Pages

Monday, February 22, 2016

MUNGY AWATAKA WATANZANIA KUZINGATIA MASHARTI NA KANUNI ZA MITANDAO (AUDIO + VIDEO)

Mungy
Mkuu wa Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Innocent Mungy.
Ili kuhakikisha kunapungua kwa makosa ya uvunjifu wa sheria ya mtandao, Mkuu wa Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA), Innocent Mungy amewataka watumiaji wa mitandao kuzingatia kanuni na masharti ya mitandao.
Mungy aliyasema hayo katika mahojiano maalumu na Mo Blog na kueleza kuwa moja ya sababu zinazopelekea watumiaji wa mitandao kufanya makosa ni kutokusoma masharti na kanuni za mitandao wanaoingia wakati wanapojisajili.
 
“Wengine hawaelewi maana ya mitandao ya kijamii lakini kabla ya kuingia wanatakiwa kusoma masharti na vigezo wakati wanajisajili kuingiza kwenye mitandao hiyo,” alisema Mungy.
Alisema makosa ya mitandao yalianza kujitokeza zaidi mwaka 2012 katika mitandao ya Facebook na Instagram na yaliongezeka zaidi baada ya kukua kwa mtandao wa Whatsapp na kuwataja waathirika wakubwa kuwa vijana na zaidi wa kike kati ya miaka 18 hadi 24.
Mungy alieleza kuwa ili kupambana na makosa ya mtandao Watanzania wanatakiwa kubadilika na kutumia mitandao vizuri na kabla hawajaweka picha au kuandika maneno wahakikishe wanachokiweka mtandaoni hakina makosa.
Aliongeza kuwa sheria zipo na watumiaji ambao wamekuwa wakivunja sheria wamekuwa wakifungwa, wengine wakitozwa faini na wengine bado wanafatiliwa na Jeshi la Polisi ili kuwatia hatiani kwa makosa ya kuvunja sheria ya makosa ya mtandaoni.
“Watanzania wanatakiwa kufuata sheria kabla ya kuweka picha mtandaoni wanatakiwa kufikiria kwanza je kama nikiweka itakuwaje maana mtandaoni kila mtu anaona na hiyo taarifa itadumu milele,” alisema Mungy.
Pia alizungumzia tukio lililotokea mtandaoni linalomhusu Miss Tanzania 1999, Hoyce Temu la kuandikwa vibaya na Mungy kueleza kuwa walipokea taarifa za Hoyce na tayari wameshalikabidhi kwa Jeshi la Polisi na hatua zaidi zinaendelea kuchukuliwa na Polisi ili kuishughulikia kesi hiyo.
Mungy alimaliza kwa kuwataka Watanzania kutumia mawasiliano kama njia ya kuleta maendeleo na sio kuvunja sheria ambayo serikali imeitunga kwa ajili ya kudhibiti makosa ya mtandaoni lakini pia kuutaja mtandao wa Mo Blog kama moja ya mtandao ambao umekuwa mstari wa mbele kukemea matumizi mabaya ya mtandao.

No comments:

Post a Comment