Pages

Tuesday, October 6, 2015

HUZUNI KUBWA::WATU WATANO WA FAMILIA MOJA WAUAWA KWA KUCHINJWA

HATIMAYE watu watano wa familia moja waliouawa kinyama kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana wamezikwa kijijini kwao huku vilio vikitawala eneo la mazishi.
Tukio hilo la kinyama lilijiri Septemba 28, mwaka huu saa 9:00 usiku katika Kitongoji cha Kisesa Kata ya Bugalama Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu wakati familia hiyo ikiwa imelala ndani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Gemin Mushi alisema chanzo cha familia hiyo kuuawa kinyama kwa kuchinjwa shingo ni mgogoro wa ardhi madai ambayo baadhi ya wanakijiji wameyakanusha wakisema si sahihi sana.
Waliouawa katika tukio hilo ni George Charles (30), Siku John (23) mama wa familia na watoto wao, Mchambi George (7) Tuma George (5) na Amos George (miezi 9). Wote walizikwa siku moja katika makaburi ya kijijini hapo.

Uwazi lilifika katika kitongoji hicho na kuzungumza na baadhi ya wanakijiji, majirani, ndugu na wazazi wa marehemu na kubaini kuwa, chanzo kinachozungumwa au kuwemo akilini mwa watu ni wivu wa maendeleo ya familia hiyo.
Baadhi ya wananchi ambao hawakutaka kutajwa majina yao gazetini wakiwemo watu wa karibu na familia hiyo, walisema chanzo ambacho kinaweza kusababisha tukio hilo ni kujituma sana kwa marehemu George hivyo kuwazidi kiuchumi wananchi wengine wa kijijini hapo.

Wananchi hao waliyataja mambo saba ambayo wanaamini yalichangia wabaya wa George kumvamia usiku na kumuua yeye na familia yake.“Kwanza kabisa marehemu alipoanza kuishi eneo lile alilokutwa na mauti alikuwa kawaida. Halafu akaja akajenga nyumba. Pili akafungua duka kubwa hapa kijijini.
“Tatu, marehemu alikuwa na roho nzuri. Anakopesha kila mtu. Lakini nne ni jinsi duka lake lilivyokuwa limejaza bidhaa nyingi

 
 kupita maduka mengine. Duka lake lilikuwa na kila kitu.“Tano, nyumba ya marehemu George ndiyo iliyokuwa na umeme hapa kijijini tena wa sola. Kwake mwanga usiku ulitofautisha nyumba yake na nyingine. Lakini jambo la sita ni jinsi maisha yake na familia yalivyokuwa ya amani. Hilo nalo naamini liliwaumiza wabaya wake.
“Saba, yule bwana mauzo ya duka lake kwa siku yaliwazidi wafanyabiashara wengine wote. Kwa hiyo alikuwa akikata mbuga kuelekea kweye mafanikio zaidi. Naamini wabaya wake walipoyaangalia haya wakaona dawa yake ni kuimaliza hii familia,” alisema mwanakijiji huyo.
Kauli hiyo ilionekana kuungwa mkono na mjomba wa marehemu, Renatus Dutu kwa maelezo kuwa kutokana na maendeleo yake marehemu, inawezekana baadhi ya wanakijiji walikuwa hawayataki.“Nyumba yake ndiyo ilikuwa na umeme tu hapa kijijini. Alikuwa akichaji simu nyingi za wananchi. Duka lake lilikuwa kubwa. Tuna wasiwasi kwamba uwezo wake unaweza kuwa chanzo,” alisema Dutu.
Portini Shili ni jirani wa familia iliyochinjwa ambapo anaeleza kuwa, chanzo hicho cha mgogoro wa ardhi hakikubaliki na wanakijiji bali maendeleo ya familia hiyo kiuchumi ndiyo yanasemwa kuchangia.
“Hilo eneo la ardhi wanaloeleza polisi lilikuwa ni la mpwa wangu (mtoto wa dada yake). Wakati wanauziana eneo hilo mimi nilikuwepo. Aliuziwa na baba wa kambo wa marehemu (George) lakini wakati ananunua eneo hilo tayari familia ya George ilikuwa ikiishi humo mpaka vifo,” alisema.
“Hakuna ukweli juu ya chanzo hiki cha mgogoro wa ardhi na baba wa kambo ambaye anatuhumiwa na amekamatwa ni mzee mwenye heshima hapa kijijini lakini hatuwezi kusema sana, sheria inachunguza. Mimi nilikuwa ndani ya familia hiyo, mapenzi ya mzee huyo kwa mtoto wake (George) yalikuwa makubwa sana kutokana na kuwasaidia,” alisema Shili.
Mbali na jirani huyo, baba mzazi wa mama wa familia, John Lutamba, ndugu wa marehemu (Zengwe Sendama, mjomba (Renatus Dutu) nao walieleza kuwa hawaamini sana kama chanzo cha vifo ni mgogoro wa ardhi kwa vile hakukuwa na mgogoro wowote katika familia hizo.

“Hakuna ukweli wa juu ya chanzo hicho mpaka sasa tupo tunajiuliza nini chanzo na wahusika ni akina nani? Na hakuna mwenye jibu katika familia yetu, hakuna mgogoro wowote wa ardhi na tulikuwa tunaishi vizuri,” alisema Lutamba.
Akizungumza na Uwazi, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Bugalama, Christopher Kulwa alisema tangu amekuwa kiongozi katika eneo hilo hajawahi kusikia au kuletewa ugomvi au mgogoro juu ya familia hiyo.

Alisema kama uongozi wa serikali ya kijiji bado unafuatilia chanzo na wahusika wa tukio hilo ambapo alisema katika hatua za awali za uchunguzi waliamua kila mwana kijiji kupiga kura ya siri.
“Tumeendesha kura ya siri kwa kila mtu ambaye anaweza kuwafahamu wahusika na chanzo. Kura hiyo tayari tumepatiwa baadhi ya majina ya watu ambao walihisiwa kuhusika, tunayafanyia kazi kwa kushirikiana na jeshi la polisi,” alisema mwenyekiti huyo.
Kamanda Mushi alisema kufuatia mauaji hayo jeshi lake linawashikilia watu watatu ambao ni Migata Lusalago (50), Jihelya Migata (30) na Sollo Kengele (31) wote wakazi wa kijiji hicho.

No comments:

Post a Comment