Mkutano
wa hadhara wa Chama Cha ACT-Wazalendo uliokuwa ukiongozwa na mwenyekiti
wa taifa Anna Mugwira jana jioni katika Viwanja vya Shycom Mjini
Shinyanga umegubikwa na vituko na zomea zomea za hapa na pale baada ya
viongozi wa Chama hicho kupanda jukwaani kuwahutubia wakazi wa
Shinyanga.
Mwenyekiti wa ACT
Wazalendo Jimbo la Shinyanga mjini Godwin Makomba alifungua mkutano wa
hadhara katika viwanja vya Shycom mjini Shinyanga
Viongozi wa ACT Wazalendo
wakiwasukuma wananchi waliokuwa na hasira,waliokuwa wanamshushia kipigo
kijana(yupo hapo chini) aliyedaiwa kuwa alikuwa anaiba pesa kwenye mfuko
wa suruali ya mmoja wa wananchi walikuwa kwenye mkutano huo
Vurugu hizo zimeanza baada
ya katibu mwenezi wa ACT Wazalendo taifa Sabini Richard kupanda
jukwaani na kuwatangazia wananchi kuwa kiongozi wa taifa wa Chama Hicho
Zitto Kabwe hatahudhuria mkutano kutokana na kuwa na kazi zingine za
kichama.
Kufuatia taarifa hizo
wananchi walianza kupiga kelele na kuondoka kwenye mkutano huo huku
wakilalamika kuwa kwanini chama hicho kiliwatangazia kuwa Zitto
atakuwepo kwenye mkutano huo.
Hata hivyo hali ilikuwa
mbaya zaidi baada ya mwenyekiti wa chama hicho taifa Anna Mugwira
kupanda jukwaani na kuwakaribisha baadhi ya madiwani waliokuwa wa
Chadema katika manispaa ya Shinyanga Nyangaki Shilungushela na Siri
Yasin ambapo wananchi walianza kunyosha vidole vya ishara ya Chadema na
kuimba Yuda Yuda Yuda!!
Wananchi hao walisikika
wakisema kuwa madiwani waliohamia ACT Wazalendo ni wasaliti wa Chadema
na hawajafanya lolote katika kata zao wakati wa uongozi wao.
Akizungumza katika mkutano
huo huku akizomewa na wananchi Aliyekuwa diwani wa viti maalum kata ya
Chamaguha Siri Yasin amesema lengo la ACT wazalendo ni kuwakomboa
wananchi na kwamba watakijenga chama hicho kama walivyofanya kazi ya
Kujenga Chadema na kuifanya ikue katika manispaa ya Shinyanga.
Yasin amesema waliofanya vurugu hizo wameowaonea wivu madiwani hao wa Chadema waliohamia ACT Wazalendo.
Naye aliyekuwa diwani wa
kata ya Kambarage Nyangaki Shilungushela akizungumza katika mkutano huo
amewataka wananchi kuwapuuza wanaobeza ACT Wazalendo na kudai kuwa hata
wakati wanaianzisha CHADEMA walionekana kupuuzwa na baadaye wananchi
kuona chama kinafaa.
Kwa
upande wake mwenyekiti wa ACT Wazalendo Jimbo la Shinyanga mjini Godwin
Makomba amewataka wananchi kuacha kufanya vurugu na kuunga mkono chama
hicho.
Awali wakati mkutano
unaanza kijana mmoja ambaye hakujulikana jina wala makazi yake
anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 20 hadi 25 alinusurika kuuawa na
wananchi waliohudhuria mkutano huo kwa madai kuwa alikuwa anaiba pesa za
mmoja wa wananchi waliohudhuria mkutano huo.
Hata hivyo walinzi wa ACT
Wazalendo wakishirikiana na askari wa jeshi la polisi walifanikiwa
kunusuru maisha ya kijana huyo kisha mkutano kuendelea huku zomea zomea
kwa kila kiongozi aliyepanda jukwaani zikitawala hadi mkutano
ulipomalizika .
Habari kutoka eneo la
tukio zinasema kuwa zomea zome hizo zimefanywa na watu wanaodaiwa kuwa
wafuasi wa CHADEMA,huku ikidaiwa kuwa hata huyo kijana aliyenusurika
kuuawa ni mpango wa watu hao kuharibu mkutano wa ACT Wazalendo.
Kijana aliyenusurika kuuawa baada ya kudaiwa kuiba pesa kwenye mkutano
Wafuasi wa ACT Wazalendo wakimwokoa kijana huyo,yuko chini
Baunsa wa ACT Wazalendo akimwokoa kijana huyo kabla ya askari hawajafika eneo la tukio
Askari polisi akimwokoa kijana huyo
Kijana akiondolewa eneo la tukio na wasamaria wema na askari polisi
Askari polisi wakiwa na kijana aliyenusurika kifo na wananchi wenye hasira
Katibu mwenezi wa ACT
Wazalendo taifa Sabin Richard akizungumza kwenye mkutano huo na baada
ya kusema Zitto Kabwe wananchi wakaanza kupiga kelele(kuzomea) kisha
kuanza kutawanyika
Wananchi wakiondoka kwenye mkutano
Katibu mwenezi wa ACT Wazalendo Sabin Richard akiwahutubia baadhi ya wananchi waliobaki kwenye mkutano
Mwenyekiti
wa ACT Wazalendo Anna Mugwira,akimtambulisha aliyekuwa diwani wa
CHADEMA kata ya Kambarage katika manispaa ya Shinyanga Nyangaki
Shilungushela,aliyeambulia kuzomewa na wananchi
Mwenyekiti wa ACT
Wazalendo Anna Mugwira,akimtambulisha aliyekuwa diwani wa viti maalum
CHADEMA kata ya Chamaguha katika manispaa ya Shinyanga,ambaye pia
alizomewa
Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Anna Mugwira,akiwahutubia wakazi wa Shinyanga katika wakati mgumu kwani zomea zomea zilitawala
Nyangaki Shilungushela
akizungumza katika mkutano huo,huku akieleza kutokereka na zomea zomea
hizo akidai kuwa hata wakati wanaianzisha CHADEMA walipuuzwa sana
Baadhi ya wananchi waliokuwa wanazomea wakiwa wamenyoosha vidole viwili wakiimba YUDA YUDA YUDA!!
Siri Yasin akizungumza katika mkutano huo
Zomea zomea na vidole viwili ikiendelea
Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog Shinyanga
No comments:
Post a Comment