Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali akichangia mjadala
katika kikao cha Bunge, mjini Dodoma. Picha na Anthony Siame
|
Dodoma. Mvutano mkali uliibuka jana bungeni wakati Bunge
lilipokaa kama kamati kupitisha Muswada wa Takwimu wa mwaka 2013, baada ya
wabunge kuupinga. Muswada huo una kipengele kinachotoa adhabu ya kifungo cha
miaka mitatu jela na faini isiyopungua Sh10 milioni kwa mtu au chombo cha
habari kitakachofanya makosa ya kutoa takwimu zisizokuwa sahihi.
Wabunge hao waliufananisha muswada huo na miswada miwili ya
habari ya mwaka 2015 ambayo itawasilishwa bungeni Jumanne chini ya hati ya
dharura kwa usiri uliopo na mpango wa kuiwasilisha bila wadau kushirikishwa.
Awali, muswada wa Takwimu uliwasilishwa kwenye mkutano wa 17
wa Bunge uliofanyika Novemba mwaka jana na wabunge wakapinga vifungu
vinavyobana waandishi wa habari kuhusu eneo la takwimu, ndipo Serikali
ilipoamua kuutoa kwa maelezo kuwa inakwenda kuurekebisha hadi ilipourejesha
jana na ukapitishwa kwa mbinde.
Jana, Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha muswada huo,
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika alihoji juu ya kifungu hicho kinachotoa
adhabu kali na Serikali kujibu kuwa imeshakifanyia marekebisho.
Hata hivyo, Mnyika hakukubaliana na maelezo hayo, bali alisema
kifungu hicho hakijafanyiwa marekebisho yoyote na Serikali na adhabu bado
inaendelea kuwa kali.
Mnyika aliungwa mkono na mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester
Bulaya aliyehoji, “Iweje Serikali iweke kinga kwa mtumishi wa Serikali anayetoa
taarifa zisizo sahihi lakini ikaacha kuweka kwa mwandishi anayepewa taarifa
hizo zisizo sahihi na ofisa huyo wa Serikali?”
Maelezo ya Bulaya yalimfanya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
(AG), George Masaju kusimama na kusema kwa kifupi kuwa “mwandishi atakwenda
kujieleza mahakamani au polisi.”
Ilivyokuwa mwaka jana
Kabla ya kuondolewa bungeni Novemba 2014 muswada huo pamoja
na mambo mengine, ulikuwa ukipendekeza faini ya Sh10 milioni au kifungo cha
mwaka mmoja jela au vyote kwa chombo cha habari kitakachotoa taarifa za
kitakwimu za uongo au zenye upotoshaji.
“Mtu yeyote, kwa
kujifanya anatimiza majukumu yake, iwapo anapata au anaomba kupatiwa taarifa
ambayo haijaidhinishwa kuipata na kuichapisha au kuisambaza atakuwa amefanya
kosa ambalo adhabu yake ni kifungo kisichopungua miezi 12 au faini isiyopungua
shilingi milioni mbili au vyote kwa pamoja,” ilisema ibara ya 37 (d) cha
muswada huo.
Muswada huo pia ulikuwa ukiainisha kwamba takwimu rasmi ni
zile ambazo zimetolewa na kuidhinishwa na taasisi zilizoelezwa kwenye ibara
hiyo ya 20 na ndizo pekee zinazoweza kutumika kama ushahidi kwenye kesi.
Adhabu kali pia zimependekezwa kwenye muswada huo kwa vyombo
vya habari ambavyo vitatoa taarifa za takwimu zitakazosababisha watu
wasishiriki kwenye shughuli zilizoandaliwa na Serikali zinazohusiana na masuala
ya takwimu.CHANZO MWANAINCHI
No comments:
Post a Comment