Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Wednesday, June 3, 2015

Vipaumbele Vya Profesa Sospeter Muhongo,Mara baada ya Kutangaza Nia Musoma‏


Profesa Muhongo: Mwenye uwezo wa kuikwamua Tanzania ni mimi
* Atangaza nia kwa kutoa takwimu za umasikini na utajiri
*Asema viwanda, gesi, umeme utaipaisha Tanzania

NA MWANDISHI WETU, MUSOMA
WAZIRI wa zamani wa Nishati na Madini Sospeter Muhongo, ametangaza nia rasmi ya kuwaomba Wana CCM kumteua kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Oktoba, huku akisema ni yeye pekee mwenye uwezo wa kuikwamua nchi katika hali mbaya ya umasikini na ukosefu wa wataalamu, hali inayoifanya nchi ishindwe kupiga hatua.

Pamoja na mambo mengine, Muhongo alitumia muda mwingi kutoa takwimu hali ya umasikini na utajiri kwa wananchi wa Tanzania, bila kusahau baadhi ya nchi ambazo zimeweza kupiga hatua kubwa kwa kujikita kwenye kuzalisha wataalamu na watafiti, akiwamo yeye, ambaye si tu ni Profesa, bali pia amebobea kwenye nishati kwa miaka mingi.

Akizungumza kwa kujiamini mbele ya wanachama wa CCM na Watanzania katika Ukumbi wa Chuo Kikuu Huria, Musoma Mjini, Profesa Muhongo alisema kwamba anayo tiba ya umasikini wa Watanzania kwa kuhakikisha kwamba anatumia utaalamu wake kwa kusimamia mambo ya gesi, mafuta, umeme, bila kusahau elimu kwa ajili ya kuwakwamua wananchi wake.

“Nchi ina upungufu mkubwa wa takwimu hali inayowafanya viongozi washindwe kujua namna gani wanaweza kuondoa umasikini na kero zinazowakumba wananchi wake, hivyo hata wale wanaosema wanataka uongozi, hawajui wangapi wenye uhitaji.

“Ukiacha takwimu ambayo kwa Dunia ya sasa ni lazima, nchi yetu lazima ijiamini, kuongeza ushindani, kuongeza upendo, bila kusahau rushwa ambayo kwa uhakika inapaswa kupigwa vita kwa vitendo ili nchi yetu isonge mbele,” alisema Muhongo.

Kuhusu uchumi, Profesa Muhongo alisema kwamba ni aibu Tanzania kupitwa kiuchumi na Mataifa waliyokuwa nayo sawa, akitolea mfano wan chi za Brazil, China, India na Kenya ambao wao wamewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye elimu na utafiti.

Alisema nchi ikiwa na watafiti, wananchi wao hawataishi kwa mashaka, huku akisema endapo atapitishwa kuwania nafasi hiyo na kuwa rais wa Tanzania, atahakikisha kwamba anakuza uchumi wan chi kutoka asilimia 7.5 hadi asilimia 10 na 15 kwa kipindi cha miaka mitano hadi 10 ya urais wake.

“Nimeweza kufanya kazi ya gesi na mafuta kwa miaka kadhaa kwenye nchi mbalimbali, hivyo hakika kama chaguo ni wataalamu, basi mimi nastahili kwa sababu sioni mwingine mwenye uwezo wa kutangaza kuondoa kero za Watanzania na jinsi atakavyoziondoa.

“Ndio unaweza kusema utaondoa umasikini kwa wananchi au kuongeza mishahara, lakini ili hilo liweze kufanikiwa kwa vitendo, ni lazima pia katika kipindi cha uongozi wako uweze kukuza uchumi wako kwa kiasi kikubwa, bila hivyo hakuna kitu,” alisema Muhongo.

Aidha Profesa Muhongo alisema kwamba Duniani kote nchi zimepiga hatua kwa kuwekeza kwenye wataalamu na viwanda, hivyo Tanzania inapaswa kuangalia namna ya kuwekeza kwenye sekta hizo, bila kusahau sekta ya elimu yenye umuhimu mkubwa.

Katika hatua nyingine, Profesa Muhongo alisema kwamba akiwa Waziri wa Nishati na Madini, ndio mtu ambaye alifanikiwa kwa vitendo kutekeleza ilani ya CCM kwa kuhakikisha kwamba vijiji vingi vinapata umeme kwa kuongeza bajeti na kusimamia kwa vitendo wakala wa umeme vijijini (REA).

Alisema kusudio la kuhakikisha kwamba wananchi wake wanaendelea kupata umeme kwa bei nafuu ni kati ya mambo anayoona yanafaa kuongezewa chapuo na usimamizi wa aina yake, hivyo mwenye uwezo wa kulitatua hilo ni yeye.

No comments:

Post a Comment