Waziri
wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Mhe. Sophia M. Simba
amemkabidhi tuzo ya umahiri katika uongozi Mhe Balozi Getrude Mongella
kutokana na juhudi zake katika kuwakomboa wanawake wa Bara la Afrika.
Hafla
ya kukabidhi Tuzo hiyo ya miaka 50 ya Pan African Women’s Organization
(PAWO) ilimefanyika leo (23/12/2013) Courtyard Hotel jijini Dar es
salaam na kuhudhuriwa na Viongozi wa Wizara waliongozwa na Katibu Mkuu
Bibi Anna T. Maembe na kushirikisha wajukuu wa Balozi Mongela.
Mhe. Sophia Simba alifafanua kuwa lengo la hafla hiyo ni kutambua
utumishi wake na kumkabidhi Mheshimiwa Mongella Tuzo ya heshima ya
Wanawake Mashuhuri Barani Afrika ambao walionesha uongozi uliotukuka
katika kutetea umoja, haki na usawa wa wanawake. Awali tuzo hiyo
ilitolewa katika Mkutano maalumu wa Mawaziri wa Wanawake na Jinsia
uliofanyika Pretoria, Afrika Kusini mwezi Agosti 2-13, 2013. Aidha,
Wizara imetambua umuhimu wa kujulisha taifa kuhusu mchango wa Balozi
Mongella na kutokana na uzoefu wake uliosaidia ukombozi wa wanawake wa
Barani Afrika.
Itakumbukwa
kuwa Mhe. Mongella alikuwa Mwenyekiti wa Mkutano wa Wanawake
uliofanyika Beijing Nchini China mwaka 1995. Matokeo ya Mkutano huo ni
maandalizi ya Azimio na Ulingo wa Beijing, ambao uliainisha maeneo 12 ya
kimkakati ambayo utekelezaji wake umesaidia kuleta usawa wa kijinsia na
wanawake kupatiwa haki zao. Nchi ya Tanzania kama mwanachama wa Umoja
wa Mataifa inatekeleza maeneo hayo muhimu ikiwa ni pamoja na elimu na
mafunzo, afya, ajira, uwezeshaji kiuchumi, usawa, kushiriki uongozi na
maamuzi na kuzuia ukatili wa kijinsia nk.
Akiwa
Rais wa Bunge la Afrika Mhe. Mongella alitumia nafasi hiyo kuelimisha
na kutetea maslahi ya wanawake Barani Afrika. Aidha, amekuwa akishiriki
kikamilifu katika mikutano mbalimbali inayohusu maendeleo ya Wanawake na
jinsia katika ngazi ya kikanda. Katika ngazi ya kitaifa Mheshimiwa
Mongela ametumikia nyadhifa mbalimbali kama vile Waziri, Mbunge, na
amekuwa mstari wa mbele katika kutetea maslahi ya wanawake hapa nchini.
Simba
alisisitiza kuwa Mheshimiwa Mongella amesimama kidete kutetea maslahi
ya wanawake, jambo ambalo linamfanya kuwa mfano wa kuingwa na wanawake
wote wa kitanzania maana ametenda kwa uthabiti na leo tunajivunia
uzoefu wake.
Akitoa
shukurani zake Mheshimiwa Balozi Mongella alikumbusha kuwa chanzo cha
kuanzishwa kwa Pan African Women’s Organization ni Tanzania (PAWO). Na
kwamba ilianza mapema hata kabla ya kuanzishwa kwa vuguvugu la Umoja wa
Nchi za Afrika (OAU). Changamoto kubwa ni kwamba kutothamini ubunifu
wetu wenyewe kumesababisha PAWO kulegalega. Hafla hii inatukumbusha
kuthamini michango ya wazalendo ili kusisimus fikra zenye manufaa katika
jamii. Njozi ya Balozi Mongella ni kuona kuwa watoto wa kike wanapatiwa
haki ya elimu ili kuzalisha akina -Mongella wengi nchini. Aidha, vijana
wameaaswa kuwa na maadili na kuepuka matusi ya waziwazi katika kutafuta
nafasi za uongozi jambo linalovunja heshima na utu.
Habari Na Erasto ching’oro- Msemaji wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto


No comments:
Post a Comment