Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema hakitakubaliana na maamuzi yoyote
ya serikali kuahirisha Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu, kwa kisingizio cha
kuchelewa kukamilika kwa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Mwenyekiti wa
Chadema Taifa, Freeman Mbowe, alitoa angalizo hilo jana, wakati wa ufunguzi wa
programu ya mafunzo itakayofanyika nchi nzima, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya
Uchaguzi Mkuu mwaka huu.
Alisema
serikali isithubutu kutumia urahisi iliyoupata kuahirisha kura ya maoni ya
katiba inayopendekezwa na kutaka kufanya hivyo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba
mwaka huu ambao unafahamika kikatiba.
“Tarehe ya
Uchaguzi Mkuu ilijulikana tangu mwaka 2010 kuwa ni Jumapili ya mwisho ya
Oktoba…uandikishaji hadi leo haujamalizika kwenye mkoa mmoja, kuna miezi minne
kufika siku ya kuanza kampeni, tunajiuliza ndani ya siku hizo
itaweza
kuandikisha nchi nzima?” alihoji.
Alisema
Chadema imejipanga kuwa kampeni za uchaguzi huo zitakazoanza Agosti 15, mwaka
huu ambazo zitatudumu kwa siku 72.
Uandikishaji
wapiga kura katika Daftari la Kudumu la wapigakura kwa mfumo wa Biometric
Voters Registration (BVR), ulianza mkoani Njombe na Februari 23, mwaka huu na
utakamilika kesho.
Tume ya Taifa
ya Uchaguzi (Nec), imepokea vifaa (BVR Kits) 498 huku ikiendelea kusubiri vifaa
vingine.
Nec ilitangaza
kuahirisha kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa iliyotakiwa kufanyika Aprili
30, mwaka huu, kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kuchelewa uboreshaji wa daftari
hilo na kwamba itatangazwa tena baada ya kushauriana na Tume ya Uchaguzi
Zanzibar (Zec).
Aidha, Tume
hiyo imesema hadi Julai 30, mwaka huu, itakuwa imekamilisha uandikishaji
wapigakura kwa mfumo wa BVR na kwa sasa wataanza kwenye mikoa ya Ruvuma,
Mtwara, Lindi na Iringa.
USHIRIKIANO
IMARA
Mbowe alisema
matarajio ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
kugombana na ushirika wao kuparaganyika, na kwamba jambo hilo halitawezekana
kwa kuwa wamejipanga kikamilifu.
Alisema
anatambua majaribu na changamoto za ushirika wowote duniani, hivyo pamoja na
changamoto zinazojitokeza kwenye Ukawa, lakini watazishinda na kusonga mbele
kwa kushika dola Oktoba, mwaka huu.
“Vikao vya
Ukawa vinaendelea vizuri na makubaliano yetu ni yale yale kuwa kila kata, jimbo
na rais kutakuwa na mgombea ambaye atapitishwa na Ukawa,” alisema na kuongeza:
“Leo kuna
watangaza nia kuliko nafasi za uongozi, sisi Ukawa tunasema watakaopata
watapata kwa misingi ya haki na usawa na siyo dhuluma, watakaoshindwa ubunge na
udiwani wasiache kuunga mkono wagombea kwa kuwa serikali itakayoundwa itahitaji
viongozi wengi ndani ya serikali ya shirikisho,” alisema.
Alisema Dar es
Salaam ina dhamana kubwa kwa kuwa katika kushika dola ni lazima kujihakikishia
ushindi wa majimbo nane ya mkoa huo.
Alisema
walichogundua Ukawa ni kuwa katika uchaguzi wa mwaka 2010, Chadema na CUF
waligawana kura katika majimbo ya Temeke na Kinondoni na kwamba hawatakubali
kuendelea kugawana katika maeneo mbalimbali nchini bali kuwa wamoja.
“Hatufanyi
mtihani wa mzaha bali ni wenye kusudio la uhakika tunashika dola…tunatambua
kuwa kila chama kina nguvu kwa upande wake ndiyo maana tumejenga ushirikiano
kwa matokeo mema ya nchi,” alisema.
Ukawa ni
Muungano wa Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, ambavyo vilianzisha umoja huo
wakati wa Bunge Maalum la Katiba.
MAANDALIZI YA
VIONGOZI
Mbowe alisema viongozi
hawazuki bali huandaliwa ndiyo maana Chadema imeanza mpango wa mafunzo kwa
viongozi wake nchi nzima na wameanzia na Dar es Salaam, kwa kuwa ina idadi
kubwa ya wapiga kura kuliko mikoa yote nchini.
Mbowe ambaye
pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema maandalizi ya
viongozi 2 2,4287 yatafanyika katika kanda 10, majimbo 242, kata 4,852, matawi
22,749, misingi 64,803 ya kichama.
Alisema
viongozi hao watafundishwa namna ya kutekeleza wajibu wao na kuimarisha wagombea
ili wawe wagombea wazuri na kunadi sera zao.
Alisema Dar es
Salaam ina majimbo sita kati yake la Kigamboni ndilo lenye wapiga kura wengi
ikifuatiwa na mengine ya jiji hilo na kwamba ni kitovu cha mambo yote ikiwamo
makao makuu ya nchi na vyombo vyote vya habari.
Alisema
dhamana kubwa ya kushinda inategemea Dar es Salaam kwa kuwa kura zake ndizo
zitakazoamua nani ataongoza nchi.
Kwa mujibu ya
Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2012 na zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu
(NBS), Dar es Salaam ina wapiga kura 2,932,930.
JOHN MNYIKA
Awali, Kaimu
Katibu Mkuu, John Mnyika, alisema wakati anaingia jimbo la Kinondoni, Manispaa
ya Kinondoni mwaka 2010, makusanyo ya ndani yalikuwa Sh. bilioni saba, lakini
kwa sasa ni Sh. bilioni 35 huku ya Serikali Kuu yalikuwa ni Sh. bilioni 87 na
ya sasa Sh. bilioni 84.
Mnyika ambaye
pia ni Naibu Katibu Mkuu Bara, alisema zaidi ya asilimia 80 ya mapato ya nchi
yanakusanywa Dar es Salaam, hivyo Jiji hilo lina umuhimu mkubwa katika ushindi
wa nafasi zote.
SALUM MWALIMU
Naye, Naibu
Katibu Mkuu Zanzibar, Salmu Mwalimu, alisema kutakuwa na timu tatu za kuzunguka
nchi nzima kufanya mafunzo hayo zitakazoongozwa na makatibu hao na wataanza
kesho.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment