Kwa Afrika Mashariki, Kerr ni jina geni lakini
katika kazi ya ukocha si jina geni kwani amewahi kuifanya kazi hiyo
katika klabu mbalimbali nchini Afrika Kusini pamoja na Vietnam.
Sambamba na kuifanya kazi hiyo, Kerr pia ni
mtaalamu wa viungo kama alivyokuwa msaidizi wa zamani wa kocha wa Stars,
Itamar Amorin ambaye baadaye alikuwa kocha mkuu wa klabu ya Azam.
Kerr pia amewahi kucheza soka la kiwango cha juu
akiwa beki wa kushoto akizichezea klabu zilizowahi kutamba kwenye Ligi
Kuu England za Sheffield Wednesday, Leeds United na Reading.
Ukiachana na historia yake na kuizungumzia kazi
yake mpya ya kuinoa Simba, Kerr ni mgeni kwa maana ya kwamba hana uzoefu
sana na nafasi ya ukocha mkuu.
Katika timu nyingi alizowahi kuzifundisha rekodi
zinaonyesha kwamba ni timu moja tu ambayo alikuwa kocha mkuu, Hi Phòng
ya Vietnam aliyoanza kuinoa akiwa msaidizi kabla ya kuwa kocha mkuu na
kuiwezesha kutwaa taji la Vietnam. Hatusemi kwamba sifa zake
zinamuondolea heshima ya kuwa kocha wa Simba, tunaamini uzoefu alionao
unatosha kuinoa timu hiyo.
Tunachotaka kusisitiza hapa ni kwa viongozi Simba
kujipanga ili kuhakikisha kocha wao mpya anafanya kazi yake kwa amani
ili atakapoharibu waweze kumbana.
Tunasema hivyo kwa sababu kama tulivyosema awali
Kerr ni mgeni na soka la Tanzania, na zaidi ya hilo hatutarajii ashiriki
kikamilifu kwenye usajili wa wachezaji, atakabidhiwa Simba
iliyoandaliwa na watu wengine. Kwa muda ambao ataanza kufanya kazi
viongozi wa Simba wajipange kuhakikisha matatizo madogo madogo hayapewi
nafasi ya kuvuruga mipango yake. Kwa mfano kuna wakati kiungo wa Simba,
Hassan Kessy alisusa kuichezea Simba wakati ligi ikiendelea kwa sababu
uongozi ulikuwa haujamtimizia ahadi zake.
Haya ni kati ya mambo ambayo tusingependa yaibuke wakati kocha wa Simba akianza kazi.
Kwa mantiki hiyo viongozi wa Simba ambao
wanaendelea na harakati za usajili wa wachezaji waliangilie hilo kwa
umakini wa hali ya juu. Usajili wa aina yoyote ni lazima uzingatie uwezo
wa klabu na viongozi wajipange kuhakikisha ahadi wanazowapa wachezaji
zinaheshimiwa kwa wakati.
Kutoheshimu ahadi za wakati wa kuwasajili
wachezaji inaweza kuwa sababu ya Kerr naye kuonekana hafai na kutimuliwa
au kuondoka mwenyewe. Ni vyema wachezaji ambao kocha atawakuta na
kufanya nao mazoezi awe na uhakika wa kuwatumia mwanzo hadi mwisho wa
msimu ili kazi yake iwe rahisi.
No comments:
Post a Comment