Pages

Monday, February 15, 2016

Ndege ya Air Tanzania Yanusurika Kuwaka Moto Katika Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere

Msemo wa waswahili kwamba ng’ombe wa maskini hazai unaonekana kuwa kweli kwa Shirika la Ndege Nchini (ATCL), ambalo ndege yake pekee imenusurika kuwaka moto katika uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam juzi.

Kwa mujibu wa mashuhuda waliokuwa wakisafiri kwenda mataifa mbalimbali ambao walizungumza na Nipashe juzi jioni, ndege hiyo ilionekana ikitoa moshi mwingi hali iliyosababisha magari ya zimamoto kufika eno hilo ili kuzima moto.

Msafiri mmoja ambaye alikuwa akipanda ndege kuelekea Nairobi, Kenya aliliambia gazeti hili kuwa waliona ndege hiyo ya ATCL ikitoa moshi mwingi hali iliyoashiria kuwa kulikuwa na hitilafu kwenye injini yake.



“Tuko hapa na tunaiona ndege inatoa moshi kweli kweli, watafuteni wahusika wawaambie tatizo nini,” alisema abiria huyo ambaye baadaye alituma picha mbalimbali za mnato na video kwa njia ya simu zikionyesha ndege hiyo ikitoa moshi mwingi.

Gazeti hili liliwasiliana na Katibu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini, Ramadhani Maleta, ambaye alisema hawezi kulizungumzia suala hilo na alielekeza watafutwe wahusika wakuu ambao ni ATCL.

“Mimi siyajui hayo na wala siwezi kuwasemea wakati wenyewe wapo, watafuteni ATCL wao ndiyo wanauwezo wa kulizungumzia kwa kina suala hili, mimi kwanza siko kazini muda mrefu,” alisema Maleta.

Alipoulizwa kuhusu hitilafu ya ndege h iyo, Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga, TCAA, Bestina Magutu, aliliambia gazeti hili kuwa ni vyema suala hilo wakaulizwa wahusika ambao ni ATCL kwa kuwa yeye si msamaji wa shirika hilo.

Jitihada za kumpata msemaji wa ATCL hazikuzaa matunda jana.

Akizungumza wakati wa siku ya sheria nchini, Rais John Magufuli alielezea kushangazwa kwake na kudumaa kwa ATCL hata kushindwa kumudu kuwa na ndege zake kama yalivyo mashirika mengine ya ndege Afrika na duniani.

Rais Magufuli alisema ana uwezo wa kununua hadi ndege sita mpya za kuliendesha shirika hilo lakini lazima wapatikane watumishi ambao watakuwa na uwezo wa kuliendesha na ikiwezekana "kuwafuta wafanyakazi wote walioko sasa."

Source:Nipashe

No comments:

Post a Comment