Pages

Tuesday, April 21, 2015

NYALANDU: UMOJA WETU NDIO UTATUFANYA TUSONGE MBELE

Waziri wa maliasili na utalii, Lazaro Nyalandu akizungumza na aliyewahi kuwa Katibu Tawala wa mkoa wa Arusha, Joshua Kileo (Kulia)  baada ya ibada katika kanisa la KKKT Mjini Kati siku ya Jumapili.
************
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema pamoja na mitihani mikubwa ambayo taifa inakabiliana nayo, umoja wa Watanzania utaifanya nchi isonge mbele kama taifa linalozingatia sheria na demokrasia.


Akizungumza baada ya Ibada ya Jumapili ya Pili ya Pasaka iliyofanyika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mjini Kati jana, Nyalandu alisema nchi itafanikiwa kupita mitihani hiyo kama wananchi wataimarisha umoja kati yao.

“Nchi inapita huku kukiwa na mambo mengi makubwa kufanya…kila mmoja anahitaji amani na hiyo tunaweza kuipata au kufanikiwa kupita salama iwapo tutakuwa na umoja.

“Nchi yetu itasimama, itashinda mitihani ambayo tunayo kama ya uandikishaji wa wapiga kura katika daftari la kudumu, upigaji wa kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa na Uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu,” alisema.

Mapema katika mahubiri yake kanisani, Mteolojia Solomoni Dereva, aliwaomba Watanzania kuliombea taifa kwa Mungu ili liweze kupita kwa utulivu katika kipindi hiki chenye mambo makubwa.

“Tumuombe Mungu pia atuletee viongozi wazuri, wenye sifa ambao watatutoa hapa tulipo na kutufikisha mbele zaidi katika maendeleo,” alisema.

Alisema kiongozi mzuri ni sawa na mchungaji mwema ambaye huanza kuchunga nafsi yake dhidi ya matendo maovu kama rushwa na ubinafsi na pia huchunga familia yake na ofisi aliyokabidhiwa ili kuwatumikia wananchi.

No comments:

Post a Comment