Mhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro, Iddi Mashaka,
ambaye pia ni afisa intelijensia wa hifadhi hiyo, amekamatwa na jeshi la polisi
kwa tuhuma za kuhusika na tukio la utunguaji wa helkopta namba 88HF na
kusababisha kifo cha rubani wake, Rogers Gower, raia wa Uingereza.
Imeelezwa mashaka amekuwa kinara mkubwa wa ujangili katika
hifadhi mbalimbali zilizopo kanda ya ziwa kwa kutoa ushirikiano kwa majangili
wenzake pamoja na kuwaazimisha silaha za kufanyia ujangili.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, kamanda wa polisi
mkoani Simiyu, Lazaro Mambosasa, amesema mtuhumiwa huyo ni mwajiriwa wa hifadhi
hiyo ya Ngorongoro.
Kamanda Mambosasa amesema jitihada zilizofanywa na jeshi la
polisi mkoani Simiyu, zikiongozwa na mkuu wa upelelezi, Jonathan Shana,
zimeendesha msako maalum uliowashirikisha askari wa vyeo mbalimbali, kikosi
kazi na askari wanyamapori pamoja na wananchi, wamefanikiwa kuwakamata
watuhumiwa wenzake nane walioshiriki katika tukio hilo.
Kamanda amewataja watuhumiwa hao ni Shija Mjika, Njile
Gonga, Masasi Mandago, Mwigulu Kanga, Mapolu Njile, Dotto Huya, Mange Balum na
Dotto Pangali ambao wamedaiwa kuhusika na tukio hilo la kikatili lililokatisha
maisha ya rubani wa helikopta iliyokuwa ikifanya doria eneo la Gululu ndani ya
hifadhi ya Maswa katika kitalu cha mwekezaji Mwiba holding ltd.
Vile vile amemtaja Dotto Pangali ndiye aliyefanikiwa
kutungua ndege hiyo kwa kutumia bunduki aina ya rifle namba 7209460 CAR na
63229, alipohojiwa alikiri bunduki hiyo ni mali ya Mange Magima.
Hata hivyo, kamanda Mambosasa amesema katika tukio hilo,
Shija, Njile na Masasi Mandago waliweza kuonyesha ushirikiano wa karibu kwa
kuwaonyesha meno mawili ya tembo yenye uzito wa kilo 31 waliyokuwa wameyaficha
chini ya daraja kijiji cha Itaba.
Ameongeza mbali na tukio hilo la kukamatwa watuhumiwa hao,
meno mawili ya tembo, jeshi la polisi waliweza kukamata bunduki 29 na risasi
141 ambazo wamiliki wake wamekamatwa kwa ajili ya mahojiano kutokana na kukiuka
masharti ya umiliki wa silaha hizo.
No comments:
Post a Comment