Gazeti la Dira ya Mtanzania, Toleo Na.404 la Februari, 29 –
Machi 6, 2016 liliandika taarifa yenye kichwa cha habari kisemacho “Uchafu wa
Ombeni Sefue Ikulu”. Taarifa hiyo, ambayo ni muendelezo wa makala nyingine
kwenye toleo la gazeti hilo la wiki iliyopita, ilimtuhumu Katibu Mkuu Kiongozi
kushawishi juu ya uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa MSD pamoja na Kampuni za “CRJE”
na “UGG” kupewa tenda ya kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma, Daraja la Kigamboni na
Reli ya Dar es Salaam – Kigali. Taarifa zote hizi ni za uongo na za kupotosha
wananchi.
Kuhusu uteuzi wa nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa MSD,
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, hakuhusika kwa
namna yoyote kushawishi uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa MSD. Uteuzi huo
ulitekelezwa kwa kufuata kanuni na
taratibu zilizowekwa. Nafasi hiyo
ilitangazwa na Bodi tarehe 20 Novemba, 2013. Usaili ulifanywa na kampuni huru
iliyopewa jukumu hilo na Bodi. Mapendekezo ya majina matatu yalipelekwa kwa
Mhe. Rais na Waziri wa Afya, kwa ajili ya uteuzi. Balozi Sefue alikuwa hamjui
aliyeteuliwa na wala hakuwahi kuwa na uhusiano naye. Alichofanya Balozi Sefue
ni kutangaza tu uteuzi baada ya Rais kuteua. Gazeti hilo pia limeandika uwongo
kuwa MSD haijawahi kuongozwa na Mkurugenzi Mkuu asiye Mfamasia. Tangu MSD
ianzishwe mwaka 1993 hadi sasa, ni Mkurugenzi Mkuu mmoja tu, Rino Meyers
(1996-1999), ndiye alikuwa Mfamasia. Wakurugenzi wengine kama Peter Mellon
(1993-1995), Jay Drosin (2001-2004) na Joseph Mgaya (2004-2013) hawakuwa
Wafamasia.
Kuhusu Kampuni ya CRJE kuhusishwa na Balozi Ombeni Y. Sefue
Suala la kumhusisha Katibu Mkuu Kiongozi na kampuni hii nalo
ni uzushi na uongo wa kupindukia. Wakati kampuni hii ikipewa tenda ya kujenga
Chuo Kikuu cha Dodoma mwezi Oktoba 2007, Balozi Ombeni Y. Sefue hakuwa Katibu
Mkuu Kiongozi; alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani.
Kadhalika mchakato wa kumpata mkandarasi wa daraja la
Kigamboni, ulipoanza mwezi Machi, 2011, Balozi Sefue hakuwa Katibu Mkuu
Kiongozi; alikuwa Balozi wa Tanzania, Umoja wa Mataifa, New York. Hata mkataba
wa ujenzi wa Daraja hilo uliposainiwa tarehe 9 Januari, 2012,
Balozi Sefue alikuwa na wiki moja tu ya kuwa Katibu Mkuu
Kiongozi kufuatia kuteuliwa tarehe 30 Disemba, 2011. Aidha, Kampuni iliyoshinda
tenda hiyo wala siyo CRJE kama ilivyoandikwa na gazeti hilo bali ni China Major
Bridges Engineering Company (BCEC) kwa kushirikiana na Kampuni ya China Railway
Construction (CRCEG).
Kuhusu tuhuma kuwa Katibu Mkuu Kiongozi Chapuo Kampuni ya
UGG:
Katibu Mkuu Kiongozi hajawahi kuipigia chapuo kampuni yoyote
ile pahala popote. Isitoshe, hakuna kampuni yenye jina la “UGG” iliyowahi
kuonesha nia ya kujenga reli ya kati. Hii ni moja ya uthibitisho kwamba gazeti
hili linatoa taarifa za kuokoteza zisizo na ukweli kama vile walivyopotosha
kuhusu jina la Katibu Mkuu Kiongozi kwenye makala yao ya pili kwenye ukurasa wa
tisa wa gazeti hilo yenye kichwa cha habari “Magufuli anaishi na jipu Ikulu” ambapo
walimpachika Katibu Mkuu Kiongozi jina la Sifuni, jina ambalo hajawahi kuwa
nalo. Balozi Sefue hajahusika, hahusiki na wala hatahusika katika kuchagua wa
kupewa tenda hiyo kwa sababu yeye si sehemu ya wenye mamlaka ya kutoa tenda.
Kuhusu Eliachim Maswi:
Gazeti la Dira ya Mtanzania limeandika kuwa moja ya “madudu”
aliyofanya Balozi Sefue ni walichoita kumsafisha Bwana Eliachim Maswi. Wanadai
hivyo wakati wamekiri kuwa alichofanya Balozi Sefue ni kusoma matokeo ya
uchunguzi, ambao hakuufanya yeye. Waliomsafisha Maswi ni Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Serikali; Sekretarieti ya Maadili ya Umma; na hatimaye kamati ya
uchunguzi iliyoongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu. Kwa hiyo, kwa maoni ya gazeti
hili, Balozi Sefue asingepaswa kusoma matokeo ya uchunguzi uliofanywa na vyombo
hivyo huru. Kwa maoni yao kusoma taarifa ya uchunguzi ni “madudu”.
Habari hizo hazina chembe yoyote ya ukweli, na wao wenyewe
ndani ya gazeti wamekiri hawana ushahidi, ni wazi kuwa habari hizo ni za kubuni
na zimetungwa.
Kwa sababu hiyo, Serikali inalitaka Gazeti la Dira ya
Mtanzania kukanusha uongo na uzushi wao na kumuomba radhi Balozi Ombeni Sefue,
kuiomba radhi Serikali na kuwaomba radhi wote walioumizwa na uzushi huo kwa
uzito ule ule uliotumika kuchapisha taarifa hiyo.
Vinginevyo iwapo gazeti la Dira ya Mtanzania lina ushahidi
wa huo “uchafu” wa Katibu Mkuu Kiongozi, waupeleke mara moja kwenye vyombo
vinavyohusika ikiwamo Sekretarieti ya Maadili na TAKUKURU. Vinginevyo, hatua
zikichukuliwa dhidi yao wasiseme Serikali inavibana vyombo vya habari.
Aidha Serikali inashauri wenye vyombo vya habari,
wachapishaji, wahariri na waandishi wa habari wajikite kwenye weledi na ukweli,
wafanye utafiti na kuandika mambo waliyo na uhakika nayo, na kamwe wasikubali
kutumiwa kuendeleza agenda za watu wengine.
No comments:
Post a Comment