Mbunge wa Jimbo la Morogoro, Abdulaziz Abood.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya
ya Morogoro, kimetangaza kufanya maandamano makubwa kwenda kwa uongozi
wa Manispaa ya Morogoro, kushinikiza kutekelezwa kauli ya Mbunge wa
Jimbo la Morogoro, Abdulaziz Abood (pichani) (CCM) ya kutaka kutolewa
taarifa ya matumizi ya Sh. milioni 720 za mradi mkubwa wa ujenzi wa
stendi ya mabasi yaendayo mikoani eneo la Msamvu.
Pamoja na fedha hizo, pia Chadema inataka maelezo mengine kutoka
kwa Uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro akiwamo Meya na
Mkurugenzi kuhusu fedha za miradi ya ujenzi wa soko kuu la Morogoro .
Hatua ya Chadema kuamua kufanya maandamano hayo imekuja siku chache
baada ya Abood kufanya ziara ya kukagua mradi huo na kunyimwa taarifa
za matumizi ya fedha ungozi wa manispaa, hivyo kulazimika kuahirisha
ziara hiyo, huku akitoa siku 14 taarifa hiyo itolewe vinginevyo suala
hilo atalifikisha kwa Rais Jakaya Kikwete.
Hata hivyo, uongozi wa Manispaa ya Morogoro kupitia Meya wake, Amir
Nondo ukizungumzia suala hilo kwa waandishi wa habari, ulieleza kuwa
ujenzi wa mradi unafanywa kwa ubia na Mfuko wa Pensheni wa Serikali za
Mitaa (LAPF) ambao ndiyo wanawajibika na fedha hizo Sh. milioni 720
walizitoa kwa ajili ya fidia ya kumlipa mtu aliyekuwa ndani ya eneo
hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa jana, Mwenyekiti wa
Chadema Wilaya ya Morogoro, alisema wanakusudia kufanya maandamano hayo
Aprili 14 mwaka huu kwenda ofisi hiyo ya mkurugenzi wa manispaa na meya
kutaka matumizi ya fedha za mradi huo wa stendi yawekwe wazi.
Alisema katika mradi huo wa ujenzi wa stendi ya kisasa kuna harufu
ya ufisadi unaofanywa na baadhi ya viongozi wa manispaa ndiyo maana
wanakataa kutoa taarifa zake kwa mbunge.
“Yule ni mbunge anapaswa kujua maendeleo ya ujenzi sasa tunashangaa
kwanini wanamnyima taarifa za mradi ambao ni sehemu ya fedha za
serikali, kama hakuna ufisadi wanaficha nini?. Sasa sisi tutafanya
mandamano ya kumuunga mkono Abood ili wananchi wapewe taarifa za mradi
huo na maendeleo yake,” alisema.
Mwenyekiti wa Chadema alilitaadhalisha Jeshi la Polisi Mkoa wa
Morogoro kuwa lisithubutu kuyazuia maandamano hayo ya amani, kwani
hawatakubali kuzuiliwa kwa kuwa hizo ni fedha za wananchi ambao wengi
wao wanashindwa kupata huduma nyingine kama za afya kutokana na mradi
huo.
Mradi wa stendi ya kisasa ya mabasi yaendayo mikoani ya Msamvu unatalajiwa kutumia Sh. bilioni 10 katika awamu ya kwanza.
No comments:
Post a Comment