Mratibu
wa Vijana, Bahati Juma (wa kwanza kulia) akiwa na wanafunzi wa darasa la saba,
shule ya Msingi Uchunga, kupitia pamoja somo la kiswahili kituoni hapo.
Mabadiliko
katika jamii yoyote kwa kiasi kikubwa huchangiwa na ongezeo la mahitaji ya
binadamu katika mambo mbalimbali. Kwamba, kadri dunia inavyopitia mabadiliko,
kadiri ile ile changamoto, mahitaji na huduma katika jamii husika huongezeka. Ili
kufikia malengo yanayotokana na misukumo na mageuzi yasiyokwepeka, binadamu
amelazimika kubuni mikakati mbalimbali ya maendeleo. Si hivyo tu, mabadiliko
haya yamemfungulia binadamu fursa ya uthubutu wa kujaribu mambo mbalimbali,
siyo tu kwa faida yake, bali jamii nzima inayomzunguka.
"Sikutegemea
kama siku moja katika maisha yangu nitapata wazo ambalo lingebadili na kushawishi
watu kuchukua hatua kwa mustakabali wa jamii.”
Hiyo
ni kauli ya mraghbishi Revocatus Richard ambaye pia, kitaaluma ni mwalimu katika
shule ya msingi Uchunga. Richard alitoa kauli hiyo baada ya kupitia mafunzo ya uraghbishi
na mwalimu mwenzake, Restusta Katobesi, ambao
baadaye kwa pamoja, walianzisha Kituo cha KIMAJU (Kituo cha Maendeleo
cha Jamii ya Uchunga) kwa kushirikiana na uongozi wa kijiji na wananchi. Na
hilo ndiyo lilifanya achaguliwe kuwa Mkurugenzi wa kituo hicho.
Hivi ni baadhi ya vitabu na majarida ambayo yapo katika maktaba ya kituo hicho
Walimu
hao walikuwa miongoni mwa waraghbishi 30 walioshiriki mafunzo ya uraghbishi yaliyotolewa
mwezi Machi, mwaka 2012 wilayani Kishapu katika mkoa wa Shinyanga. Kutokana na
faida na maarifa waliyoyapata kwenye mafunzo hayo, walimu hao waliamua kuunda
umoja uliokuwa chachu ya kuanzishwa kituo hicho cha maendeleo.
Mwanazuoni
Sarah Earl, aliwahi kusema: "Maendeleo ni watu na mazingira yao. Kwamba,
kusingekuwa na maana iwapo barabara, hospitali, shule na miradi mingine ya maendeleo inayojengwa kwa ajili ya watu
isingetumika." Mraghbishi ni
mwananchi anayeleta uhai mpya ndani ya jamii kwa kutambua matatizo na
kupendekeza njia sahihi za kuyatatua.
Kulikuwa
na uraghbishi katika kijiji cha Uchunga ambapo baada ya kupatiwa mafunzo ya
uraghbishi, walimu hawa walirudi kijijini kwao wakiwa na jukumu moja la kutambua
changamoto zinazoikabili jamii yao na kupendekeza nini kifanyike wakitumia
nafasi na uwezo walio nao. Kikubwa walichoangalia ni mustakabali wa mtoto wa Kijiji
cha Uchunga, kwa maana ya nafasi ya mtoto, ikiwamo ya kufahamu huduma
anazopata. Katika kufikiria sehemu ya kuanzia na ili kumpa mtoto wa kike nafasi
katika jamii, hasa ya kuongoza, walianza na wanafunzi wa shule wanayofundisha, Uchunga.
Baadhi ya
wananchi na wajumbe wa Kituo cha Maendeleo cha Uchunga wakiwa mbele ya kituo
kabla hakijaezekwa na mabati.
“Nimepata
bahati ya kuwa mwalimu mkuu msaidizi mara kadhaa na nimetumia fursa hiyo kuleta
mabadiliko, nikianzia kubadilisha utaratibu wa kuchagua viongozi wa wanafunzi
katika shule yetu," alisema Richard na kuongeza: "Kwanza
tulibadilisha wazo la Kaka Mkuu na badala yake tukasema tutakuwa na Kiranja
Mkuu, ili kutoa fursa kwa wanafunzi wa kike kushika nafasi za uongozi wa
wanafunzi." Hadi sasa chaguzi mbili za kidemokrasia za kuchagua viongozi
wa wanafunzi zimefanyika shuleni Uchunga Julai 2012 na Mei 2013. Katika kuhakikisha
wanaendeleza mawazo hayo, waraghbishi hao walikuja na wazo la kujenga kituo cha
kujisomea. Walianza kuwatembelea wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kata ya
Uchunga wanaoishi katika kijijini hapo.
Ili
kufikia malengo yao, waliomba ushirikiano, siyo tu kwa walengwa ambao ni
wanafunzi, bali kutoka kada zingine ndani ya jamii.
