Pages

Thursday, March 26, 2015

Mambo matatu yanayoipa CCM nguvu dhidi ya UKAWA


Wakati Taifa likielekea katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu, ushindani wa wazi wa kisiasa kati ya chama tawala (CCM) na vyama vya upinzani kupitia Ukawa unaonekana bayana.
 
Kambi hizo mbili, zinatunishiana misuli huku kila moja ikijigamba kuibuka na ushindi na hatimaye kushika dola.
 
Licha ya kauli za majigambo kutoka kambi hizo, bado 


hakujawa na uhakika kambi ipi itakamata dola. Hata hivyo, masuala kadhaa yanatajwa kuwa vigezo vya ushindi kwa kila kambi.
 
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema mambo yanayotazamwa ni pamoja na uimara wa kila kambi hasa kwa kuegemea kwenye maeneo kama nguvu ya fedha katika kufadhili harakati za siasa, kukomaa kwa demokrasia, umakini na uwezo wa viongozi wake na kubwa zaidi, wingi au uhakika wa wanachama katika maeneo mbalimbali.
 
Nguvu ya fedha
Kigezo cha nguvu ya fedha ni muhimu  kwani ndilo eneo linalochangia ushindi kwa kiwango kikubwa katika siasa za  ushindani.
 
Fedha ndiyo inayowezesha viongozi kutembelea maeneo mbalimbali nchini kujinadi na kutafuta uungwaji mkono.
 
Kwa Tanzania, vyama vyote vinavyoshiriki katika uchaguzi vinakidhi kigezo hiki, japo kwa  uwezo tofauti.  Kwa mfano, vyote vinapata ruzuku kutoka serikalini.
 
Hata hivyo, CCM ndiyo inayoongoza kwa kupewa kiasi kikubwa cha fedha kama ruzuku. Wakati CCM ikipata ruzuku ya takriban Sh800 milioni kwa mwezi, Chadema inapata Sh203.6 milioni huku CUF ikipata Sh117.4 milioni na NCCR-Mageuzi Sh10 milioni.
 
Ukiachilia mbali kiasi kikubwa cha fedha za ruzuku inachopata CCM, bado chama hicho kina sifa ya nyongeza kulinganisha na upinzani, kwani ndicho chama chenye vitegauchumi vingi na wafadhili wengi wakiwamo wafanyabiashara wakubwa nchini.
 
Mtandao wa wanachama
CCM pia inao mtaji wa wanachama nchi nzima kutokana na mtandao wake kilioujenga tangu wakati wa mfumo wa chama kimoja.

Ni CCM iliyoanzisha mfumo wa uongozi katika ngazi ya shina (mabalozi wa nyumba kumi), mtindo unaokiwekea mazingira mazuri ya kujikusanyia wanachama wa uhakika katika maeneo mengi ya nchi, hususan vijijini ambako upinzani umeshindwa kupenya kwa kiasi kikubwa.
 
Mfumo huu wa uongozi wa mashina umeigwa na Chadema. Hata hivyo,  mafanikio yake hayalingani na ya chama hicho kikongwe kilichojikita mizizi kwa muda mrefu.
 
Demokrasia ndani ya vyama
Licha ya kuwapo kelele za matumizi makubwa ya fedha na vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi, mfumo wa uongozi wa chama hicho tawala unaonekana kuwa wa kidemokrasia kulinganisha na ule wa vyama vya upinzani.
 
Ni CCM ndiyo inayoonekana viongozi wake  wakiachiana madaraka kwa njia ya kidemokrasia kila baada ya miaka fulani.
 
Wakati CCM ikiweka bayana katika Katiba yake vipindi viwili vya uongozi, kwa vyama vya upinzani hakuonekani kuwapo kwa demokrasia hiyo, baadhi yao tangu vianzishwe viongozi wa kitaifa ni walewale. Vyama vyote vinavyounda Ukawa havina ukomo wa madaraka na viongozi wake wote wa taifa, wamedumu katika kwenye uongozi kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitano.
 
 Wasemavyo wachambuzi
Mhadhiri mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Kitila Mkumbo anasema pamoja na ukweli kuwa CCM inaweza kuvizidi vyama vya upinzani katika kila eneo,  bado upinzani una nafasi kubwa ya kufanya vizuri na hata kushinda katika uchaguzi ujao.
 
Anasema kwa hali ilivyo sasa, wananchi wengi wamechoshwa na matukio mengi yasiyofaa yanayofanywa na viongozi wa Serikali iliyopo madarakani na wanachotaka ni mabadiliko.
 
Anasema licha ya kuwapo kwa matatizo katika mifumo ya uongozi ndani ya upinzani, ikiwamo kuminywa kwa demokrasia,  wananchi wengi wanataka mabadiliko na wapo tayari kuing’oa CCM.
 
Kuhusu kigezo cha fedha na mtandao wa uongozi, anasema mambo hayo hayawezi kuwa kigezo cha ushindi kwa CCM,  kwa sababu kwa hali ilivyo sasa  vyama vya upinzani navyo vina fedha nyingi na vinaweza  kuzitumia kuwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi.
 
“Kwa mfano, Chadema wana pesa nyingi zinazowawezesha kuzunguka mikoani kujijenga na kujiimarisha,” anasema.


Mchambuzi wa masuala ya siasa na utawala bora nchini, Buberwa Kaiza anasema ni vigumu kutabiri chama kipi kitashinda uchaguzi katika kipindi hiki, kwa kuwa ushindi wa chama utategemea na mgombea atakayesimamishwa.
 
Anasema ni kweli, CCM inaonekana kujijenga tangu chini, lakini kilikuwakimejengwa na vyama vya ushirika ambavyo sasa vimekufa.
 
Anasema vyama vya upinzani kupitia Ukawa, vinaonekana kuungwa mkono zaidi na watu wa mijini na wasomi kwa kiasi fulani. Anasema kwa sasa ni vigumu kutabiri ushindi wa Ukawa kwa kuwa umoja huo haujaweka bayana jina la mgombea wake.
 
‘’CCM wameshuka kiasi fulani na upinzani umepanda kwa kiasi fulani, tukifikia wakati vyama vikaweka wagombea wake hadharani, labda ndipo watu watakuwa na uamuzi,’’ anasema.
 
Kuhusu suala la nguvu ya fedha, Kaiza anasema ingawa CCM inaonekana kuwa na fedha nyingi,  ukweli ni  kuwa ndani ya vyama watu ndiyo wenye fedha na siyo za vyama.
 
“Siamini kuwa CCM wana fedha watakazozitumia wakati wa uchaguzi na siamini kuwa wapinzani nao hawana fedha kabisa. Ninachojua ni kuwa hawa wenye fedha watazipeleka pale wanapoona kuna ushindi,’’ anaeleza.
 
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda anakubaliana na vigezo vinavyokipa chama tawala nafasi ya kufanya vizuri, lakini anasema endapo Ukawa itasimamia mpango wake wa kuungana na kuwa kitu kimoja katika uchaguzi mkuu ujao, umoja huo unaweza kufanya maajabu.
 
“Naamini wapinzani wanaweza kuleta upinzani wa maana na juhudi zao zinaweza zikawa kigezo kikubwa cha kuufanya upinzani ushinde,” anasema.

No comments:

Post a Comment