Pages

Wednesday, December 23, 2015

UWAJIBIKAJI WA VIONGOZI WA VIJIJI NI DHANA KUU YA KUTATUA KERO ZINAZOWAKABILI WANANCHI WANAO WAONGOZA.



Baadhi ya wenyeviti toka Halmashauri ya wilaya ya Kishapu wakimsikiliza mkufunzi (hayupo pichani) wakati wa mafunzo yao yaliyofanyika wilayani hapo. 

“Unakuja kwenye ofisi yangu na kutoa taarifa za ubadhirifu wa mtendaji wa kijiji. Nakuuliza, je umechukua hatua zipi kama kiongozi wa kijiji kabla kuja kwenye ofisi yangu? Unanijibu hapana, hii si sahihi,”  Hayo ni maneno ya mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Hashim Mgandilwa, aliyoyatoa wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya  wenyeviti wa vijiji, watendaji wa kata na vijiji kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Loliondo.
Alisema hayo kwa lengo la kufafanua dhana ya uwajibikaji kwa viongozi kama njia muhimu ya kutatua kero zinazowakabili wananchi wa maeneo ya vijijini katika wilaya yake. Ni dhahiri kwamba viongozi wa ngazi za vijiji na kata wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za kiutendaji katika maeneo husika.  Kuna nafuu kwa watendaji wa kata na vijiji,  ambao ni waajiriwa wa serikali na hupewa kazi kutokana  na miongozo, lakini siyo kwa wenyeviti wa vijiji na madiwani, wakati mwingine hata wabunge.



Akielezea changamoto hiyo wakati wa mafunzo ya wenyeviti wa vijiji kupitia mradi wa Chukua Hatua yaliyofanyika Septemba mwaka huu na shirika mdau la CABUIPA, mwenyekiti wa kijiji cha Nyakafulu kilichopo wilaya ya Mbogwe, mkoani Geita, Salum Said amesema:  “Baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa kijiji hiki, hakika sikufahamu vya kutosha kuhusu majukumu yangu mapya kama kiongozi. Na hii ni changamoto kubwa kwa wenyeviti wa vijiji karibu vyote vya wilaya yetu.” 


Yeye ni mmoja kati ya wenyeviti 200 wanaopatiwa mafunzo katika mikoa ya Shinyanga, Geita na Simiyu. Wakati wananchi wakiwezeshwa kuwasimamia viongozi wao, viongozi hawakuwa wakiwezeshwa kutimiza majukumu yao kuwasikiliza na kuwahudumia wananchi wao.  Hivyo kuna haja ya kutoa mafunzo kwa viongozi hao ili waweze kutimiza majukumu yao kwa wananchi waliowachagua, ilikuwa lazima. 
Wanakijiji wa Kijiji cha Uchunga wilayani Kishapu wakiendelea na mkutano pamoja na viongozi wa kijiji na wazee Maarufu
Akielezea umuhimu wa kuwawezesha wenyeviti wa vijiji  wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya wenyeviti na watendaji wa kata Julai 2015, mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri  ya Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, Jane Mutagurwa alisema “Kwa muda mrefu wenyeviti mmekuwa mkilalamika kusahaulika kwenye programu zetu za mafunzo, fursa ndio hii imekuja. Tunafahamu kwamba wenyeviti wetu mnakutana na changamoto nyingi za kiutendaji zinazotokana na uwelewa mdogo katika majukumu yenu, hasa kwa wale wanaoingia madarakani kwa mara ya kwanza. Hivyo mtumie mafunzo haya vizuri.” 


Pamoja na umuhimu wa mafunzo hayo kwa viongozi wa ngazi  ya kijiji na kata, bado imekuwa ni changamoto kubwa kwa serikali kuwawezesha wenyeviti kujua majukumu yao. Na hii inatokana bajeti kuwa na vipaumbele vingine ambavyo halmashauri huwa wamejiwekea katika  kutimiza majukumu yao."