Haya ndio mazingira ya kituo cha maendeleo ya jamii kilichopo Kijiji cha Unyeyembe kata ya Uchunga wilayani Kishapu mkoani Shinyanga
Akielezea
jinsi walivyoanza, mraghbishi Katobesi alisema: “Tulikutana na wanafunzi na
kuunda umoja wa kikundi wa Wanafunzi wa Sekondari Uchunga (UWASU). Kikundi hiki kiliamsha hamasa kwa wanafunzi
waliokukubali kujitolea kufanya kazi.”Na baadhi ya wanafunzi hao wametembelea
shule nyingine na kuhamasisha wenzao kujitolea kusaidia kazi mbalimbali kama kuchota maji na kuokota mawe kwa ajili ya
ujenzi wa jengo la kituo hicho cha
kujisomea. Ndani ya jamii yoyote kuna
mamlaka, hivyo ili malengo yao yatimie kuliwalazimu waraghbishaji hao kupata
ruhusa kutoka kwa walimu na aliyekuwa mwenyekiti wa kijiji wakati huo, Mahona
Punguja.
“Baada
ya kutoka kwenye mafunzo yao, walikuja kuzungumza na mimi kuhusiana na mambo
waliyojifunza na jinsi watakavyoleta mabadiliko. Nilikubaliana nao na kuweka utaratibu
wa kuwashirikisha wazazi kama wadau muhimu na makundi mengine maalumu,” alisema
Punguja. Makundi maalumu ni pamoja na watumishi wa uma, kwa maana ya walimu na
mtendaji wa kijiji na kata, wazee maarufu, viongozi wa dini, vijana na wajumbe
wa halmashauri ya serikali ya kijiji. Waraghbishi hawa kwa ushirikiano na
uliokuwa uongozi wa serikali ya kijiji waliweza kukutana na makundi hayo ili kuwaelimisha
kuhusu wazo la kituo cha kujisomea. Baada ya kila kundi kukutana na
waraghbishi, uliitishwa mkutano wa pamoja wa kujadili jambo hilo na kamati ikaundwa ya kusimamia mchakato mzima. Kamati
hii ilichaguliwa kwa kila kundi kuwa na mwakilishi wake.
Mmoja wa wanafunzi wa kijiji cha Unyenyembe akiwa anasoma gazeti ili kujua yaliyojili kutoka sehemu mbalimbali Tanzania na Dunia kwa ujumla.
“Njia
ya kwanza ilikuwa ni kukusanya fedha, kisha kuwaomba wananchi kuchangia nguvu zao.
Kila mmoja kwa nafasi yake alijitolea. Wengine tulisomba mawe na kuchimba
msingi. Wanawake walileta vyakula kwa
ajili ya mafundi ambao nao walijitolea pia utaalamu wao bure”, anaelezea
Michael Butu, Mwenyekiti wa Kituo cha KIMAJU. Wanajamii waliohamasika waliombwa
kuchangia kila mmoja Shilingi 10,000 za Kitanzania, ingawa baadhi walitoa nusu
ya mchango huo. Kila kitongoji kiliombwa kuchangia Shilingi 60,000. Michango
hii ilikusanywa baada ya kuundwa kwa nguvu ya pamoja na wenyeviti wa vitongoji.
Kati ya vitongoji vitatu, viwili vilikamilisha ahadi zao.
Harakati
hizi ziliwezesha wanajamii kujenga kituo hadi ngazi ya linta, kabla ya mlezi wa
kituo hicho, Charles Dida kutoa shilingi
355,000 kama mkopo kwa ajili ya kununua
mabati na mbao. “Nilipoona jengo letu linasuasua, niliamua kujitolea
kufanikisha ujenzi. Niliamua kumshirikisha mke wangu, ambaye aliunga mkono
uamuzi wangu kwa kujua mafanikio yatakayopatikana ni ya jamii nzima,” alisema Charles
Dida. Katika hili tumejifunza mahusiano yaliyopo baina ya baba na mama katika
kufanya maamuzi ya pamoja. Ni tofauti na mfumo dume uliozoeleka katika jamiii
ya kisukuma. Na mpaka sasa kituo kimeweza kulipa kiasi cha Shilingi 110,000 na
hivyo bado kinadaiwa Shilingi 245,000.
Baadhi ya wanakijiji wakiwa katika mkutano wa pamoja eneo la kituo cha maendeleo cha Jamii katika kijiji cha Unyenyembe.
