Dar es Salaam. Wakati mashambulizi ya kigaidi yakiendelea
kutikisa maeneo mbalimbali duniani ikiwamo nchi jirani ya Kenya huku kukiwa na
angalizo kuwa huenda na Tanzania ikashambuliwa, jarida moja la kimataifa
limetaja mambo 10 ya kufanya baada ya shambulio.
Mambo hayo ambayo ni hatua za kumsaidia mtu aliyenusurika
katika shambulio husika ili kunusuru maisha yake, yametajwa wakati zikiwapo
taarifa za tisho la shambulizi katika miji ya Dar es Salaam na Mwanza.
Jarida hilo lilifanya mahojiano na wataalamu wa sayansi
ambao walitoa mapendekezo ambayo mtu anaweza kufuata wakati au baada ya mlipuko na kuwa asilimia
50 ya watu wanaokutwa katika mashambulizi ya kigaidi hujeruhiwa na wengine kupoteza maisha kwa
sababu hawafahamu jinsi ya kujihami.
Tanzania iliwahi kukumbwa na shambulio la ugaidi mwaka 1998
wakati Ubalozi za Marekani, jijini Dar es Salaam ulipolipuliwa na kusababisha
vifo vya watu kumi na moja. Shambulio hilo lilitokea sambamba na lile la
ubalozi wa nchi hiyo, Nairobi, Kenya lililosababisha vifo ya watu 213.
Uvumi zaidi umeendelea kuenea baada ya shambulio la kigaidi
lililotokea wiki iliyopita katika Chuo Kikuu cha Garissa, Kenya na kuua wanafunzi 148.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias
Chikawe alisema pamoja na kusikia taarifa hizo, mpaka sasa Serikali haijaweza
kuthibitisha ripoti hizo zinazoenea, lakini inachukua tahadhari juu ya suala
hilo.
Polisi, Serikali wajiandaa
Akizungumzia tahadhari mbalimbali za mashambulizi ya kigaidi
au Watanzania kushiriki katika ugaidi, Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa
ya Jinai (DCI), Diwani Athuman alisema hali hiyo ina taswira kuwa Taifa si
salama kwa asilimia 100.
“Kuna usemi usemao mwenzako akinyolewa wewe tia maji,
Tanzania si kisiwa, kuna changamoto kubwa kwa sababu tumepakana na wenzetu
Kenya ambao wameathiriwa na ugaidi, ndiyo maana hatuwezi kusema tupo salama kwa
asilimia 100,” alisema.
Alisema kutokana na hali ilivyo sasa, Watanzania hawana budi
kutilia mkazo umoja kama njia ya kutokomeza uhalifu na kuacha kushabikia
masuala ya ugaidi.
Kuhusu vijana kujiunga na makundi ya ugaidi, Diwani alisema
wazazi hawana budi kuwafuatilia watoto huko shuleni ili wajue kinachoendelea.
“Tanzania ni lazima irudi kule ambako ilikuwa. Kila mmoja ni
mlinzi wa mwingine, sasa hivi watoto wanaachwa hadi wanapumbazika na kujiunga
na makundi ya ugaidi. Hii si kazi ya vyombo vya dola peke yake ni ya kila
mmoja,” alisema.
No comments:
Post a Comment