Dar es Salaam. Treni ya kisasa (Delux), kwenda Bara yenye
mabehewa 22 ilianza safari yake ya saa 30 kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma
ikiwa ni tofauti ya saa sita ikilinganishwa na safari ya treni ya zamani.
Kutokana na tofauti hiyo, abiria walioanza safari kwa furaha
na matumaini jana saa tano asubuhi wanatarajiwa kufika Kigoma leo saa 11 jioni
badala ya saa tano usiku.
Hata hivyo, abiria hao watalazimika kuingiza mikono yao
zaidi mifukoni, kutokana na kiwango kipya cha nauli kuwa Sh79,400 badala ya
Sh75,700 za awali kwa daraja la kwanza.
Huku nauli za daraja la pili ikishuka kutoka Sh55,400 hadi
Sh,47,600 zile za daraja la tatu zimepanda kutoka Sh27,700 hadi Sh35,700.
Kwa mtazamo wa haraka, mabehewa hayo yanavutia
yakilinganishwa na yale ya awali yaliyokuwa yamekithiri kwa uchakavu,
yaliyokuwa yamejaa mende na yenye milango na madirisha mabovu.
Mabehewa hayo yana viti vya kutosha, huduma ya intaneti,
swichi za umeme za kuchajia simu na kuunganisha kompyuta na safari zake
zimeongezeka kutoka mbili hadi tatu kwa wiki.
Akizungumza muda mfupi kabla uzinduzi huo, Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRL), Mhandisi Kipallo Kisamfu alisema
wamelazimika kupandisha viwango vya nauli kutokana na gharama zitakazokuwa
zinatumika katika uendeshaji wa treni hiyo.
“Licha ya kuongeza kidogo kiwango cha nauli, dhamira yetu ni
kuwapatia abiria huduma safi na ya raha... kila msafiri atasafiri akiwa ameketi
kwenye kiti chake. Hakuna abiria atakayesafiri akiwa amesimama,” alisema na
kuongeza: “Treni inayozinduliwa leo inatumia mabehewa mapya 22 yaliyonunuliwa
kutoka Korea Kusini na kichwa cha treni kiliundwa upya kwenye karakana ya TRL
iliyopo Morogoro mabehewa mapya yamegharimu Serikali Sh28.6 bilioni.”
Kuhusu vituo vya ambavyo treni hiyo alisema itasimama kwenye
vituo vikubwa ambavyo vingi ni vile vya miji, wilaya na mikoa.
Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Dk Shabaan Mwinjaka
aliwataka abiria kuwa walinzi wa treni hiyo ili kuhakikisha usafiri huo
unadumu.
“Kumekuwa na tabia ya watu kujiamulia kuharibu mali za umma,
ninawaomba abiria mtakaopanda treni hii muwe walinzi wa wenzenu kwa sababu
baadhi ya abiria wamekuwa na tabia ya kuchora kwenye viti,” alisema Dk
Mwinjaka.
Mmoja wa abiria, Saida Roman alisema Serikali inahitaji
kupewa pongezi kwa hatua hiyo kwani hivi sasa abiria wanaotumia usafiri wa
treni kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma watasafiri kwa raha tofauti na
ilivyokuwa zamani.
No comments:
Post a Comment