Dar/Arusha. Licha ya Baraza Kuu la Uongozi la Chama cha
Wananchi (CUF) kupokea taarifa ya Ukawa na kuamua chama hicho kiendelee
kushiriki katika umoja huo, bado suala la mgombea urais wa vyama vinavyounda
umoja huo limeendelea kuwa siri nzito.
Taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya CUF jana, zilisema
kuwa katika kikao chake kilichoketi juzi na jana mjini Zanzibar, baraza hilo
lilipokea taarifa ya Ukawa, kuithibitisha na kuamua chama hicho kiendelee na
ushirikiano huo.
Mkutano wa waandishi wafutwa
Pamoja na hayo, jana kutwa nzima viongozi wa Ukawa walikuwa
kwenye vikao mfululizo na hakukuwa na taarifa rasmi zilizopatikana na hata
mkutano na waandishi wa habari ulioitishwa jana jioni uliahirishwa bila kueleza
utaitishwa tena lini.
Ingawa taarifa ya mkutano wa Ukawa na wanahabari haikutaja
ajenda, habari zilizoenea katika mitandao ya kijamii zilibainisha kuwa walikuwa
wanakusudia ama kutangaza chama kilichopitishwa na Ukawa kusimamisha mgombea
urais au kutangaza jina la mgombea mwenyewe pamoja na mgombea mwenza.
Vyanzo mbalimbali ndani ya Ukawa, vilieleza kuwa ufunguo wa
hatua hiyo ulikuwa unashikiliwa na CUF, ambayo hivi karibuni ilijitenga na
umoja huo ili masuala yake yajadiliwe kwanza na vikao vyake vya maamuzi kabla
ya kurejea kwenye meza ya majadiliano.
Taarifa za uhakika kutoka katika kikao hicho kilichoketi
Zanzibar kwa siku mbili, zilibainisha kuwa wajumbe waliafikiana kinyume na
ilivyotarajiwa kuwa wangevurugana.
Miongoni mwa mambo ambayo inadaiwa wameafikiana ni kuwa
mgombea urais atoke Chadema na chama hicho kitoe mgombea mwenza.
Jussa: Watanzania mtafurahi
Hata hivyo, mmoja wa wajumbe wa baraza hilo, Jussa Ismail
Ladhu alipoulizwa alisema ikiwa itaamuliwa mgombea mwenza wa Ukawa atoke CUF,
hakutakuwa na shida kwa kuwa chama hicho kina wanasiasa wazuri, safi na makini
na kwamba kitatoa mtu ambaye Watanzania wote watafurahi.
“Ikiamuliwa kuwa mgombea mwenza atoke CUF, wananchi msiwe na
wasiwasi, CUF ina hazina nyingi, itatoa mtu bora, itawapa chaguo ambalo
Watanzania wote wataridhika nalo,” alisema Jussa.
Pamoja na kuthibitisha kuwa Baraza hilo limeamua CUF
iendelee kushiriki katika umoja huo, Jussa alisema kwenye mjadala matatizo
kidogo yalikuwapo katika mgawanyo wa majimbo.
Hata hivyo alisema baada ya kuweka vigezo vya kuwa na
mgombea wa Ukawa, sasa hakuna shida kwa kuwa majimbo machache yaliyosalia
utaratibu wake utatangazwa hivi karibuni.
Kuhusu mgombea mwenza, Jussa alisema CUF ina nafasi kubwa ya
kutoa mgombea huyo kwa sababu ndicho chama chenye nguvu Zanzibar na kina
wanasiasa mahiri na makini.
Wagombea wetu tunataka wawe ni wale watakaohakikisha kuwa
Katiba Mpya inapatikana mara baada ya uchaguzi ili kuyaweka sawa mambo
yanayohitaji kuwekwa sawa.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Katiba, mgombea urais na mgombea
mwenza wanapaswa kutoka chama kimoja, hivyo kama Chadema itamtoa mgombea urais
inabidi pia mgombea mwenza atoke chama hicho.
Habari ambazo bado si rasmi zinasema kuwa mmoja wa viongozi
wa CUF anaweza kuhamia Chadema ili kukidhi matakwa hayo ya Katiba.
Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Habari, Uenezi na
Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salim Bimani alisema kuwa mambo katika Ukawa ni
mazuri, wapo waliofikiri kuwa watavurugana, lakini wamekubaliana na sasa
Watanzania wasubiri kupata wagombea safi katika ngazi zote.
Bimani alisema CUF kitaendelea kushirikiana na vyama vingine
vya upinzani nchini ili kuhakikisha demokrasia inazidi kukua.
Vikao mfululizo Chadema
Habari zaidi zilizolifikia gazeti hili zilisema mshirika
mwingine wa Ukawa, Chadema jana viongozi wake walikuwa katika kikao cha dharura
cha Kamati Kuu kilichoshirikisha wajumbe wachache, hasa wale wanaopatikana kwa
kupigiwa kura ili kuweka mambo sawa.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini
Makene alikiri kuwapo kwa kikao hicho.
“Kamati Kuu ya Chadema inaendelea kukutana jijini Dar es
Salaam kwa kikao maalumu cha dharura kujadili mambo mbalimbali,” alisema Makene
katika taarifa yake fupi aliyotuma jana usiku.
