JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA
RAIS IKULU
RAIS wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mama
Mwantumu Mahiza, kufuatia vifo vya watu 11 waliopoteza maisha katika ajali ya
barabarani iliyosababishwa na Basi la Kampuni ya Simbamtoto kugongana uso kwa
uso na Lori lililobeba mchanga katika eneo la Pandamlima, Wilaya ya Muheza Mkoa
wa Tanga.
Ajali hiyo
imetokeo leo tarehe 11 Februari, 2016 majira ya saa 1:15 asubuhi katika eneo
hilo lenye mteremko, ambapo basi la Kampuni ya Simbamtoto lilikuwa likisafiri
kutoka Tanga kwenda Dar es Salaam na Lori lililokuwa limebeba mchanga, lilikuwa
likielekea kiwanda cha Saruji cha Tanga.
Rais Magufuli
amewapa pole Ndugu, Jamaa na Marafiki wote waliofikwa na msiba huo na amewataka
kuwa wavumilivu na wastahimilivu katika kipindi hiki kigumu.
"Nimepokea
taarifa ya vifo hivi kwa mshituko mkubwa, na kupitia kwako Mkuu wa Mkoa wa
Tanga, napenda kuwapa pole nyingi wote waliofikwa na msiba huu mkubwa na
naungana nanyi katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo"
alisema Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli
amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi, na amewapa pole
majeruhi wote 21 walioumia katika ajali hii.
Aidha, Rais
Magufuli amewakumbusha watumiaji wote wa barabara hususani madereva wa vyombo
vya moto, kuwa makini watumiapo barabara kwa kuzingatia sheria zote
zinazosimamia usalama barabarani ili kuepusha ajali.
Gerson
Msigwa
Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es
salaam.
11
Februari, 2016.
No comments:
Post a Comment