Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Thursday, February 4, 2016

KASI YA RAIS MAGUFULI YAGONGA MWAMBA POLISI MLANDIZI

Kituo cha Polisi cha Mlandizi, wilayani Kibaha, Pwani.

Na Mwandishi Wetu

ASKARI wa Kikosi cha Polisi cha Usalama barabarani, Kituo cha Polisi Mlandizi

wamewasotesha kwa takribani masaa mawili  na nusu wanahabari kupata risiti

ya malipo ya faini aliyotozwa dereva wao baada ya kudaiwa kufanya kosa la

kutaka kulipita gari lingine sehemu isiyoruhusiwa.


Sakata hilo lilianza wakati polisi alipolisimamisha gari hilo katika Kituo cha

Visiga, Mlandizi, wilayani Kibaha, Pwani ambapo alimuomba dereva leseni yake

na kumuamuru ateremke ili ajieleze akiwa nje ya gari na hatimaye kumlipisha



faini ya sh. 30,000 kwa kosa hilo.


Baada ya wanahabari waliokuwa kwenye gari hilo kumsubiri dereva kwa

takribani nusu saa, waliamua kuteremka kumfuata kujua kinachoendelea, kwani

walikuwa wana haraka ya kufika Dodoma muda waliopangiwa  ili waungane na

msafara wa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kwenda Singida kwenye

maadhimisho ya miaka 39 ya kuzaliwa CCM.


Lakini baada ya mmoja wao kuwauliza Trafiki sababu zinazosababisha

kutomwachia dereva, walijibu kwa kashfa na kejeli, wakihoji kwani nyie ni akina

nani? na dereva wenu asipolipa faini basi watakaa hapo kituoni hadi jioni.

Mmoja wa wanahabari hao alilipa faini ya sh. 30,000 na kuomba risiti.

Hapo ndo songombingo ilianza ambapo Trafiki wa kike alijibu kuwa  hawana

risti bali kinachofanyika pale ni kuandikiwa tu taarifa ya kosa lao na kwenda

Kituo cha Polisi cha Mlandizi kilichopo takribani umbali wa Km 5, na wengine

waliokamatwa kwa makosa mbalimbali ya usalama barabarani waliamuliwa

kwenda kupata risiti katika kituo hicho.


Mabishano makubwa yalitokea hapo baina ya Trafiki na wanahabari waliokuwa

wanahoji ni kwa nini kitabu cha risiti wala mashine za kielekroniki havipo hapo

ili kurahisisha kazi. Askari wa kike na mmoja wa kiume walijibu kuwa

wasifundishwe kazi.


"Msitupotezee muda hapa, nendeni Mlandizi, mkapate hiyo risiti,"alisema trafiki

wa kike. Wakati anasema hivyo kumbe mhasibu wao alikuwepo palepale Visiga,

lakini bila kuwaambia ondokeni naye ili akawahudumie."


Pia, mmoja wa Trafiki aliuponda sana utaratibu wa wakosaji kulipia faini kwa

kutumia mashine za elekroniki akidai kwamba ni hasara kwa trafiki na madereva

ni bora mashine hizo ziishie Dar es Salaam zisipelekwe Mkoa wa Pwani.Trafiki

wengine walisikika wakisema kuwa hivi hawa jamaa wanaolazimisha kupewa

risiti ni akina nani, waache waende zao, wakafie mbali.


Maneno hayo yalionekana kuwaudhi wanahabari na kuamua kuondoka kwenda

Kituo cha Polisi Mlandizi, kufuatilia risiti, lakini walichokikuta huko ni maajabu,

hasa ya kuambiwa kuwa Mhasibu hayupo ofisini kwake amekwenda kununua

peni.


Baada ya wanahabari hao kusubiri kwa takribani saa moja, waliamua kwenda

kaunta kuulizia na kuomba kuzungumza na Mkuu wa Kituo ili awasaidie kupata

risiti wawahi kwenda Dodoma, lakini mmoja wa askari aliyekuwa zamu aliwajibu

kuwa Mkuu wa Kituo hajafika ofisini amepitia Kibaha Mjini kwenye mkutano.

Alipoombwa awasaidie kumpata mhasibu, askari huyo alitoka nje hadi ofisi ya

Mhasibu alipomkosa akaamua kumpigia simu na kuwajibu kuwa ametoka mara

moja kwenda kununua peni. Jambo hilo liliwashangaza sana wanahabari na

kuanza kuhoji kwamba iweje kitendo cha kununua peni  kitumie muda wote huo

na kusababisha watu wakiwemo wao kukosa huduma tena asubuhi majira ya

saa 3?


Mmoja wa wananchi aliyekwenda kituoni kupata huduma ya risiti, alisikika

akilalamika kuwa tabia hiyo ya kuchelewesha kutoa huduma ipo sana kituoni

hapo na kwamba wanaoonekana kabisa hawaendani na kasi ya kufanya kazi

anayoitaka Rais Dk  John Magufuli ya 'Hapa Kazi Tu'.


Mle ndani ya Kituo cha Polisi walisikika wakiulizana kwamba hivi haw watu

wanaowasumbua na kutaka kuzungumza na mkuu wa kituo ni akina nani hawa,

eti wanataka risiti, ebu tumpigie simu mhasibu aje atuondolee balaa hapa.

Baada ya muda askari mwenye E 3275 alitoka nje na kuwaambia wanahabari

kuwa mhasibu amepigiwa simu atakuja muda si mrefu mhudumiwe muondoke,

lakini mmoja wa wanahabari hao anayemiliki blogu ya Full Shangwe, John

Bukuku,  alihoji kuwa hivi ni kwanini polisi wa kituo hicho hawaendani na kasi

ya Rais Dk. Magufuli? alijibu kuwa kwani kuna nini?


Baada ya muda Mhasibu aliwasili kwa Bodaboda, na alipofika aliwakebehi
wanahabari kwamba anawashangaa kwa yeye kumuacha kule Visiga
alikokuwa nao na kuwahi kituoni, ndipo wanahabari nao wakashangaa kumuona
tena kituoni hapo wakati wlipofika kituoni waliambiwa ameenda kununua peni.

Dereva alimwambia haya twende ukachukue risiti yako muondoke na
watu wako. Dereva aliingia na kupatiwa risiti kutoka kwenye kitabu kipya
ambacho kwa mujibu wa dereva kilionekana dhahiri kuwa ni kipya.
Lakini kwa masaa yote waliyokaa wanahabari kituoni hapo (takribani masaa
mawili), hawakuwaona madereva wa magari waliokamatwa pamoja na gari lao
na kuandikiwa makosa na faini pale Visiga, hawakufika Kituo cha Polisi
kupatiwa risiti, kitendo ambacho kinaashiria fedha wanazolipishwa madereva
kwa kutenda makosa hazitolewi risiti, hivyo mapato ya serikali kupotelea

mifukoni mwa baadhi ya askari wa kikosi cha usalama barabarani.

Baada ya wanahabari hao kupata risiti majira ya saa 4:15 waliamua kuondoka

kituoni hapo kuanza safari ya kwenda Dodoma kuwahi msafara wa Katibu Mkuu

wa CCM, Komredi Abdulrahman Kinana uliokuwa unawasubiri kwenda Singida.

Mwisho

No comments:

Post a Comment