Elnest Mangu.
TANZANIA tuna majeshi kadhaa na vyombo vya ulinzi na usalama vinavyotambulika kisheria. Tunalo Jeshi la Wananchi, Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza. Chini yake, JWTZ unawakuta JKT, kwa polisi, tunao Zimamoto, FFU, Usalama barabarani (Trafiki) na Mgambo.
Majeshi na vikosi hivi vina majukumu yanayofahamika na kukubalika. Kwa hiyo haishangazi tunapoona polisi wakitumika kuwakamata majambazi, ambao wakati mwingine huwa ni askari kutoka JWTZ. Ni jukumu lao na ndiyo maana huwezi
kuona jeshi la wananchi wakilalamika vijana wao kukamatwa wanapokutwa na hatia ya uhalifu.
Polisi tunajua ndicho chombo halali kinachofanya kazi zake kuhakikisha kunakuwepo ulinzi wa raia na mali zao. Katika miaka ya hivi karibuni, kisiasa, kumekuwa na sintofahamu baina ya viongozi na watendaji wa vyama vya upinzani. Wao, kwa kile wanachoamini kuwa Jeshi la Polisi linatumika kukilinda chama tawala, wameamua kuunda vikosi vyao, ambavyo wenyewe wanasema ni vya ulinzi.
Kwa CCM katika kujibu mapigo, wameamua kuwatumia vijana wa Chipukizi, kama ndiyo kikundi cha ulinzi wao, baada ya kuona CUF wakiwa na Green Guard na Chadema wakiwa na Red Brigade. Hivi ni vikosi vya ulinzi ambavyo vyama vya upinzani vinadai vitatumika kuhakikisha vinalinda kura wakati wa uchaguzi mkuu ujao.
Yapo madai ya kuibiwa kura za vyama vya upinzani kunakofanywa na chama tawala kwa kushirikiana na watendaji wa serikali. Kwa kiwango gani madai haya yana ukweli, ni jambo lenye kuhitaji muda na kujiridhisha, lakini kauli hizi zinazofanywa sambamba na picha zinazowaonyesha vijana wa vikosi hivi vya ulinzi wakiwa mazoezini, vinatia shaka.
Vikosi hivi vitalindaje kura za vyama vya upinzani zisiibiwe? Maana tunavyofahamu, kura zote huhesabiwa mbele ya mawakala wa kila chama kilichoshiriki, pasipo hata uwepo wa Jeshi la Polisi. Ni vipi vikosi hivi vitajua kuhusu wizi huu?
Rai yangu kwa serikali ni kuwa makini na nyenendo za vyama vya siasa, kwa sababu kadiri tunavyojaribu kuchekacheka, ndivyo tunavyoweza kukaribisha maangamizi yanayoweza kuzuiliwa. Mamlaka zinazohusika zikataze shughuli zozote za Chipukizi, Red Brigade na Green Guard kwenye harakati za kisiasa!
No comments:
Post a Comment