Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT),
kimesema kinatarajia kunyakuwa majimbo manne ya ubunge katika Uchaguzi Mkuu
utakaofanyika Oktoba, mwaka huu.
Kimetaja majimbo hayo kuwa ni Ubungo, ambalo linaongozwa na
John Mnyika (Chadema), Kawe linaloshikiliwa na Halima Mdee (Chadema), Segerea
ambalo Mbunge wake ni Makongoro Mahanga (CCM) na Kahama la James Lembeli (CCM).
Kiongozi Mkuu wa Chama hicho, Zitto Kabwe, alisema hayo
katika kipindi cha Hot Mix kinachorushwa na kituo cha EATV.
Zitto aliendeleza msimamo wake wa kutogombea ubunge kwenye
jimbo lake la awali la Kigoma Kaskazini.
"Nina maombi jimbo la Kahama, Kawe, Ubungo na Segerea
lakini kwa kuwa ACT kinaongozwa kizalendo, tutaweka utaratibu mzuri wa kuweka
wagombea kila eneo, binafsi kwa sasa siwezi kusema wapi nitagombea,"
alisema.(P.T)
Alipoulizwa ni eneo gani kati ya hayo aliyoyataja huduma
yake inahitajika, alijibu kwa kifupi kuwa, nchi nzima ina muhitaji.
"Kabla ya kampeni kuanza wagombea wakirudisha fomu
ndipo mtajua Zitto anagombea jimbo gani, lakini lazima niongozwe na chama
nikagombee wapi , wanaweza kusema Zitto kagombee jimbo A," alisema.
Aliongeza kuwa, ACT kinahitaji kujipanga kuingia kwenye
mapambano ya kufyeka msitu wa siasa kwa kuwa ndani yake kuna vyama zaidi 22 na
vingine vikiwa na uzoefu mkubwa kutokana na kudumu zaidi ya miaka 23.
Alisema kazi kubwa walionayo ni kukijenga chama ili kiweze
kulirudisha taifa kwenye misingi ya waasisi waliyoiacha.
Aliongeza kuwa, baadhi ya watu wanamuona kama anaanza upya
kwa sababu wapo wachache waliwahi kujaribu na kuishia njiani.
Alipoulizwa kuhusu wachambuzi wa siasa wanavyomchukulia hivi
sasa, Zitto alisema wapo wenye mtazamo hasi na wengine chanya.
Alisema kwa wale wanaomchukulia kwa mtazamo hasi anaendelea
kuwafundisha na kuwaonyesha kwamba muono wao ni tofauti wakati wale wa chanya
anaendelea kuwasikiliza ili kupata muongozo zaidi kutoka kwao.
"Tukumbuke hii nchi watu wamezoea kuchukia mabadiliko
angalia kwenye sanaa wakimuona Diamond amefanikiwa waanza kutoa maneno ambayo
siyo, watu wanachukia mabadiliko," alisema.
Kuhusu kuitwa msaliti ndani ya Chadema kwa madai kuwa baada
ya kuikosesha Chadema jimbo kule Katavi, alisema jambo hilo siyo la kweli na kwamba
amekitumikia chama hicho nusu ya maisha yake na alichokifanya kinafahamika kwa
wanachama na viongozi.
"Ambacho sikufanya mimi ni binadamu sipo sawa kwa kila
kitu hakuna binadamu ambaye hana makosa lakini yapo mema ambayo nimefanya
lakini sasa nimeyakunja na kuyaweka pembeni na tumechora mstari na kuanzisha
chama cha siasa cha wazalendo," alisema.
Kuhusu kurasa zake kwenye mitandao ya kijaamii kuwa na maoni
hasi, Zitto alisema kila mtu ana mawazo yake na hawezi kuyabadisha.
"Wito wangu ni kwa watu ambao ni waoga wa kuchukua
maamuzi, waweke akiba ya maneno kwa sababu ACT ni sawa na moto wa pumba ambao
ukiwaka juu unadhani hakuna moto lakini ukiweka mguu kuna moto mkali
sana," alisema.
Chanzo:http://allytz.blogspot.com/
No comments:
Post a Comment