Dar es Salaam. Serikali imeanza kutimiza ahadi yake ya
kuyafuta mashirika na asasi zisizo za kiserikali, NGO, yakiwamo ya kidini na
kwa kuanzia imetangaza kusudio la kuzifuta asasi 24 katika kipindi cha siku saba
kuanzia jana.
Miongoni mwa asasi hizo ni taasisi mbili za dini ambazo ni
Tanzania Muslim Social Community na Tanzania Christian Outreach Ministries
ambazo zimepewa siku saba kujitetea.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Issack Nantanga
aliliambia gazeti hili kuwa asasi zote zitakazothibitika kwenda kinyume na
malengo ya kuanzishwa kwake, zitafutwa.
Nantanga pia alisema panga hilo litazipitia pia asasi ambazo
zimekuwa haziwasilishi kwa msajili ada ya kila mwaka na taarifa za fedha
zilizokaguliwa na wakaguzi waliosajiliwa.
“Haya mashirika 24 ndio tumeanza nayo na ukaguzi unaendelea.
Tumetoa muda wa siku saba kuanzia leo (jana) kujitetea kwanini yasifutwe na
wakishindwa kufanya hivyo, yatafutwa rasmi,” alisema.
Aliyataja mashirika mengine kuwa ni Kagwa Development
Society, Morning Star Production Training Centre, Chama cha Kujitegemea na
Kujiendeleza na The Organisation of Tanzania Community.
Mashirika mengine ni Mbezi Juu and Salasala Woman
Agricultural and Environmen Association, Waridi Training Society, Vituka
Machimbo Development Association na Gerezani Nguvukazi.
Mengine ni Nyakasangwe Small Scale Farmers Association,
Vitendo Trust Fund, Bahari Beach Silvers and Woman Association, Owners Social
Club na Magovent Development Association.
Kwa mujibu wa Nantanga, mashirika mengine yaliyomo katika
orodha hiyo ni Hananasifu Quarters Women Association, Mburahati Barafu
Development Community na The Movers Club.
Pia yamo Umoja wa Maendeleo ya Jamii Mlima Mindu, Tabata
Tujiimarishe Club, Umoja wa Wauza Miche Ubungo, Kunguru/Kinzudi Development
Association na Women & Environment Association.
“Ukitazama katika tovuti ya wizara utakuta tuna orodha ya
mashirika 10,624 yaliyosajiliwa tangu 1953. Tutapitia moja baada ya jingine na
yatakayobainika kukiuka sheria yatafutwa,” alisisitiza.
Wakati Serikali ikianza mchakato huo, imebainika kuwa baadhi
ya klabu za waandishi wa habari za mikoa, nazo ziko hatarini kuangukiwa na
rungu hilo kwa kutolipa ada. Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa baadhi ya
klabu hizo za waandishi wa habari hazina taarifa za fedha zilizokaguliwa na
wakaguzi waliosajiliwa na wala taarifa hizo haziwasilishwi kwa msajili.
No comments:
Post a Comment