Pages

Tuesday, April 14, 2015

Mahabusu dawa za kulevya wagomea chakula Segerea


Jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
Mahabusu zaidi ya 15 wa gereza la Segerea, jijini Dar es Salaam wanaokabiliwa na kesi za kusafirisha na kuingiza dawa za kulevya nchini, wanadaiwa kugoma kula wakilalamikia kusota gerezani kwa muda mrefu huku kesi zao zikiendeshwa muda mrefu bila kumalizika.  
Mahabusu hao ambao waligoma kwa siku tano hadi jana wanalalamika kwamba, wamecheleweshewa haki zao zaidi ya miaka minne tangu wafunguliwe mashitaka na Jamhuri.

Kwa mujibu wa barua ya mahabusu hao ambayo NIPASHE imeiona, wanailalamikia Jamhuri kwa kuwasotesha zaida ya miaka minne wakati kesi zao zilikuwa kwenye hatua ya kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri na utetezi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) aliwafutia mashitaka na kuwafungulia upya mashitaka yale yale katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Mbali na mgomo wa kula, barua hiyo imeeleza kwamba, baadhi yao wamejishona midomo kwa sindano na kwamba bwana jela wa gereza hilo anawatembezea mkong’oto ili wasiendelee na mgomo huo.
Pamoja na mambo mengine, watuhumiwa hao wanalalamika kwamba hawaruhusiwi kupelekewa chai, sukari, majani ya chai, vitumbua, maandazi na vitu vingine kwa mahitaji yao.
“Tumeamua kugoma kula chakula, tumechoka kusota mahabusu zaidi ya miaka minne sasa kesi zetu zilifikia hatua ya kufunga 
ushahidi wa Jamhuri na nyingine utetezi ... ajabu DPP amezifuta na kuturudisha nyuma mahakama ya chini, tunateseka sana kukaa 
ndani... ndugu zetu wamepigwa marufuku kutuletea mahitaji mbalimbali muhimu bila sababu za msingi,” ilieleza sehemu ya barua hiyo.
Aidha, barua hiyo iliendelea kudai kwamba, Bwana Jela wa Segerea amewazuia watuhumiwa wote wanaokabiliwa na tuhuma za dawa za kulevya wasikutane wala wasifanye mawasiliano yoyote na kwamba ikitokea wakakutwa wanaongea, wanashushiwa kipigo.
MSEMAJI WA MAGEREZA
NIPASHE ilimtafuta Msemaji wa Jeshi la Magereza nchini, Deodatus Kazinja, kuzungumzia madai hayo, lakini alisema kwa sasa yuko kwenye mafunzo, hivyo hawezi kuzungumza chochote.
“Niko kwenye mafunzo, siwezi kuzungumzia suala hilo wasiliana na Mkuu wa Magereza wa mkoa,” alisema Kazinja kwa njia ya simu. 
MKUU WA MAGEREZA DAR
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dar es Salaam, ASP Joel Bukuku, alithibitisha kutokea kwa mgomo huo, ingawa hakutaka  kulielezwa kwa undani.
Aliliambia NIPASHE jana kuwa kulikuwapo na jaribio la mgomo wa kula, lakini kwa sasa hali imerejea kama kawaida baada ya kuzungumza nao Alhamisi iliyopita alipokwenda katika gereza la Segerea kuwasikiliza.
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kwa njia ya simu kati ya NIPASHE na ASP Bukuku:
NIPASHE: Afande habari za Jumapili, unazungumza na NIPASHE, kuna taarifa mahabusu wa kesi za dawa za kulevya kule Segerea wamegoma kula siku ya tano leo (jana).
ASP Bukuku: Nzuri, habari za kazi, mmmh sina taarifa hizo kama kuna mgomo, lakini ngoja nicheki nitakujibu.
Baada ya nusu saa mahojiano yaliendelea hivi:
NIPASHE: Afande habari za muda vipi kuhusu taarifa za mrejesho za mgomo wa mahabusu?
ASP Bukuku: Kiukweli hakuna mgomo, kwa sasa hali iko shwari kwa sababu nilikwenda kuongea nao siku ya Alhamisi niliposikia wana jaribio la mgomo.
NIPASHE: Nini hasa malalamiko yao mpaka wafanye jaribio la kugoma kula?.
ASP Bukuku: Watuhumiwa hao wanalalamika kuhusu kesi zao kupangiwa tarehe za kuanza kusikilizwa na wana muda mrefu wako mahabusu, nimewasihi watulie kwa sababu wiki za sikukuu ofisi za serikali zilisimama kufanya kazi, kwa hiyo tutalishughulikia suala lao wasitishe jaribio hilo kwa hiyo kifupi hakuna mgomo ila walifanya jaribio kama nilivyokueleza.
Februari mwaka huu DPP aliwafutia watuhumiwa zaidi ya saba wa kesi za dawa za kulevya na kuzirejesha Mahakama ya Kisutu na baada ya kumalizika usikilizwaji wa maelezo ya mashahidi, kesi hizo zinasubiri tarehe ya kusikilizwa Mahakama Kuu

No comments:

Post a Comment