tume ndiyo iwe chanzo cha migogoro lakini nadhani kilichosababisha hili ni uwezo mdogo tu wa tume katika kulimudu hili,” alisema Mangula.

No comments:

Post a Comment