Kwa upande wa Ngorongoro, mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya hiyo mkoani Arusha anaeleza:“Tangu tulipofanya uchaguzi mwaka jana hatujawahi kutoa mafunzo kwa wenyeviti. Kwa hiyo tunaunga mkono mafunzo haya yanayotolewa na PALISEP yatasaidia sana kwenye kuwawezesha viongozi hawa na watendaji wetu,”  Kutokana na hali hii, wenyeviti wamekuwa na changamoto za kuelewa mipaka ya majukumu yao, hivyo muda mwingine hujikuta kwenye mzozo na watendaji wa vijiji vyao.  Mwenyekiti anawajibika kwa mwananchi aliyemchagua, wakati mtendaji anawajibika kwa mkurugenzi aliyemwajiri. Kutokana na tofauti hizo, mafunzo ya sasa ya wenyeviti na watendaji yanaendeshwa kwa pamoja kuwafanya waelewe mipaka yao ya kiutendaji, hivyo kuboresha utendaji wao.


Afisa Programu wa CABUIPA, Michael Ikila anafafanua: “Tunawafundisha vitu sita muhimu; taratibu za uendeshaji serikali za mitaa, majukumu na haki za  wenyeviti wa vijiji, uwajibikaji na utawala bora,  mamlaka za vijiji, masuala ya fedha, ikiwamo uandaaji wa  bajeti na mawasiliano mazuri baina ya viongozi wa  vijiji.”  Mada hizi ni kwa mujibu wa mwongozo wa wizara ya Tawala za Mikoa and Serikali za Mitaa (TAMISEMI).  Majukumu mengine ya wenyeviti hawa ni pamoja na  kuhamasisha shughuli za maendeleo, utawala na  kuhakikisha usalama wa watu katika maeneo yao kwa kushirikiana na watendaji wa kata na vijiji.
Viongozi wa Kijiji cha Negezi wakiwa pamoja na wanakijiji kujadili mambo mbalimbali ya eneo lao.
Kwa upande wa Wilaya ya Ngorongoro, hii ni mara ya kwanza kwa wenyeviti kufundishwa majukumu yao. Mwanzoni mafunzo haya yaliwalenga madiwani ambao kimsingi hawakuyapenda kwa sababu ya kutokuwapo kwa posho. Hivyo mafunzo yao yakaamishiwa kwa wenyeviti wa vijiji ambao walipokea mwaliko kwa furaha pasipo kudai posho. “Mafunzo haya yatatusaidia kuboresha mahusiano na utendaji wetu. Mara kadhaa unakuta wenyeviti wanaingilia mipaka yetu ya kazi, hivyo kuathiri uhamasishaji wa shughuli za maendeleo. Na hii hutokea pale mwenyekiti mpya anapotaka kuwaonyesha wapigakura wake kwamba mwenzake aliyepita hakufanya kazi,” anaelezea mmoja wa watendaji wa kijiji aliyehudhuria mafunzo hayo.


Pamoja na changamoto hizo, bado washiriki ambao ni wenyeviti, watendaji wa kata na vijiji wamekiri kwamba mafunzo hayo yatakuwa chachu ya kumaliza tofauti zinazojitokeza baina yao. Lakini si hivyo tu, viongozi wa wilaya wameonyesha kuunga mkono mafunzo hayo kwa kuwa yanasaidia kuhamasisha wananchi kutimiza majukumu yao. Lakini pia viongozi hao walionyesha umuhimu wa kufikia wajumbe wengi zaidi ya halmashauri za serikali ya kijiji. Kwa mfano, wakati akizungumza na wakufunzi kwenye ofisi yake, mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu, alisema: Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu ina jumla ya vijiji 117 vyenye wajumbe 2,925. 

Katika mazingira hayo, mkurugenzi alitoa ombi maalumu la kusaidiwa kuwawezesha wakufunzi 25 wa wilaya watakaotoa mafunzo kwa wajumbe wa halmashauri za vijiji hivyo. Gharama za wakufunzi hawa kuwafikia wajumbe wengine zitakuwa ni za serikali.  Na huu ni ushirikiano unaotakiwa baina ya sekta ya umma na binafsi kwa kuwa ni jukumu letu sote kwa mustakabali wa maendeleo yetu.
 

No comments:

Post a Comment