![]() |
| Abiria wakiwa wamekwama katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo jijini Dar es Salaam jana baada ya kukosa tiketi kutokana na uchache wa mabasi. |
Mamia ya abiria wamekwama kusafiri katika Kituo Kikuu cha Mabasi
yaendayo mikoani na nchi jirani cha Ubungo (UBT) jijini Dar es Salaam, kufuatia
kupanda kwa nauli na uchache wa magari uliopo hivi sasa.
Hali hiyo
ilioneka jana saa 4:00 asubuhi baada ya NIPASHE kutembelelea kituo hicho na
kushuhudia idadi kubwa ya wasafiri wanaokwenda mikoani wakiwa wamekwama huku
wengine wakiamua kupiga kambi kituoni hapo wakiwa na watoto pamoja na mizigo.
Wakizungumza
na NIPASHE, baadhi ya abiria waliokumbwa na adha hiyo hususani wale wanaosafiri
kuelekea mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Mwanza, Mara, Kagera na Kigoma, walisema
mamlaka za udhibiti na usimamizi wa usafirishaji wa abiria zimeshindwa kazi
kutokana na tatizo hilo kujitokeza kila ifikapo mwisho wa mwaka.
Walisema
kuwa mbali na kuwapo kwa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini
(Sumatra), Chama Cha Kutetea Abiria (Chakua) pamoja na Chama cha Wamiliki wa
Mabasi Nchini (Taboa), hakuna juhudi zinazoonekana kusaidia abiria.
“Kwa
kweli wananchi tunapata shida sana na hapa Sumatra wapo humu ndani tangu
asubuhi, lakini mchezo wa urushaji (kupanda) nauli upo pale pale, inafika
wakati baadhi ya abiria leo wengine wamepanda magari ya mizigo ya Fuso kwa
Shilingi 25,000 kwenda Tanga,” alisema Zuberi Abbas.
Walisema
kuwa katika kipindi cha kawaida, nauli ya kutoka Dar es Salaam kwenda Tanga ni
Sh.12,000, lakini tangu jana abiria walikuwa wanatozwa nauli ya kuanzia Sh.
25,000 hadi Sh. 40,000.
Abiria
wapatao 60 waliotarajia kusafiri jana kuelekea mkoani Mara kwa basi la ‘Musoma
Express’ walionekana wakitoa malalamiko yao Sumatra, Polisi na kwa wakala wa
basi hilo kutokana na kucheleweshwa safari yao iliyotakiwa kuanza saa 12:00
asubuhi, lakini walikuwa bado kituoni hadi kufikia saa 5:10.
Kwa
upande wa usafiri wa mabasi yaendayo mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini,
hali ilionekana kuwa shwari licha ya nauli kupanda tofauti na iliyopangwa na
Sumatra.
Mabasi ya
kutoka Dar es Salaam kwenda Iringa yamepandisha nauli kati ya Sh. 22,000 na
30,000 kutoka Sh.18,000.
Msemaji
wa Chakua, Gervas Rutaguzinda, alithibitisha kuwapo kwa shida ya usafiri kwa
abiria waendao mikoani na kusema kuwa hatua zilizochukuliwa ni kutafuta mabasi
mengine ya ziada ili kuwasafirisha.
Alisema
kuwa abiria zaidi ya 120 watasafirishwa na mabasi ya kampuni ya ‘Princess Muro’
kuelekea mikoa ya Kaskazini iliyojitolea kuwasafirisha kwa nauli iliyopangwa na
Sumatra.
“Usafiri
ni wa shida na abiria kama mnavyoona wamejaa humu ndani Ubungo, lakini kuna
mabasi mawili ya kampuni hii ambayo siyo ‘route’ yao kuelekea Arusha,
wamejitolea kusafirisha abiria hawa na watawatoza nauli ya siku zote,” alisema
Rutaguzinda.
Naye
Mjumbe wa Taboa, Mustapha Mwalongo, alisema tatizo halipo kwenye mabasi ila ni
kutokana na msimu wa mwisho wa mwaka kuwa na abiria wengi kuliko wakati
mwingine.
Alisema
kuwa walishatoa agizo kwa abiria na mawakala wa mabasi kukata tiketi za abiria
ndani ya ofisi na siyo nje ya ofisi ili kuepuka udanganyifu na usumbufu
unaoweza kujitokeza.
“Mabasi
yanayosafirisha abiria kila siku ni yale yale, ila abiria wameongezeka. Kipindi
hiki vyuo, shule, wafanyakazi wa serikalini wanapewa likizo mwisho wa mwaka,
hii inaleta msongamano mkubwa wa abiria,” alisema kisha kuongeza kuwa kungekuwa
na utaratibu wa kubadili msimu wa kufunga shule ili kupunguza msongamano huo.
Alisema
kwa hali ya sasa abiria anayetarajia kusafiri kesho yake hana uhakika wa safari
kwa kuwa hakuna kampuni yenye mabasi mengi ya kukata tiketi siku hiyo na
kuondoka.
“Kwa hapa
nchini, hakuna mmiliki wa mabasi mwenye magari ya ziada, bado hatujafikia
viwango vya nchi nyingine abiria anakatiwa tiketi ya safari ya kesho huku
analiona gari likiwa limeegeshwa, sisi ni tofauti gari linakuwa safarini siku
hiyo na lolote linaweza kujitokeza njiani kama ajali na hata kuharibika na
safari ya kesho yake isiwapo,” alisema Mwalongo.
Kamanda
wa Polisi UBT, Yussuf Kamotta, alisema wamedhibiti watu wanaosafirisha abiria
kwa magari ya mizigo hususani Fuso na kwamba wanashirikiana na Sumatra ili
kutoa vibali vya muda vya kuwasafirisha abiria ambao wamekwama kituoni hapo.
Naye Ofisa Leseni Udhibiti Sumatra, Sebastian Lehay, alisema kuwa kumekuwapo na ongezeko la abiria kila ifikapo mwisho wa mwaka na wamekuwa wakitoa ushauri kwa abiria kukata tiketi mapema.
CHANZO: NIPASHE

No comments:
Post a Comment