Dar es Salaam. Hoja za kisheria alizowasilisha Askofu wa
Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kuhusu kutakiwa kuwasilisha nyaraka
10 za utajiri na usajili wa kanisa lake polisi zimezaa matunda.
Sasa, agizo la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam la
kumtaka Askofu Gwajima kuwasilisha nyaraka hizo leo limesitishwa kusubiri
utatuzi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali au Ofisi ya Mkurugenzi wa
Mashtaka.
Wakili John Mallya anayemtetea Askofu Gwajima alilieleza
gazeti hili jana usiku kuwa baada ya makubaliano na polisi mteja wake leo hatafika
Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kama ilivyokuwa imepangwa
mpaka hoja hizo za kisheria zitakapotolewa uamuzi.
Alhamisi iliyopita, polisi ilimtaka Gwajima kuwasilisha
vielelezo hivyo, lakini hatua hiyo ilipingwa
na kiongozi huyo akieleza kuwa
hatapeleka nyaraka yoyote iwapo jeshi hilo halitajibu barua aliyoliandikia
kutaka liombe vitu hivyo kwa maandishi.
Nyaraka zilizotakiwa kuwasilishwa polisi ni hati ya usajili
wa kanisa, namba ya usajili, majina ya Baraza la Wadhamini (Baraza la Kiroho),
idadi ya makanisa (matawi) anayohudumia na nyaraka za helikopta ya kanisa.
Nyaraka nyingine ni; muundo wa uongozi wa kanisa, waraka wa
maaskofu uliosomwa makanisa yote, nyaraka za nyumba na mali za kanisa, nyaraka
kuonyesha taarifa za hesabu kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Hiari na kuambatana
na mtu anayepiga picha za video kanisani hapo.
“Siwezi kuwasilisha kwa mdomo kwa kuwa hizi si mali za
Gwajima… ni mali ya taasisi na si vitu vyake binafsi,” alisema wakili huyo.
Katika barua yake kwa polisi, Wakili Mallya alisema:
“Tunaiomba Polisi kumwandikia rasmi mteja wetu kimaandishi nyaraka
mnazozihitaji na vifungu vya sheria vinavyotumika na polisi kutaka nyaraka
hizo… tutashukuru kupata hati hiyo.”
Kauli ya Kova
Mapema alipoulizwa kuhusu kitakachotokea leo, Kamanda Kova
alisema: “Suala la Mchungaji Gwajima kwenda na vielelezo alivyoagizwa na Polisi
siwezi kulizungumzia hadi hapo itakapotokea hakuja navyo ndipo nitakapotoa
tamko langu la mwisho.
“Nitazungumziaje hili? Si hadi itokee hakuja na vielelezo na
kama akija navyo halafu mimi nimeongea tofauti, nimeona italeta malumbano kati
yangu na yeye na mimi sitaki ifikie huko.
“Kuna mambo mengi ya kufanya hivyo nitalitolea tamko la
mwisho kwa waandishi wa habari kuhusu mchungaji Gwajima kama itatokea hivyo ili
tuendelee na mambo mengine.”
No comments:
Post a Comment