Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli amefanya uteuzi wa mabalozi watatu katika Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda
na Kimataifa.
Rais Magufuli pia amefanya uteuzi wa makamishna wanne wa
Jeshi la Polisi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa
(NIDA).
Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue,
imewataja mabalozi walioteuliwa kuwa ni Dkt. Asha-Rose Mtengeti Migiro,
Mheshimiwa Mathias Meinrad Chikawe na Dkt. Ramadhan Dau.
Vituo vya uwakilishi
kwa mabalozi hawa vitajulikana baada ya taratibu husika za kidiplomasia
kukamilika.
Kwa upande wa Makamishna wa Polisi, Balozi Sefue amewataja
walioteuliwa kuwa ni:
1. Naibu Kamishna
wa Polisi Simon Nyakoro Sirro ambaye amepandishwa cheo kuwa Kamishna wa Polisi,
na ameteuliwa kuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam. Kamishna
Sirro anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Kamishna Mstaafu Suleiman Kova.
2. Naibu Kamishna
wa Polisi Albert Nyamuhanga ambaye amepandishwa cheo kuwa Kamishna wa Polisi na
ameteuliwa kuongoza Idara ya Fedha, Utawala na Lojistiki. Kamishna Nyamuhanga
anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Kamishna wa Polisi Clodwing Mathew Mtweve aliyeteuliwa
kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza.
3. Naibu Kamishna
wa Polisi Robert Boaz Mikomangwa ambaye amepandishwa cheo kuwa Kamishna wa
Polisi na ameteuliwa kuongoza Idara ya Intelijensia. Kamishna Mikomangwa
anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Kamishna Valentino Mlowola aliyeteuliwa kuwa
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
4. Kamishna
Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Nsato Marijani Mssanzya ambaye amepandishwa cheo
kuwa Kamishna wa Polisi na ameteuliwa kuongoza Idara ya Mafunzo na Operesheni.
Kamishna Mssanzya anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Kamishna wa Polisi Paul
Moses Chagonja aliyeteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi.
Aidha, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli amemteua Dkt. Modestus Francis Kipilimba kuwa Kaimu Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA). Kabla ya Uteuzi huu Dkt.
Kipilimba alikuwa Mkurugenzi wa Menejimenti ya Udhibiti (Director of Risk
Management) katika Benki Kuu ya Tanzania. Dkt. Kipilimba anajaza nafasi
iliyoachwa wazi na Bw. Dikson Maimu ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.
Teuzi zote zinaanzia leo tarehe 15 Februari, 2016
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
15 Februari, 2016
No comments:
Post a Comment