Shirika la Ugavi na Usambazaji wa Umeme nchini (TANESCO),
limekiri kuwepo na matatizo ya mfumo wa kununua Lipa Umeme Kadiri Utumiavyo (LUKU),
ulioanza Ijumaa jioni wiki iliyopita hadi jana na kuwa matatizo hayo yanatokana
na mfumo wa kuuza umeme wa LUKU.
Akizungumza na mwandishi jijini Dar es Salaam jana, Meneja
Mawasiliano wa TANESCO, Adrian Shogholo
alisema ni kweli kuwa tatizo hilo lipo
na limetokana na mfumo wa manunuzi wa umeme wa LUKU.
“Ni kweli tunaomba radhi wateja wetu kwamba kuanzia Ijumaa
jioni kulianza tatizo la kununua umeme wa luku, kwa wateja wetu, ila tumegundua
tatizo na mafundi wetu kwa kushirikiana wa mafundi kutoka Afrika Kusini, ambao
walitengeneza mfumo huo, wanalishughulikia tatizo hilo”,
alisema Shogholo.
Aidha aliahidi kwamba muda wowote kuanzia leo, huduma
zitaanza kupatikana na kwamba wakati tatizo hilo likiendelea kushughulikiwa,
wateja wa Luku wanaweza kununua umeme kupitia benki ya CRDB, NMB na Max Malipo.
“Kuna wateja wanaotumia simu kununua umeme, wapo waliotuma
fedha na hawajarudishiwa majibu ya umeme, na wengine wamepata umeme ila
wakiingiza kwenye LUKU hauingii, wasihofu fedha zao ziko salama na watapata
umeme, tutawatumia namba nyingine ambazo wakiingiza zitakubali”,
alisema Shogholo.
No comments:
Post a Comment