PICHA NA MAKTABA |
Mashuti makali yaliyopigwa na wachezaji wa timu ya Taifa
Stars kwenye mazoezi yao kwenye Uwanja wa CCM Kirumba yamewavutia mashabiki
wachache waliofika ili kufuatilia mazoezi hayo.
Baadhi yao wametamka kuwa kama wakiyatumia Jumapili kwenye
pambano na Malawi, basi wataondoka na kapu la mabao.
Stars wanafanya mazoezi jijini hapa tangu juzi na kwa muda
mwingi juzi walipiga mashuti ambayo
makipa Aishi Manula na Mwadini Ally, wote
kutoka Azam waliokaa magoli tofauti walikuwa na wakati mgumu.
Washambuliaji wa Stars, Mbwana Samatta,Thomas Ulimwengu,
John Bocco walikuwa mwiba mkali kwa makipa hao kutokana na mashuti makali
waliyopiga, kufunga huku mengine wakiyapangua.
Katika mazoezi hayo, Samatta aliwakosha mashabiki baada ya
kuruka kichwa maridadi na kumfunga kipa Mwadini Ally ambaye hakufanya chochote
zaidi ya kuuangalia mpira ukiingia wavuni.
Kocha John Tegete wa Toto African ya hapa aliyekuwa uwanjani
hapo alisema kuwa kocha wa Stars, Martin Nooij katika mazoezi hayo amekuwa
akiwaelekeza mbinu za kila mchezaji kufunga.
“Hii safi, naona muda mwingi kocha anafundisha namna ya kila
mmoja kufunga bao, si beki wala mshambuliaji, wote wanafunga, ndiyo maana
unaona muda mwingi ameutumia kufanya hili zoezi inapendeza,” alisema Tegete.
Wadau wa soka jijini hapa, Juma Kosky, Kadiri Ramadhani na
Issa Ally walisema kuwa mazoezi hayo yamewapa faraja kuwa mechi hiyo
haitatakuwa ngumu kutokana na morali ya wachezaji hao, hasa Samatta.
“Kama haya mashuti wanayopiga wakiyafanya kwenye mechi yetu
ya Jumapili na hao Malawi, basi kazi itakuwa rahisi, wamenikosha, ila wachezaji
wanatakiwa kuyafanya yale ambayo wameelekezwa mazoezini, tumeona morali yao iko
juu,” walisema mashabiki hao.
No comments:
Post a Comment