Pages

Sunday, February 21, 2016

UNUNUZI WA GARI LA HALMASHAURI YA NACHINGWEA UTATA MTUPU

Na.Ahmad Mmow, Lindi-Nachingwea.
Ununuzi wa gari lenye namba usajili DFPA 1695, Landcruiser mali ya Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, mwanzo mwanzo mwa wiki iliyopita ilizua mvutano baina ya madiwani na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Mhandisi, Jackson Masaka.
Landcruiser
Wakizungumza kwenye mkutano wa pili cha baraza la madiwani kwa mwaka wa fedha 2015/2016 Madiwani hao walisema walikuwa na mashaka katika ununuzi wa gari hiyo, kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya fedha zilizotumika kununulia gari hiyo na bila kuwashirikisha.


Diwani wa kata ya Mkutokuyana, Sada Makota, alisema mchakato wa ununuzi wa gari hiyo umegubikwa na utata, kwa madai kuwa fedha ambazo awali zilitengwa kwa ununuzi wa gari hiyo ni shilingi 84 milioni, wakati zilizoidhinishwa kwenye bajeti ni shilingi milioni 120.00 tu, hata hivyo ilionekana ilinunuliwa kwa shilingi 124.76 milioni.

Alisema licha ya ongezeko hilo, lakini pia taarifa haikuonesha fedha za nyongeza zilitoka wapi na kwaidhini ya nani.

Diwani wa kata ya Lionja, Joachim Mnungu, alisema mkurugenzi alikuwa na kila sababu ya kuwajulisha madiwani kila hatua iliyohusu mchakato wa ununuzi, ikiwamo mabadiliko ya mara kwa mara ya bei.

Alisema fedha zilizokatengwa kwa ajili ya ununuzi ni shilingi 84 milioni. Hata hivyo kabla ya gari hiyo kuletwa, bei ilipanda na kufikia shilingi 96 milioni.

Kama hiyo haitoshi, baada ya kuletwa waliambiwa imenunuliwa kwa shilingi 124.76 milioni.
"Gari imekuja na namba za usajili za gari za misaada (DFPA) tena mtumba, wakala wa manunuzi gani anaweza kuleta gari yenye namba za usajili wa magari ya misaada," alisema na kuhoji Mnungu.

Mkurugenzi mtendaji, Mhandisi Masaka akijibu hoja za madiwani hao, alisema ingawa yeye alikuwa hajahamia katika Halmashauri hii, wakati mambo hayo yanafanyika.

Lakini taarifa zinaonesha mchakato ulikwenda sawa bila kukiuka taratibu, kanuni na sheria. Kwani ununuzi ulifanywa na wakala wa manunuzi wa serikali(GPSA) na kwamba shilingi 4 milioni ziliongezeka kutokana na gharama ya kusafirisha gari hiyo ambayo gharama yake halisi ni shilingi 115milioni.
"Hizo shilingi 95.4 milioni zilirejeshwa na GPSA baada yakuonekana hazitoshi kununua gari iliyokuwa inatakiwa, ilibidi ziongezwe fedha" gharama ya gari ni shilingi 115, kusafirisha ni dola 4,354 sawa na shilingi 9milioni," alifafanunua Mhandisi Masaka.

Alisema kiasi kilichongezeka kilitoka kwenye akaunti ya utawala. Nakwamba kiasi kilichoongezeka(shilingi 4milioni) kiliweza kutolewa bila kupata idhini ya madiwani kwani sheria inampa mkurugenzi uwezo huo.

Akibainisha kuwa gari hiyo siyo ya msaada bali walilazimika kuchukua kabla ya taratibu kukamilika baada ya kupewa maelezo na GPSA kuwa wanaweza kusubiri hadi taratibu za usajili zikamilike au waipokee na wakati wowote wakachukue namba za usajili.
"GPSA walitoa maelekezo kama tunaweza kusubiri au tupokee gari hiyo, ili baadae ikakachukuliwe baada ya taratibu zote kukamilika ikiwa ni pamoja na namba za usajili," alibainisha Masaka.

Hatahivyo majibu hayo hayakuwaridhisha. Diwani wa kata ya Ugawaji, ambaye pia ni mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Ahmad Makoroganya, alisema hakubaliani na majibu hayo kwani hadi baraza la madiwani la Halmashauri hiyo linavunjwa mwaka jana, mchakato wote kuhusu ununuzi wa gari hiyo ulikuwa umekamilika, ulibaki ufuatiliaji tu.

Hivyo maelezo yaliyotolewa na mkurugenzi ilibidi waelezwe kipindi cha mchakato wa ununuzi.

Madai ya madiwani hao yaliungwa mkono na mkuu wa wilaya hii ya Nachingwea, Pololeti Mgema, ambae alisema wataalamu walishindwa kuonesha thamani ya dola kwa shilingi ya Tanzania kwenye mabadiliko hayo ya bei ambayo yalikuwa yanafanyika.

Aliwashauri madiwani hao waendelee kuhoji ili wapate maelezo yanayojitosheleza kwenye mkutano au waunde kamati ya uchunguzi, ambayo pamoja namambo mengine ichunguze uhalali wa gari hiyo kubandikwa namba za usajili wa magari yanayotolewa kwa msaada na wahisani.

Mvutano ulikwisha baada ya madiwani hao kukubaliana kujadili suala hilo kwenye kikao cha kamati ya madiwani, baada ya baraza hilo kujigeuza nakuwa kamati.MWISHO.

No comments:

Post a Comment