Jeshi la Polisi mkoani Morogoro, linamshikilia mkazi wa
Manispaa hiyo, Josephat Asenga (47), mwenye taaluma ya uhasibu, kwa tuhuma za
kujifanya Padri.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, alisema
kuwa, Asenga alikamatwa juzi saa 10:30 jioni, katika maeneo ya Modeco, Kata ya
Mazimbu katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Maria.Kwa mujibu wa Kamanda
Paulo, mtuhumiwa
huyo alifika parokiani hapo Juni mwaka jana akiwa amevaa
mavazi ya Padri na kujitambulisha kwa Paroko wa parokia hiyo, Malt Dyfrig
Joseph, kuwa yeye ni Padri anaishi Jimbo la New York Marekani.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, baada ya kujitambulisha kwa
Paroko huyo na kuonesha kitambulisho chake, alimuomba Paroko huyo kumpangia
zamu ya kuendesha Misa ya Jumapili iliyofuata na kukubaliwa na Paroko huyo bila
kukagua vizuri kitambulisho chake.
Alisema mara baada ya misa hiyo, Paroko alipata taarifa
kutoka kwa msamaria mmoja wa Kituo cha Amani cha Chamwino mjini hapa, kuwa
Padri huyo feki anaishi na mwanamke katika maeneo ya Ujenzi kinyume na taratibu
za upadri.
Baada ya kupata taarifa hizo, inadaiwa Paroko huyo aliwaomba
waumini wamshawishi Padri huyo feki, afike parokiani hapo na baada ya kufika,
alihojiwa na Paroko huyo na kudai kuwa alipata upadrisho katika Jimbo Kuu Katoliki
Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, baada ya Paroko huyo kupata
maelezo hayo alifanya mawasiliano na Katibu wa Jimbo hilo la Dar es Salaam na
kujibiwa kuwa hakuna jina la Padri huyo.
Juzi Alhamisi majira ya saa 10:30, Padri huyo feki alimpigia
simu Paroko huyo na kumuomba ampange kuendesha Misa Takatifu ya Jumapili
parokiani hapo, na kukubaliwa na paroko huyo na kumtaka afike kanisani.
Baada ya kufika, taratibu za kujulisha Polisi zilifanywa na
askari walipofika kanisani hapo, walimkamata mtuhumiwa huyo.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, baada ya kufanya mahojiano na
mtuhumiwa, alikiri kuwa yeye sio Padri na walipokwenda nyumbani kwake kwa ajili
ya kufanya upekuzi, walimkuta akiwa na majoho saba ya upadri.
Mtuhumiwa huyo ameendelea kushikiliwa Polisi na atafikishwa
mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika
No comments:
Post a Comment