Siku
moja baada ya Wakala wa Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini
(SUMATRA) kutangaza kupungua kwa mwendo kasi wa mabasi yaendayo mikoani
hadi kufikia spidi 80, wasafiri jijini Mwanza wamekumbana na adha kubwa
ya kukosa usafiri baada ya mabasi kutoka Dar es Salaam kushindwa kufika
kwa wakati mjini hapa.
Katika
stendi kuu ya mabasi eneo la Nyegezi jijini hapa, wasafiri hao walisema
kauli hiyo ya serikali itawaumiza, hivyo wameiomba kuwasaidia kwa
kuisihi iruhusu safari kwa mwendokasi wa kawaida, vinginevyo wao ndiyo
wanaopata maumivu.
Walisema
walikata tiketi mapema lakini wameshindwa kusafiri kutokana na
msongamano mkubwa wa watu na hata wakipanda, magari hayo hayaondoki.
Mmoja
wa mawakala wa mabasi ya kampuni moja, alisema hatuwezi kuendelea
kuharibu magari yao kisa spidi 80, hivyo ni bora wakaegesha magari yao
kusubiri ya serikali yatakayokuwa na spidi 80 ili yafanye kazi hiyo.
Madereva
wa magari hayo, ambao walikataa kuondoka stendi licha ya abiria
kupanda, walisema ni vigumu kwa mabasi hayo yenye spidi 180, kusafiri
kwa mwendo unaotakiwa na SUMATRA kwani kwa kufanya hivyo magari hayo
yataharibika mapema.
“Serikali
ni wavivu wa kukagua magari mabovu ambayo kwa asilimia kubwa ndiyo
yanayosababisha ajali na pia kwenye haya magari, baadhi ya madereva
hawajakidhi viwango, wao wanatakiwa kuwakagua hawa ili wabaki wenye
vigezo, kusema magari yaende kwa spidi 80 ni kujisumbua kwani hakuna
mmiliki atakayekubali,” walisema baadhi yao.
Mpaka
mwandishi wa habari hizi anatoka kwenye stendi hiyo majira ya saa 5
asubuhi hakuna basi hata moja lililokuwa limewasili kutoka jijini Dar.
No comments:
Post a Comment