SIKU chache baada ya sehemu ya ukuta wa uzio wa mjengo wa
msanii nyota wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ kuanguka, mtaalam wa
majengo aliyejitambulisha kwa jina la Injinia Stuart Daniel ameupiga zengwe
akidai licha ya kuonekana kuwa na nakshinakshi nyingi, lakini ni dhaifu na
unaweza kudondoka.
Akizungumza na Gazeti la Amani mwanzoni mwa wiki hii baada ya nyota huyo kutupia picha za uzio
wake katika mtandao ukiwa chini kwa
mwereka wa mvua, Injinia Stuart alisema anaamini nyumba ya Diamond imejengwa
chini ya kiwango na mafundi walimchakachua simenti.
MSIKIE MWENYEWE INJINIA
“Kama jengo lote lilijengwa kwa staili hii, basi ni suala la
kusubiri kwa muda tu kabla hatujasikia habari za kuanguka kwake na kama
hatakuwa makini, linaweza kumletea madhara makubwa. “Kitu ambacho ningeweza
kumshauri ni kuwaita wakaguzi wa majengo waangalie mafundi wake walivyojenga
ili kuepuka hasara anayoweza kuipata,” alisema mtaalam huyo.”
ACHAMBUA UJENZI ULIVYO
“Kuna kitu katika ujenzi tunaita ratio (uwiano) kati ya
mchanga wa kujengea na simenti. Huu mchanganyiko inabidi ukamilike kutegemea urefu,
unene na ukubwa wa kinachojengwa, kitu chochote kikipungua, matokeo yake ndiyo
haya, mafuriko kidogo au tetemeko dogo tu linaweza kuporomosha jumba zima,”
alisema Injinia Daniel.
WALICHOSEMA WANAOMJUA DIAMOND
Amani pia lilizungumza na baadhi ya watu wa karibu wa
Diamond ambao walisema kuwa, tatizo lililomtokea staa huyo linatokana na tabia
ya umaarufu.“Unajua watu maarufu na wenye pesa, wanapojenga wanapenda sana
kuwasiliana na mafundi wao kwa njia ya simu. Utakuta mtu yupo mjini,
anawasiliana na fundi yupo saiti, fundi anaomba shilingi laki moja anunulie
simenti, inatumwa kwa njia ya mitandao ya pesa.
“Sasa hapo unategemea nini? Fundi atatumia elfu hamsini,
elfu hamsini ataweka ndani. Ndiyo maana ukiangalia ukuta wa nyumba ya Diamond
ulioanguka, nondo zilikuwa nyembamba sana na inaonekana hata simenti ilikuwa
chache kwenye matofali,” alisema mmoja wa watu hao akiomba jina lake
lisiandikwe gazetini.
Mwingine alisema: “Ki ukweli Diamond ‘amepigwa’ na mafundi
kwenye ile nyumba. Iko haja ya kuchukua wataalam wa majengo wakakague ili kama
ni kweli mpaka matofali yaliyotumika kujengea nyumba kubwa yako chini ya
kiwango, achukue hatua. Lakini mwenyewe anakimbilia kusema mafundi ni wawili
tofauti.”
DIAMOND AULIZWA, AKIRI KUCHAKACHULIWA
Baada ya maelezo hayo yote, Amani liliwasiliana na Diamond na kumuuliza kuhusu zengwe hilo
linalodaiwa amepigwa kwenye mjengo wake aliohamia hivi karibuni.Kwanza alikiri
suala la mafundi waliojenga awali kufanya uchakachuaji wa kutumia simenti
kiduchu na nondo zisizositahili.
“Ni kweli, wale mafundi nimeambiwa kwa jinsi walivyojenga,
walichakachua simenti. Hata hivyo, kwa kulitambua hilo nimechukua mafundi wapya
na kazi inayorudiwa sasa ni ya uhakika zaidi. Huu ujanjaujanja uliofanyika hata
mimi sijakubaliana nao.”
Amani: “Kwa hiyo unarudia ujenzi wa nyumba yote?”
Diamond: “Aaa! No! Unajua mafundi waliojenga ule ukuta
ulioanguka siyo waliojenga nyumba kubwa. Ni mafundi wawili tofauti. Kwa hiyo
nina imani nyumba kubwa ipo sawasawa.”
Amani: “Baadhi ya marafiki zako wanasema fundi ni mmoja ila
unasema ni wawili ili usibanwe kuhusu kuirudia nyumba kubwa.”
Diamond: “Hamna bwana! Waliojenga ukuta wa uzio siyo wa
nyumba kubwa. Ndiyo maana nimewaita wengine kujenja upya uzio. Unajua naishi
kwa wasiwasi, maana kama wale walichakachua si ipo siku unaweza kukuta ukuta
wote chini na wezi wameingia, nakuwa na wasiwasi sana.”
INJINIA ARUDIWA
Baada ya Diamond kuzungumza hayo kuhusu mafundi wa nyumba
kubwa kuwa wengine na mafundi wa uzio, Amani lilimrudia Injinia Daniel na
kumuuliza kuhusu sheria ya ujenzi wa aina hiyo inasemaje.“Hapo sasa ni ujenzi
holela! Mjenzi anatakiwa kuwa mmoja tu. Huyohuyo wa nyumba kubwa anatakiwa
amalizie na uzio kama mtu ataamua kuweka uzio.
“Ndiyo maana huwa tunawataka watu wafuate sheria za kuajiri
wajenzi wenye viwango vya kisheria ili waweke na ule ubao wa maelekezo ya
ujenzi.“Kwa kawaida kile kibao kina maelezo ya; project (mradi), contractor
(mjenzi), client (mteja), consultant (mshauri), supervisor (msimamizi). Kuna
mabango mengine hadi mtoa pesa ambaye ni financier anaandikwa pia na siku ya
kuanza ujenzi na makadirio ya kumaliza.”
No comments:
Post a Comment