Kisiwa cha Mnemba |
JUHUDI za haraka zinahitajika kuchukuliwa ili kukihami
kisiwa kidogo cha Mnemba kilichopo Matemwe mkoa wa Kaskazini Unguja, kutokana
na kasi ya maji kuvamia maeneo ya nchi kavu, kutokana na mabadiliko ya tabia ya
nchi.
Mjumbe wa Kamati ya Kulinda Mazingira mkoa wa Kaskazini
Unguja, Makame Mussa Makame alisema hayo wakati alipozungumza na gazeti hili
kuhusu athari za mazingira zinazoikabili kisiwa hicho na mikakati ya kukihami
na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.
Alisema maji ya baharini, yamekuwa yakipanda juu na kuingia
maeneo ya fukwe, karibu na majengo ya hoteli ya kitalii iliyopo katika kisiwa
hicho na hivyo kutishia maendeleo ya sekta ya utalii.
“Juhudi za haraka zinahitajika kwa Serikali kuweza kukihami
kisiwa cha Mnemba ambacho kipo katika hatari ya kutoweka kutokana na athari za
mabadiliko ya tabia ya nchi ya maji ya bahari kuja juu kwa kasi na kuharibu
mazingira,” alisema.
Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira Zanzibar, Sheha Mjaja
alikiri kuwepo kwa hatari za kisiwa cha Mnemba, kuvamiwa na kasi ya maji
yanayotokana na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Mjaja alisema athari kama hizo, zipo kwa baadhi ya visiwa
vilivyopo Unguja na Pemba ambavyo vinakabiliwa na kasi ya maji kuvamia maeneo
ya makaazi ya watu.
Visiwa vidogo ambavyo vinatajwa vipo katika hatari ya
kuathirika na mabadiliko hayo ya tabia ya nchi ni Mtambwe Mkuu, Kisiwa Panza na
Kokota, ambapo baadhi ya wananchi wameanza kuhama na kuja nchi kavu.
Mjaja alitaja baadhi ya juhudi zinazochukuliwa kukabiliana
na tatizo hilo kuwa ni kupanda miti ya aina mbalimbali, ikiwemo mikoko
pembezoni mwa fukwe za bahari ili kudhibiti hatari hiyo.
“Athari za mabadiliko ya tabia ya nchi, zimeleta majanga
makubwa, ikiwemo kasi ya maji ya bahari kuvamia maeneo ya nchi kavu na kutishia
maisha ya wananchi wanaoishi maeneo hayo,” alisema.
Alisema tayari zaidi ya mikoko 60,000 imeoteshwa na
kusambazwa kwa wananchi mbalimbali kupitia vikundi vya ushirika kwa ajili ya
kukabiliana na hatari ya majanga hayo.
Mikoko ni miti maarufu inayoota pembezoni mwa baharini,
ambayo husaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia nguvu ya kasi ya maji kuvamia maeneo
ya ardhi na kusababisha uharibifu mkubwa.
No comments:
Post a Comment