Ili
kuhakikisha kituo kinaendelea kutoa huduma kwa watoto wa Uchunga wajumbe wa
kamati tendaji wanafanyakazi kwa kujitolea kwa kuwa wao kuwa sehemu ya jamii ya
wananchi wa kijiji cha Uchunga. “Nilihamasika baada ya kupendezwa na wazo la
kuanzishwa kwa kituo hiki. Na siku nilipoombwa kuwa sehemu ya kuleta mafanikio,
nilikubali mara moja na kushiriki mikutano na ratiba nyingine,” alifafanua
katibu wa vijana, Bahati Juma. Moja ya majukumu aliyokabidhiwa ni huhakikisha
kituo kinafunguliwa saa mbili asubuhi na kufungwa saa 10 jioni. Kwa wastani,
kituo kinahudumia wanafunzi 20 kwa siku. Mbali na katibu huyo, watendaji wengine ni
pamoja na mkurugenzi, katibu, mhasibu, na kamati tendaji chini ya mwenyekiti na
mlezi wa Kituo. Nafasi hizi zote zina wasaidizi isipokuwa ya mkurugenzi na mlezi.
Watendaji
wa Kituo cha Maendeleo cha Jamii ya Uchunga wakiwa katika picha ya pamoja na
wanafunzi mbele ya jengo la kituo hicho likiwa limekamilika kutokana na
michango yao ya fedha na nguvu kazi.
Uongozi
huu ulipatikana kidemokrasia kwa kuchaguliwa kwenye mkutano mkuu wa kijiji.
Baada ya kupata uongozi walitengeneza katiba na kukisajili kituo chao. Kwa
mujibu wa katiba ya kituo hicho, uongozi unachaguliwa kila baada ya miaka
mitatu. “Waasisi wa kituo ndio
waliopendekeza mfumo wa uongozi na baada ya hapo wakauwakilisha kwenye mkutano
mkuu wa kijiji. Kwa hiyo walioweza walishiriki. Na kila mtu aliyeona anafaa
kuwa sehemu ya uongozi wa kituo hicho alipendekeza jina lake ama la mwenzake.
Baada ya majina hayo kupatikana ndipo yalipigiwa kura na kupata viongozi,”
anafafanua mwenyekiti wa kituo, Michael Butu. Tukiachilia suala la uongozi, kuna utaratibu
maalumu wa kuendesha kituo hicho. Kuna vijana wanaohusika na kuhakikissha ofisi
inafunguliwa ili kutoa huduma za kujisoma bure, ikiwa ni mkakati wa kuhamasisha
watu na kukifahamu kituo.
Taasisi
hii ya kijamii kwa kiasi kikubwa imelenga kwenye uzalishaji maarifa kwa kutoa
huduma ya maktaba, ambayo wanafunzi wanaoishi kijiji cha Uchunga hutumia kusoma
na kufanya kazi za nyumbani baada ya masomo shuleni. Katika ziara za
ufuatiliaji na uwezeshaji, wafanyakazi wa shirika mtendaji la TAMASHA katika
mradi huo wa Chukua Hatua, walishauri kituo kupanua wigo wa huduma zake, kama
anavyoelezea Afisa Mradi Winston Churchill.
“Tuliwashauri
kuwalenga pia vijana walio nje ya shule ili kuwawezesha vijana wote kutumia
kituo hicho vizuri kijijini hapo.” Watu wazima pia wanatumia kituo hicho
kujisomea magazeti, ambayo huwa ni ya siku nyingi na hii ndio sababu ya umuhimu
wa kutafuta redio ili watu wasikilize taarifa za habari. Hali hii imehamasisha wanafunzi wa shule za
sekondari na msingi kuja kujisomea, kama anavyoelezea mwanafunzi wa darasa la
saba Leticia Isaka kutoka Shule ya Msingi Uchunga.
“Kituo
kinanisaidia kutambua mambo mbalimbali, kwa mfano kupitia mafunzo ya hapa,
napata malezi bora ya kuniandaa niwe mwalimu au daktari. Lakini si hivyo tu, wakati
wa mapumziko ya saa sita huwa tunakuja kujisomea hapa baada ya kupatiwa mazoezi
na walimu shuleni,” "Mbali na
mafanikio haya, kituo kina changamoto kadhaa ikiwamo ukosefu wa meza, viti na
makabati ya kuhifadhia vitabu," anasema mkurugenzi wa kituo, Richard na
kuongeza: “Haya mabenchi na meza tumeazima kanisani na tukimaliza tunarudisha
sehemu husika. Hatuna vitabu vya mitaala kwa ajili ya wanafunzi wetu, ingawa
eneo la kujisomea lipo vizuri, nishati ya umeme nayo ni shida.”
Kimsingi,
wanajamii wa Uchunga kwa kushirikiana na waraghbishi na uongozi kwa kijiji
wamefanikiwa kufikia malengo. Ni dhahiri kwamba wana safari ndefu, lakini
itoshe kusema kwamba kituo kinaweza kutimiza dhamira yake ya kuzalisha fedha za
kujiendesha chenyewe. Tuendelee kuwaunga mkono katika hizi harakati zao.
No comments:
Post a Comment