Wakati kamatakamata ya waganga wa kienyeji ikiendelea
kupamba moto katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, mmoja amenaswa akiwa na
viungo vya binadamu, kikiwemo kichwa ambacho bado kilikuwa na nywele
zake.
Mganga huyo, Nyamizi Makunga (70), mkazi wa Kijiji cha
Igurubi wilayani Igunga, Tabora, alitiwa mbaroni juzi. Mbali na viungo
hivyo, pia alikutwa na vifaa vingine, zikiwemo nyara za serikali.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Igurubi, George Henry, alisema
Makunga alikamatwa nyumbani kwake kutokana na msako mkali unaendelea kwa
lengo la kuwabaini waganga wanaofanya ramli chonganishi.
Msako huo umetokana na kukithiri kwa mauaji ya watu wenye
ulemavu wa ngozi, ambapo serikali katika kubaini chanzo, imekuwa ikisaka
waganga wanaotuhumiwa kufanya ramli hizo.
Henry alisema polisi walifanikiwa kumnasa Makunga kutokana
na taarifa kutoka kwa raia wema, ambapo walipofanya msako walikuta fuvu
la kichwa la binadamu likiwa na nywele zake.
Mbali na fuvu hilo, polisi pia walikuta kipande cha mfupa
wa binadamu, mkia wa nyumbu, gamba la kobe na ngozi za wanyama
mbalimbali.
Wananchi wa Kijiji cha Igurubi, wamepongeza msako
unaofanywa na polisi kuwatia mbaroni waganga ambao ndio chanzo cha
kushamiri kwa mauaji ya albino.
Pia walisema kwa muda mrefu Makunga amekuwa kikwazo cha
maendeleo kwenye eneo hilo kutokana na kufanya mambo kinyume na kwamba
wananchi wamekuwa wakimwogopa.
Alipohojiwa, Makunga alikiri viungo hivyo ni vya binadamu na kuwa aliachiwa na baba yake ili kuendesha shughuli za uganga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Suzana Kaganda, alithibitisha kukamatwa kwa mganga huyo akiwa na viungo vya binadamu.
No comments:
Post a Comment