KATIKA hali isiyo ya kawaida, mkulima kutoka Kijiji cha Mjimtala Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma, Eldoforce Bilohe (43) jana alitinga makao makuu ya Chama Cha Mapindizi (CCM) kuchukua fomu ya kuomba ridhaa kuteuliwa kuwa mgombea urais, bila kuwa na ada huku akiwa amebeba maji ya chupa kwapani.
Bilohe ambaye alisema elimu yake ni ya darasa la Saba, aliwasili
makao makuu ya CCM muda wa saa 5:40 asubuhi na kuelekea Ofisi ya kupokea
wagombea ndani ya ofisi baada ya kuwapita waandishi wa habari wakiwemo
wapiga picha, waliokuwa wamejipanga kumsubiria, lakini aliwapita
waandishi bila kumtambua kuwa ni mgombea.
Akiwa amevaa suruali ya kaki na fulani yenye rangi ya kijani na
njano, alionekana kuduwaza watu wengi, ambao walikuwa wakiwasuburi
wagombea, ambao walikuwa wakichukua fomu jana.
Akiwa kati ya watu waliokuwa kwenye orodha ya kuchukua fomu, Bilohe
alikuwa amebeba chupa ya maji kwapani baada ya kufika na kupokelewa na
maafisa, ambao walimtambua kuwa ni mgombea na ndipo wapiga picha
waligutuka na kuanza kupiga picha.
Kisha aliingia ndani ya ofisi ya kuchukua fomu na alitoka baada ya muda mfupi na kuanza kuhojiwa na waandishi wa habari.
Alisema amefika Dodoma kwa ajili ya kuchukua fomu ya kuteuliwa kuwa
mgombea urais, lakini kwa sababu ambazo hazijafahamika, aliambiwa
akachukue fedha.
“Nilipigiwa simu wakati niko benki ya CRDB nikiwa kwenye foleni,
nikisubiri kuchukua fedha, ndiyo nikakimbia kuja hapa,” alisema.
Alisema amekuwa mwanachama hai wa CCM tangu mwaka 2003 na elimu yake
ni ya msingi na ana uzoefu kutokana na kuwa katika chama kwa muda mrefu.
“Nimekuja kama nilivyo kwa sababu sijawahi kuwa na makundi unayoyaona
wewe, mimi ni mwanachama wa kawaida kama wanachama wengine,” alisema.
Mmoja wa maofisa wa chama, ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema
Bilohe amerudishwa si kwa sababu hana hela, bali kuna vigezo ambavyo
havijafikiwa, ikiwemo barua ya utambulisho kutoka kwa Katibu wa CCM
Wilaya aliyotoka.
“Hajakamilisha taratibu za kumwezesha kuhukua fomu,” alisema.
Hata
hivyo, taarifa zilizopatikana baadaye zilisema kuwa tayari mkulima huyo
ameshalipia ada ya fomu ya Sh 1,000,000 na atachukua fomu yake leo saa
10 jioni.
No comments:
Post a Comment