Pages

Monday, October 10, 2011

Bei ya petrol yashuka, dizeli yapanda


MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imetangaza bei elekezi ya mafuta itakayoanza kutumika kuanzia leo, inayoonyesha kuwa petroli  imeshuka kwa Sh38.35 wakati dizeli ikipanda kwa Sh6.95 na mafuta ya taa kwa Sh9.35.

Wiki mbili zilizopita, bei ya rejareja ya petroli ilipanda kwa Sh70.12 sawa na asilimia 3.57 wakati dizeli ilipanda kwa Sh 44.88 sawa na asilimia 2.38 na mafuta ya taa kwa Sh 33.02 sawa na asilimia 1.77.

Katika kipindi hicho, petrol jijini Dar es Salaam iliuzwa kwa  kwa Sh 2,102 kwa lita moja ikilinganishwa na Sh2,031, wiki nne zilizopita..

Kupanda na kushuka kwa bei ya nishati hiyo ya mafuta kwa lita, ni sehemu ya utekelezaji wa kanuni ya ukokotoaji inayotumiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).

Ukokotoaji huo hufanyika kutokana na kushuka kwa bei ya nishati hiyo katika soko la dunia na kushuka au kuimarika kwa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani.Hata hivyo, katika ukokotoaji huo, jana  Ewura  ilisema  bei za rejareja kwa petroli imeshuka na bei ya dizeli na mafuta ya taa, imepanda.

Bei katika baadhi ya miji mikuu

Ilifafanua kwamba, petroli imeshuka kwa Sh38.35 kwa lita ambayo ni sawa na asilimia 1.82, huku dizeli ikipanda kwa Sh16.95 kwa lita sawa na asilimia 0.85 na  mafuta ya taa yamepanda kwa Sh 9.35 kwa lita sawa na asilimia 0.48.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, bei kwa miji mikuu ikiwamo Dares Salaam, petrolil itauzwa kwa Sh2063, dizeli Sh2,016 na  mafuta ya taa Sh 1,976.

 Arusha petroli itauzwa kwa Sh 2,147 dizeli 2, 100 na mafuta ya taa Sh2,060.

Ewura ilizitaka kampuni za mafuta nchini kanza kufanya mabadiliko ya bei kwa kubandika bei mpya zinazoanza kutumika leo na kuonya kwamba, kampuni ambazo hazitafanya hivyo zitachukuliwa hatua za kisheria.


Mamlaka hiyo pia  imewataka watumiaji wa nishati hiyo kuhakikisha kuwa wanapata stakabadhi ya malipo, ambayo itatumika kama kithibitisho i cha mnunuzi kama kutakuwa na malalamiko.
Mvutano kupinga kanuni
Kanuni hiyo ya ukokotoaji iliwahi kuibua mvutano mkubwa baina ya Ewura na kampuni za kuuza mafuta nchini Agosti 2 mwaka huu.

Mvutano huo ulitokana na uamuzi wa Ewura kutangaza  kushusha bei  ya mafuta ambapo petroli ilishuka kwa Sh202.37 kwa lita ambayo ni sawa na asimilia 9.17, dizeli  ilishuka kwa Sh173.49 ambayo ni sawa na asilimia 8.32 na mafuta ya taa yalishuka bei kwa Sh181.37, sawa na asilimia 8.70.

Uamuzi huo uliibua mvutano kati ya wamiliki  wa kampuni za mafuta na serikali huku wamiliki hao wakitunisha msuli na kugoma kuuza nishati hiyo muhimu.

Lakini, Agosti 10 serikali ilitoa saa 24 kwa kampuni hizo za mafuta kutangaza kwanini yasichukuliwe hatua za kisheria kwa kukiuka agizo halali la serikali.

Ewura baadaye ilitoa onyo kwa kampuni zilizogoma ikiwemo Engen, Camel Oil, huku ikimfungulia mashtaka Mkurugenzi Mkuu wa BP, kwa kushindwa kutii amri ya kushusha bei.

Siku 11 baada ya kushusha bei na nchi kutikiswa na mgomo, Ewura ilipandisha tena bei kwa kisingizio cha kuporomoka kwa shilingi na kupanda kwa bei ya nishati hiyo katika soko la dunia.

Hata hivyo, wiki mbili zilizopita hadi kuishia jana Ewura ilitangaza kupandisha bei tena ya mafuta na kutoa.

No comments:

Post a Comment