Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Raisi Muungano na
Mazingira Mh. Luhaga Mpina (MB) amekifungia kiwanda cha kuzalisha cement na
chokaa kilichopo jijini Tanga cha Rhino
Cement, leo jioni kutokana na kile
kinachodaiwa kuwa ni uharibifu na uchafuzi wa mazingira na kuvunja sheria ya
usimamizi wa mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake.
Mh. Mpina amechukua uamuzi huo, baada ya kupokea malalamiko
kutoka kwa wananchi wa kata ya maweni kupitia diwani wa kata hiyo Bw. Joseph
Colvas na kujionea mwenyewe namna ambavyo kiwanda hicho kinavyo achilia moshi
mzito kwenda angani, pamoja na vumbi lisilovumilika kusambaa katika maeneo ya
makazi ya wanachi wa kata hiyo ikiwa ni pamoja na kusambaa katika maeneo ya
shule ya sekondari ya Don Bosco ambapo, Mh. Mpina ameelezwa kuwa athari
zitokanazo na uachiachi wa hewa hiyo chafu angani si tu kwa watoto wa shule
zinazozunguka kata hiyo bali pia ni kwa viumbe hai na mazingira.
“Hawa jamaa wamekuwa wakiachilia vumbi jingi na moshi mzito
kutoka katika kiwanda hiki mara kwa mara, hivi tangu jana wamezima mitambo yao
wakijua kabisa kuwa kuna ugeni wa Naibu Waziri kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais,
Alisisitiza Bw. Joseph.”
Kwa upande wake Afisa Afya wa jiji la tanga aliyejulikana kwa
jina moja la bwana Kizito alimuelezea Naibu Waziri Mpina kuwa ni kweli kiwanda
hicho kimekuwa kikifanya uchafuzi huo wa mazingira, na Afisa uendeshaji kutoka
Baraza la Taifa na HIfadhi ya Mazingira NEMC Bw. Novatus Mushi ameeleza kuwa
kiwanda hicho kimeshawahi kutozwa faini ya shilingi milioni kumi na saba (17)
kwa kosa la kuchelewa kulipa ada ya mwaka ya mazingira pamoja na uharibifu wa
mazingira uliokuwa ukifanywa na kiwanda hicho kwa upande wa kuzalisha chokaa.
Mh. Mpina ameelekeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi
wa Mazingira ( NEMC) kukifunga kiwanda hicho kisiendelee na uzalishaji kwa muda
usiopungua miezi mitatu, na kulitaka baraza hilo lijiridhishe na kufuatilia
namna kiwanda hicho kinavyotakiwa kutekeleza sheria ya mazingira kwa kujenga
mfumo wa kisasa wa kutoa taka zitokanazo na uzalishaji kiwandani hapo pamoja,
na kupima vumbi na moshi utokao kiwandani hapo kama hautakuwa na madhara na
athari kwa mazingira na viumbe hai. Kinyume na hapo kiwanda hicho kitafungiwa
moja kwa moja.
Aidha, akitolea mfano wa kiwanda cha bonite bottles cha mjini
moshi kwa kuwa kinara katika upandaji miti na utunzaji wa mazingira, mh Mpina
alivitaka viwanda vingine viige mfano wa kiwanda hicho cha coke cola.
Ziara ya Mh. Mpina Jijini Tanga ilihusisha pia kuangalia
namna ukuta wa fukwe ya Pangani uliojengwa enzi za mkoloni, ulivyo athirika na
madhara yatokanayo na athari za mabadiliko ya tabia nchi na kusema kuwa, ukuta
huo huko kwenye mchakato wa kujengwa na kuboreshwa upya, ifikapo mwezi wa nne mwaka huu mradi wa ujenzi wa ukuta huo
utaanza kutekelezeka kwa kuwa tenda imeshatangazwa na jumla ya kiasi cha fedha
za kimarekani dola milioni 1,400 zimepatikana kupitia mfuko wa nchi maskini
zaidi duniani (LDCf).
Mh. Mpina aliwaasa wakazi wa mji wa Tanga na viunga vyake
kutunza mazingira kwa kupanda miti na kufanya usafi kama ilivyoagizwa na
serikali, ili kuhepukana na nchi kuwa janga na magonjwa yatokanayo na uchafu.
Waziri Mpina Pia alitembelea kiwanda cha maziwa cha Tanga Fresh
na kiwanda cha Tanga Cement na kuridhirishwa na namna ambayo wanatekeleza
sheria ya mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake.
Chanzo Issa Michuzi Blog
No comments:
Post a Comment