JUMAPILI
ya Oktoba 25, 2015, Tanzania inafanya Uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge pamoja
na kumpata Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Uchaguzi
ni nini? Zipo tafsiri mbalimbali lakini mojawapo na iliyo wazi ni kwamba, hii
ni njia ya kidemokrasia inayotumiwa na watu katika kuchagua viongozi wa
kuwaongoza kwa kipindi fulani kwa mujibu wa Katiba au utaratibu waliojiwekea
wenyewe.
Huu ni Uchaguzi Mkuu wa Tano kufanyika tangu mfumo wa vyama
vingi ulipoanza tena mwaka 1992, lakini ni wa 11 tangu Tanganyika na Zanzibar
zilipoungana mwaka 1964.
Uchaguzi
wa mwaka huu una umuhimu wa kipekee kwa sababu kadha wa kadha, mojawapo ikiwa
umri wa miaka 23 tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanza.
Huu
ni umri mkubwa, na kwa hakika vijana wengi waliojitokeza kujiandikisha
safari hii ni wenye umri wa kati ya miaka 18-35, ikimaanisha kwamba wengi wao
walizaliwa kuanzia mwaka 1992. Hawa wanatengeneza asilimia 57 ya wapigakura wote.
Umuhimu
mwingine ni kwamba, kulinganisha na uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka
1995, safari hii demokrasia imekua na kupanuka kiasi cha kushuhudia wapigakura
22.75 milioni, idadi ambayo ni kubwa zaidi kuwahi kutokea nchini tangu tupate
Uhuru.
Kwa
upande mwingine, hamasa imeongezeka, upinzani umeimarika zaidi na uhuru wa
habari umepanuka ukiwamo ukuaji wa sekta ya habari na mawasiliano, hususan
mitandao ya kijamii.
Haya
yote yanatokea kutokana na kuwapo kwa amani na utulivu, sifa ambazo zimeendelea
kuitambulisha vyema Tanzania hata katika jumuiya za kimataifa.
Uchaguzi
Mkuu ni gharama kubwa kifedha, rasilimali watu na muda, na kama mambo
yatakwenda mrama maana yake nchi itakuwa imeingia hasara kwa kupoteza fedha,
lakini pia itaingia kwenye machafuko ambayo yatatowesha amani iliyodumu kwa
miaka mingi.
Madhara
ya machafuko au vita – kama tulivyoshuhudia kwa majirani zetu Rwanda na Kenya
ni vifo, ulemavu wa kudumu, kutengana na familia, ukimbizi na kuvurugika kwa
uchumi, jamii na siasa kwa ujumla.
Kwa
miaka yote tangu Uhuru, licha ya uchanga na umaskini kama taifa, Watanzania
hatujazoea maisha ya vurugu na machafuko na ndiyo maana tuna wajibu wa
kuhakikisha uchaguzi huu unapita salama.
Wajibu
wa kulinda amani ya nchi yetu ni wa kila Mtanzania bila kujali rangi, dini,
kabila ama nafasi yake katika jamii.
Tunaposema
hivyo tunamaanisha kwamba, vyombo vya dola vinapaswa kutekeleza wajibu wao kwa
mujibu wa sheria na kuhakikisha Watanzania wanapiga kura kwa amani kuchagua
viongozi wao kwa utaratibu waliojiwekea.
Kimsingi,
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ndio wasimamizi wa chaguzi zote, hivyo wana
dhamana kubwa kuhakikisha kila aliyejiandikisha na kujitokeza siku hiyo
anatumia haki yake ya kikatiba kupiga kura bila kubughudhiwa.
Ili
kuondoa utata huo, NEC pia inapaswa kuhakikisha kunakuwa na uwazi kuanzia hatua
ya kupiga kura mpaka wakati wa kutangaza matokeo, ambayo pia yanatakiwa
kutolewa kwa wakati ili kuondoa mashaka miongoni mwa wagombea na wananchi kwa
ujumla.
Wanasiasa,
hususan wagombea ama wapambe wao, wanapaswa kutoa kauli za kuhamasisha amani na
utulivu kwa siku hizi chache zilizosalia kuelekea uchaguzi mkuu, siku ya
uchaguzi na baada ya kutangazwa kwa matokeo.
Wanasiasa
wanaaminika kwa wananchi, kwa hiyo kauli yoyote watakayoitoa ama inaweza
kujenga au kubomoa amani iliyopo, hivyo kuondoa utulivu na kuisambaratisha
Tanzania ya sasa iliyotukuka ulimwenguni kote kama kisiwa cha amani na utulivu.
Vyombo
vya habari navyo vina wajibu mkubwa zaidi kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa
usalama na amani na hata baada ya matokeo kutangazwa viendelee kudumisha amani
hiyo.
Hilo
litawezekana tu iwapo vyombo vya habari vitaandika au kutangaza habari kwa
kufuata sheria za nchi, miiko na maadili ya taaluma na fani ya uandishi wa
habari ikiwa ni pamoja na kutoegemea upande wowote, kuepuka lugha za uchochezi
na ushabiki wa kisiasa, kabla na wakati wa kutangaza matokeo.
Kutokana
na umuhimu huo, sisi wamiliki wa mitandao ya kijamii nchini Tanzania (Bloggers)
tumejadiliana na kukubaliana kwa pamoja kuhusu hatma na mustakabali wa taifa
letu kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa wakati na baada ya uchaguzi huu
wa kidemokrasia na kwa kauli moja tumetoa msimamo wetu kuhusu amani ya nchi
hii.
Kwa
ujumla, hakuna anayeweza kujisifu kuwa ana uhalali zaidi wa taifa hili kuliko
mwingine, taifa hili ni letu sote, hivyo wajibu wa kulinda na kudumisha amani
na usalama wa nchi ni wa kila mmoja.
Tunaomba
Watanzania wote wenye sifa wajitokeze kupiga kura kwa amani na utulivu,
wasubiri matokeo kwa amani na utulivu, wapokee matokeo kwa amani na utulivu,
maisha yaendelee kwa amani na utulivu, tusonge mbele kwa amani na utulivu huku
tukijua kwamba kuna maisha baada ya uchaguzi, na hilo ndilo muhimu zaidi.
MUNGU
IBARIKI TANZANIA!
No comments:
Post a Comment