“Mambo hayo ni pamoja na maandalizi ya chama kuelekea
uchaguzi mkuu, kupokea taarifa za mwenendo wa kura za maoni na uteuzi wa awali
wa nafasi za ubunge wa majimbo na viti maalumu zinazoendelea nchini nzima,”
alisema Makene.
Habari za ndani ya kikao hicho kilichofanyika katika Hoteli
ya Bahari Beach jijini Dar es Salaam, zilisema kuwa kilikuwa na jukumu la
kupokea taarifa ya utafiti iliyofanywa nchini kote kuhusu mgombea anayekubalika
zaidi.
Ingawa hakukuwa na taarifa rasmi kuhusu utafiti huo, lakini
taarifa zinazoendelea kusambaa zinalitaja jina la waziri mkuu wa zamani, Edward
Lowassa kuwa yuko mbioni kuhama chama chake cha CCM na kwenda Chadema, huku
mgombea mwenza akitajwa kuwa atatoka upande wa Zanzibar CUF.
Mgombea mwenza kuhamia Chadema
Habari za ndani ya Ukawa zinasema chini ya makubaliano ya
Ukawa ikiwa mgombea urais atatoka Chadema, mgombea mwenza akitoka chama kingine
itabidi ahame chama chake ili aingie chama alicho mgombea urais ili kukidhi
matakwa ya kikatiba.
“Tutakaposhinda uchaguzi, kama makamu wa rais atatoka CUF
itabidi kila akitoka katika ofisi ya makamu wa rais, kituo cha kwanza atasimama
Makao Makuu ya CUF kwa ajili ya kupeleka taarifa na kupata baraka za chama
katika masuala muhimu.”
Chanzo chetu cha habari kinasema: “Ikiwa Ukawa tutashinda Uchaguzi Mkuu Oktoba
25 na kupata nafasi ya urais, jambo la kwanza litakuwa ni kufanya Mabadiliko ya
Katiba na kuruhusu demokrasia pana ya watu kuungana.”
Alisema hakuna ajabu yoyote kwa rais kutoka chama kimoja na
makamu wa rais kutoka chama kingine.
“Hilo hata sasa linatendeka Zanzibar ambako Rais na Makamu
wa Kwanza wa Rais wanatoka vyama tofauti na hakuna matatizo yoyote katika
utendaji wa Serikali, kila mmoja anasimamia kwanza maslahi ya Taifa pili kuhakikisha
sera za chama chake zinatekelezwa,” kilieleza chanzo cha habari.
Lowassa atajwa
Hii ndiyo ajenda ambayo imetawala mijadala kuhusu fununu za
Lowassa kuhama CCM kwenda Chadema ili kukamilisha safari yake ya matumaini.
Gazeti hili linafahamu kuwa mazungumzo na Lowassa
yamekwishafikia hatua nzuri ingawa kulikuwa na viongozi wachache ndani ya
Chadema waliokuwa wameshikilia msimamo wa kumkataa lakini kutokana na presha
iliyopo ndani na nje ya chama wasingefua dafu.
Mtei amkaribisha
Huku mjadala kuhusu Lowassa ukizidi kukolea, mwasisi wa
Chadema, Edwin Mtei amemkaribisha mwanasiasa huyo na makada wengine wa CCM
kujiunga na chama hicho kikuu cha upinzani.
Akizungumza na Mwananchi jana, Mtei alisema kwa sasa Chadema
na Ukawa wanahitaji kura za kutosha kuing’oa CCM, hivyo hata kura ya mtu mmoja
ni muhimu.
“Nimesikia Lowassa anatajwa kutaka kujiunga na Chadema, mimi
namkaribisha aje, si yeye tu, aje na makada wengine wa CCM kwa kuwa tunapaswa
kuimarisha nguvu za kuiondoa CCM madarakani,” alisema.
Alisema Chadema ni chama cha Watanzania wote hivyo hakiwezi
kumfungia milango Mtanzania mwenye sifa za kujiunga na chama hicho asijiunge.
Hata hivyo, Mtei alisema makada hao wa CCM ambao wanataka
kujiunga na Chadema endapo watakuwa na nia ya kupata uongozi, wajue kuna vikao
vya kuwapitisha.
“Tunawakaribisha Chadema makada wote wa CCM bila masharti na
kama wana nia ya uongozi Chadema ina vikao vya kupitia kulingana na sifa zao na
vikao vitakuwa na maamuzi ya mwisho,” alisema.
Akizungumzia uchaguzi mkuu ujao, alisema ana uhakika
muungano wa upinzani ndio silaha kubwa ya kuing’oa CCM madarakani.
“Uchaguzi uliopita Chadema tulishinda lakini
tulichakachukuliwa lakini safari hii kupitia Ukawa tumejipanga kuhakikisha
upinzani tunashinda kwa kiasi kikubwa,” alisema.
Alisema hadi sasa Chadema na ukawa kwa ujumla wake kuna
viongozi wenye sifa ya kushinda urais na wanakubalika nchi nzima
- Mwananchi
No comments:
Post a Comment