Waandishi Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam/Sumbawanga. Mkutano Maalumu wa Chadema Jimbo
la Temeke umempitisha Bernard Mwakyembe kugombea ubunge katika jimbo hilo.
Mwakyembe (33) alipata ushindi wa asilimia 66.7 kwa kuvuna kura 80 kati ya 120
katika mkutano uliotaka kuingia rabsha baada ya wajumbe kutoka Kata ya Sandari
kuzuiwa kupiga kura kutokana na kutokidhi vigezo vya katiba.
Msimamizi wa uchaguzi huo, Halfan Milambo alisema mgombea
Emmanuel Msuya alipata kura 39 sawa na asilimia 32.5 huku Mhandisi Samson
Msambaza akipata kura moja sawa na asilimia 0.8. Mwakyembe ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Temeke, iwapo atafanikiwa kupitishwa na Kamati
Kuu ya chama hicho, atasubiri kihunzi cha mwisho ndani ya Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) kabla ya kuvaana na CCM na vyama vingine. Hata hivyo, baadaye
wagombea hao walipopigiana kura wenyewe kwa wenyewe kumchagua anayefaa
kupeperusha bendera ya Chadema, mgombea wa mwisho wa kura za mkutano mkuu
aliibuka mshindi. Milambo alisema katika kura hizo za kupigiana, Mwakyembe
alishika nafasi ya pili huku Msuya akifunga pazia.
Wajumbe 120 kati ya 145 wa
Mkutano Mkuu Jimbo la Temeke ndiyo waliopiga kura jana mchana.
Sintofahamu Ukonga
Hali ya sintofahamu
iliibuka jana wakati wa mchakato wa upigaji kura ya maoni Jimbo la Ukonga baada
ya baadhi ya wajumbe wa Serikali za Mitaa na wanachama wengine kutoruhusiwa
kuingia mkutanoni. Hali hilo ilisababisha shughuli kusimama kwa muda huku
viongozi wakijitahidi kueleza taratibu za mkutano huo na watu wanaotakiwa
kushiriki. Hata hivyo, Mjumbe wa Mtaa wa Kivule, Chacha Marwa alisema walifika
eneo hilo kuwasikiliza wagombea.
Mwanachama mwingine, Abdallah Khalfan alisema viongozi wameanza kuwagawa
wanachama bila sababu za msingi. Akitoa ufafanuzi juu ya utaratibu wa mkutano
huo, Kaimu Mratibu wa Chadema Kanda ya Pwani, Casmir Mabina alisema waliotakiwa
kupiga kura ni wajumbe wa kamati ya utendaji na wenyeviti wa Serikali za Mitaa
katika jimbo husika. Baada ya ufafanuzi huo, mkutano ulianza na hadi saa moja
usiku ulikuwa ukiendelea.
Malila apeta Sumbawanga
Katika Jimbo la Sumbawanga Mjini, Shadrick Malila aliibuka
na ushindi wa kishindo. Msimamizi wa uchaguzi huo, Ofisa wa Chadema Kanda ya
Nyasa, Paschal Ngaiza alimtangaza Malila ambaye ni mfanyabiashara maarufu kwa
jina la Ikuwo kuwa ni mshindi kwa kura 280 akifuatiwa na mfanyabiashara
mwingine, Cassiano Kaegele ‘Upendo’ aliyepata kura 30. Wagombea wengine, na
kura zao Mussa Ndile (10) Baraka Lyimo (3), Eliud Mwasenga (2) na James Kusula
(1).
Imeandikwa na
Nuzulack Dausen, Peter Elias na Mussa Mwangoka.
No comments:
Post a Comment