Pages

Saturday, February 20, 2016

HAWA NDIO WANAFUNZI BORA 10 KWENYE MATOKEO YA KIDATO CHA NNE MWAKA 2016


Dar es Salaam. Baadhi ya wanafunzi walioshika nafasi 10 za juu katika matokeo ya kidato cha nne yaliyotangazwa jana na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), wameelezea ndoto zao, huku wazazi na walimu wakibainisha siri za mafanikio yao, huku shule za binafsi zikishika kumi bora.
Wakizungumza na waandishi wetu jana, wanafunzi hao walisema kumtanguliza Mungu, kusoma kwa bidii na nidhamu ndivyo vilivyowawezesha kupiga hatua hiyo.
Aliyeshika nafasi ya kwanza
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Canossa, Butogwa Shija (17) aliyeshika namba moja kitaifa amesema kilichomsaidia kufaulu vizuri ni kufanya marudio, kumwomba Mungu na kujiwekea lengo la kwenda kusoma Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani.
Alisema alianza kujiandaa kwa safari hiyo ya kwenda Harvard tangu akiwa kidato cha kwanza ambako amekuwa akiongoza hadi alipomaliza.
“Nilipopigiwa simu nilikuwa nasuka hivyo nilipoambiwa nimeongoza, nikaona safari yangu ya Harvard imeanza,” alisema Butogwa.
Alisema alipokuwa kidato cha tatu, alimuomba baba yake amuandalie hati ya kusafiria kwa sababu anajua atafanya vizuri katika mitihani yake.
“Wazazi wangu hawawezi kunipeleka Harvard lakini kwa juhudi zangu nitakwenda. Mimi ubongo wangu ni kama memory card,” alisema.Chanzo Mwanainchi

 
Mama mzazi wa Butogwa, Angela Shija alielezea furaha ya kufaulu kwa binti yake na kusema mara baada ya matokeo hayo yaliyotangazwa akiwa ofisini, alianza kupigiwa simu nyingi jambo lililomlazimu kuacha shughuli zake na kurudi nyumbani.
“Tangu akiwa kidato cha kwanza alishaniambia kuwa atafanya vizuri na sisi tumekuwa tukimsisitiza asome,” alisema.
Angela alisema binti yake huyo amekuwa na tabia ya kujisomea kila wakati akisema kila alipokuwa nyumbani wakati wa likizo, alikuwa akijisomea hata pale alipokuwa kwenye gari katika safari yoyote.
Aliyeshika nafasi ya pili
Aliyeshika nafasi ya pili kitaifa Congcong Wang (16) kutoka Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Feza alisema alijiunga na shule hiyo mwaka 2006 akitokea China na kulazimika kujifunza lugha tatu; Kiswahili, Kiingereza na Kituruki ambazo hutumika katika shule hiyo ili aweze kuwasiliana na wenzake vizuri.
Alisema baada ya kujua lugha hizo, ilikuwa rahisi kwake kuelewana na wenzake na walimu walimsaidia.
“Walinisaidia wakijua baadhi ya vitu sitaelewa. Cha muhimu ni kwamba hakuna njia ya mkato zaidi ya kusoma,” alisema Congconge, ambaye ni raia wa China aliyepata alama B somo la Kiswahili.
Aliyeshika nafasi ya tatu
Mwanafunzi aliyeshika nafasi ya tatu, Innocent Lawrence (20) wa Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Feza alisema kusoma, nidhamu na kumtegemea Mungu ndiko kulikomfikisha hapo.
“Nilikuwa nafuatilia ratiba ya kusoma niliyokuwa napanga. Wanafunzi wengi huwa wanapanga ratiba lakini hawazifuati,” alisema Innocent.
Baba mzazi wa Innocent, Lawrence Nyakabunda alisema walitarajia matokeo hayo kwa kuwa ndiye aliyeongoza pia katika matokeo ya kitaifa ya darasa la saba.
“Matokeo hayo yametufurahisha, nidhamu, kumtegemea Mungu na kuheshimu malengo aliyojiwekea ndiko kumemsaidia,” alisema Nyakabunda.
Aliyeshika nafasi ya tano
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Ilboru, Sang’udi Emmanuel aliyeshika nafasi ya tano kitaifa alisema hakutarajia mafanikio hayo na kusema siri ya ushindi ni kusoma kwa bidii, nidhamu na kumwamini Mungu.
Sang’udi ambaye alishika nafasi ya kwanza kitaifa katika mtihani wa majaribio wa kidato cha nne mwaka jana, alisema anawashukuru walimu, wanafunzi na wazazi wake kwa malezi mazuri.
“Nimefurahi sana, kushika nafasi ya tatu kitaifa na siri ya ushindi ni Mungu, nidhamu na kushirikiana na wenzangu darasani,” alisema.
Alisema malengo yake ni kuwa mhandisi wa ndege baada ya kumaliza masomo yake.
Mwalimu Mkuu wa Sekondari ya Ilboru, Julius Shulla alisema alitegemea kuwa Sang’udi angeshika nafasi za juu, kwani tangu kidato cha kwanza hadi cha nne amekuwa akifanya vizuri na mwenye nidhamu darasani.
“Ni kijana mzuri, ana nidhamu na amekuwa akiongoza katika soko la hesabu, mwaka jana aliongoza kitaifa na darasani amekuwa akishika nafasi za juu sambamba na mwenzake David Joseph aliyeshika nafasi ya nane kitaifa,” alisema.
Mlezi wa mwanafunzi huyo, Veronica Sang’udi alisema amekuwa na nidhamu na amefuata nyendo za dada yake, Getrude Mande ambaye mwaka 2014 alikuwa mmoja wa wasichana waliofanya vizuri.
Aliyeshika nafasi ya tisa
Mwanafunzi aliyeshika nafasi ya tisa kitaifa, Bright Mwang’onda (17) alisema ufaulu huo utamuwezesha kuifikia ndoto yake ya kuwa mhandisi wa ndege.
Bright aliyehitimu katika Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Marian alisema tabia njema, bidii katika masomo na kumuomba Mungu vimekuwa ngao ya ufaulu wake.
“Nakumbuka niliwahi kuwa wa mwisho wakati nikiwa chekechea, cha ajabu wazazi wangu na walimu hawakunichukia badala yake walinitia moyo wakiniambia nikikazane kusoma nitafaulu. Namshukuru Mungu, tangu darasa la tatu hadi leo, maendeleo yangu ya shule yamekuwa mazuri,” alisema.
Mama yake mzazi, Hamida Kejo alisema haikuwa rahisi kupokea matokeo ya mwanaye na kwamba, ufaulu wake umeifurahisha familia yao.
“Nilikuwa kwenye kazi za bustani nilipopigiwa simu na kaka yangu (Rashid Kejo, Mhariri Msanifu Mkuu wa Mwananchi), akinipa hongera ya mtoto kufaulu, baadaye nikaambiwa ameingia 10 bora hakika imekuwa furaha na tunamshukuru Mungu,” alisema.
Aliwashauri wanafunzi wengine kusoma kwa bidii, kuwapenda walimu wao na kuepuka makundi mabaya yanayoweza kuwapotezea ndoto zao.
Imeandikwa na Kalunde Jamal, Tumaini Msowoya na Mussa Juma.

No comments:

Post a Comment