Licha ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kumtaka Mkuu wa
Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima, kuhamisha makazi ya kanisa
lake lililopo katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam,
bado hajatekeleza.
Wiki iliyopita, Meneja Uhusiano wa NHC, Yahya Charahani,
alilieleza NIPASHE kuwa walimpatia notisi Askofu Gwajima ya kuhama eneo hilo
mwezi mmoja uliopita, muda ambao ulimalizika jana.
Jana NIPASHE lilitembelea
katika viwanja lililopo kanisa hilo saa 5:00 asubuhi na kukuta shughuli
za kiibada zikiendelea kama kawaida.
Katika viwanja hivyo, kulikuwapo na mahema madogo madogo
yaliyokuwa na waumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu
Gwajima wakifundishana Neno la Mungu.
Kadhalika, mbele ya uwanja huo, kulikuwapo na jukwaa kubwa
lililopambwa kwa vitambaa na hakukuwa na dalili zozote za kuhamisha vifaa
vikiwamo vya muziki na spika kubwa.
Hata mwandishi alipoingia katika viwanja hivyo, alipokelewa
na baadhi ya watumishi wa kanisa hilo na kuulizwa kama amekuja katika maombi au
anahitaji huduma ya kiroho.
“Majeshi Majeshi, karibu tukuhudumie mpendwa, umekuja kwenye
maombi au unahitaji huduma yoyote kutoka katika kanisa letu?,” mmoja wa
wahudumu ambaye hakufahamika jina lake alimhoji.
Hata hivyo, Askofu Gwajima mwenyewe hakuwapo na hata
alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi, iliita bila majibu na alipotumiwa ujumbe mfupi wa mkononi, pia
hakujibu.
Kwa mujibu wa Charahani,
NHC walimpatia notisi Askofu Gwajima ya mwezi mmoja kuondoka katika
viwanja hivyo na kwamba notisi hiyo ilimalizika tangu Machi 9, mwaka huu.
Alisema baada ya kumalizika kwa notisi hiyo, NHC lilimpatia
muda zaidi Askofu huyo ambao ulimalizika jana.
Hata hivyo, jana alipotafuwa Mkuu wa Kitengo cha Huduma na
Mawasiliano wa NHC, Suzan Omary, kuelezea hatua gani zitafuata endapo Askofu
Gwajima hatahamisha huduma za kanisa lake baada ya notisi kuisha, alieleza kuwa
atafutwe leo kwa kuwa hakuwa ofisini wakati huo.
“Sipo ofisini leo (jana), nitafute kesho (leo), nitakupa
ufafanuzi zaidi, na hata nikikuelekeza kwa mtu mwingine hatakusaidia kwa kuwa
leo hakuna mtu ofisini,” alieleza Omary
No comments:
Post a Comment